KINAYA: Kuanzisha kituo binafsi cha polisi ni ushahidi Kenya tuna kila kitu
MSOMI, mwandishi na mwanahabari bingwa, marehemu Profesa Ken Walibora, alihimiza mno siku za uhai wake kwamba tusivizuie vipawa.
Hata hivyo, hakurejelea vipawa vya ajabu kama vile watu binafsi kuanzisha vituo vyao vya polisi na kujasiria kuviremba kwa rangi rasmi.
Kenya kuna watu wabunifu! Usicheze na nchi ambayo iliwahi kuwa na ‘yesu’ wake! Usijifanye humkumbuki ‘Jehovah’ Wanyonyi, mzee aliyejifanya mwokozi wetu kwa miaka mingi kisha akaaga dunia na ‘kurejea kwake’.
Mtu anapojiita ‘yesu’, akifa anakwenda wapi? Nadhani anaamini anarejea kwake, kwani Wakristo wanaamini wakiondoka duniani watakwenda kwa Yesu wa kweli.
Wafuasi wa ‘Jehovah’ Wanyonyi walisubiri afufuke siku ya tatu, mwili ukaingia baridi, wakatambua kuwa mzee aliwacheza shere muda huo wote, wakamzika kimya-kimya na kwa aibu kubwa.
Ama nchi hii tuna mchezo sana, tumekuwa kichaa, au tumekolea ubunifu kiasi cha kuisaidia serikali kutatua matatizo mengi.
Nchini Kenya, kujiajiri pia ni kuisaidia serikali kwa sababu imekataa kukuajiri, na wala haijakubunia mazingira rafiki ya kujiajiri.
Kimsingi, unang’ang’ana na ugumu wa maisha mpaka unapata wazo la kukufaa. Wengine wakifaidika katika harakati hizo ni sawa tu hata ikiwa hukukusudia kuwafaa.
Kila mtu anajaribu kuwa hai siku inayofuata tu. Matumaini yameshuka. Serikali yenyewe haijui vijiji vingi, kwa hivyo hata mnaoita haiwajui wazee rasmi wa vijiji.
Akitokea mtu na Sh2,000 na ushei, aamue kubadili mambo yalivyo huko, atakumbatiwa na watawala, na hata polisi.
Ushirikiano wa aina hiyo si jambo ngeni, ndiyo maana nawasuta wanafiki wanapoona ajabu kwamba kijana wa miaka 26 ameanzisha kituo cha polisi kijijini kwao.
Kabla ya kuropoka, jaribu kuulizia mara ya mwisho serikali ilifika lini kijijini huko kushughulikia matatizo ya wakazi.
Watu wamezaa shujaa, amechoshwa na maisha duni ya kijijini, ametoa mia tano zake kununua rangi ya maji, akatafuta msanii akachora ngao ya polisi na kupaka rangi itakiwavyo, nawe unapiga domo tu.
Umesaidia kijiji chenu na nini?
Angaa kijana wa watu ana mawazo mapana. Ni sahihi kusema anaishi kijijini na mawazo ya uzunguni ambako jela na magereza huwa majengo watu binafsi, serikali hulipa wenyewe kodi za nyumba.
Kasongo hudai kufanya mambo upesi; hebu na akifanye rasmi kituo hicho cha polisi, tena awaruhusu watu binafsi waliochoshwa na utovu wa usalama kuanzisha vituo vingine kama hivyo kote nchini.
Kenya ina madanguro mengi sana ambayo hayana faida yoyote, mbona tusiyapake rangi za polisi, za mtoza ushuru (KRA) na za Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) ili tushughulikie mambo madogo yanayotuudhi kila siku?