Jamvi La Siasa

Kinaya: Mlima hauziki ndovu na pembe zake

Na  DOUGLAS MUTUA March 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NDOVU anasubiriwa mlimani! Hivi akienda atafanikiwa kuukwea mlima, au una utelezi unaoweza kumbwaga hadi chini?

Akwee asikwee mlima, wenyeji wa eneo hilo wanasema, “Ndovu hazikwi na pembe zake.” Ni msemo tulioachiwa na wahenga, lakini sasa umekuwa maarufu sana katika mazingira ya kisiasa.

Kimsingi msemo huo unamshauri mtu asiwe zuzu wa kukataa fursa ya kunufaika inapojiri, aelewe vya kutupa na vya kusaza.

Mjadala mkubwa umetokea katika janibu hizo, watu wakiulizana iwapo ni vyema kumkaribisha ndovu na maguu yake makubwa, hata baada ya kuvamia mashamba yao na kuharibu mimea.

Siri iliyo wazi ni kwamba ndovu hapendwi tena mlimani, na sidhani atawahi kupendwa kamwe. Kwa hivyo? Aende tu, litakalotokea litokee.

Binafsi ukiniuliza nitakwambia ndovu anapaswa kwenda mlimani saa hii, tena kwa kasi ya kupigiwa mfano, kwa sababu hakuna wakati utakaokuwa bora zaidi kwake kuwazuru wakazi.

Ingawa kuna pande mbili za mjadala huo, wote wanakubaliana kwamba pembe za ndovu ni za thamani kubwa, hazipaswi kuzikwa watakapoandaa mazishi yake.

Natumai ndovu mwenyewe anajua kuwa wajinga ndio waliwao. Huenda anajua, lakini nina shaka naye kwa kuwa kawaida yake anapenda kuonyesha maguvu aliyonayo, ukubwa wa mwili wake, uzito wa nyayo zake.

Kwake kwenda mlimani si hoja, atakwenda tu hata ikiwa atauzunguka wote na kuacha pembe zake huko, wenyeji wazigawane huku wakimcheka na kuambiana hawawezi kumpa hata jani moja la mchicha!

Hata hivyo, sijui atatumia mbinu gani kuwasadikisha wasimwite ‘Kaongo’ kwa sababu mara ya mwisho alipozuru huko alitoa ahadi nyingi tu ambazo bado hajatimiza.

Ajabu, ahadi za uongo zinazowakera si za maendeleo. Wana tatizo na marafiki zake wapya, hasa hawamtaki wala kumtambua mke-mwenza anayetokea ziwani!

Wanauliza: “‘Kaongo’ anawezaje kutudanganya kwamba hatamgawia mtu mkate wetu hata kipande kimoja wala kumnusisha harufu, halafu anafanya hivyo na kuponda watoto wetu kwa unene wa maguu yake?”

Wanajua ndovu anaweza kutumia unene wake kupasua msitu wowote mara kadha na kuwaachia njia za kupitia.

Inayowaudhi sana ni ile njia ya y ambayo ilianzishwa na ndovu aliyemtangulia ndovu wa sasa kwa sababu huyu mpya aliahidi kupitia hapo na kuhakikisha panapitika na kila mtu, ila inajiotea magugu ovyo.

Mradi anaahidi kukata njia, na pembe zake zote anazo, mlimani wanaamini pembe zenyewe zitaanguka siku moja waokote na kujinufaisha. Laiti zingepasulika vipande kama mihogo au muwa, wangejichukulia kwa wingi wa mikono yao!

Ndovu hapendi masihara, kwa hivyo ni lazima wamwendee kwa makini sana. Wanajua akishuku tu kwamba wanachotaka ni pembe zake, kamwe hawampendi, anaweza kuchemka kwa hasira na kupita na mtu!

Nimwambie ndovu ukweli kabla hajakwenda huko kesho au niache…?