KINAYA: Zakayo, kukomesha Wakenya si kuwafokea, ni kuwapa ukweli na ithibati
UKIACHWA, achika. Ukichengwa, chengeka. Na ukishindwa, shindika. Kimsingi, kubali yaishe. Kwani Zakayo hajui ukweli huu?
Angali anateta kuhusu mikataba yake na kampuni ya Adani Group, ambayo tulimshinikiza mpaka akaifutilia mbali ilipobainika kwamba mbia wake huyo amefunguliwa mashtaka ya ufisadi Amerika.
Sasa tumejua Zakayo alifuta shingo upande mikataba hiyo ya kujenga na kusimamia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomko Kenyatta (JKIA) na mingineyo.
Ukikutana naye, mwambie akubali kwamba Wakenya walio macho wamempiku kwa ujanja, wamemwonea maguu kumi na manane, janja zake na mitego ya kila aina itateguliwa upesi.
Anapopanda jukwaani kutuita wasaliti wasioipenda nchi yao, kisa na maana hatutaki aitawale nchi yetu kama anavyoweza kuisimamia biashara binafsi ya kuuza kuku, hafai kunung’unika.
Hatumchukii kamwe, tunachukia tabia zake. Alipaswa kujua hata kabla ya kuamua kuwania urais kwamba Wakenya si wapole, tena hawapendi amani iwapo itapatikana kwa gharama ya manyanyaso.
Nchi hii ni yetu, itatawaliwa tunavyotaka. Kanuni ni wengi wape, lau sivyo wachukue kwa wingi wa mikono yao. Hilo lisipomwingia akilini, basi ana uhuru wa kujiengua, tumshangilie kama mstaarabu aliyejiuzulu kama Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania.
Vilevile, anaweza kuamua kutotetea wadhifa wake ifikapo mwaka 2027, lakini namshauri aifiche siri hio ili tusiingie wazimu tukishangilia uamuzi huo. Wakenya hatuli kiapo cha uaminifu kwa kiongozi yeyote, akifanya ya hovyo tunampungia mkono ama aache au tumwachishe.
Zakayo anachekesha, na kuudhi wakati mwingine, kwa kuonyesha wazi kwamba anapendelea kushirikiana kikazi na raia wa India au watu wenye asili ya nchi hiyo hata wakati ambapo Wakenya wanamshinikiza kutofanya hivyo.
Je, umewahi kujiuliza kwa nini baadhi ya vibonzo humsawiri akiwa na kilemba cha kalasinga? Michoro hiyo ilianzia katika kashfa ambapo, akiwa naibu rais, alihusishwa na unyakuzi wa ardhi ya shule iliyo karibu na hoteli yake ya Weston.
Alikanusha vikali kumiliki ardhi hiyo, akadai kuwa inamilikiwa na Mhindi fulani kwa jina Singh, wajanja wanaoitwa Wakenya wakafanya uchunguzi na kujua ukweli wa mambo. Tangu hapo kilemba hakijamtoka kichwani! Na akiudhi anaitwa jina la msimbo: ‘Singh’.
Inachekesha anapotukasirikia na kututukana kwa kushuku kwamba ana maslahi binafsi katika kampuni ya mabati ya Devki ambayo pia inamilikiwa na Wahindi.
Njia rahisi ya kuwaambia Wakenya wakukome si kuwakasirikia na kuwatukana, ni kuwaambia ukweli unaoambatana na ithibati, wasipokuamini uwaambie wakushtaki, halafu ufyate domo na kuendelea na kazi zako.
Vinginevyo, watakuchokoza, wakutukane, wakuaibishe na hakuna kitu ambacho utawafanyia. Hata hivyo, ikiwa una nguvu na muda, ingia kwenye tope upigane miereka na nguruwe, tuone mwishowe utafaidikaje.
Usisahau kuwa kwa matusi na maudhi ya mtandaoni, Wakenya ni mashetani! Barani Afrika wanashindana na raia wa Nigeria pekee, tayari wamekwisha kuwakomesha raia wa mataifa mengineyo waliothubutu kuwakabili. Wanaona raha wanapokutukana halafu unakasirika.
Ukimwona Zakayo mwambie asitukasirikie, ni hulka yetu kuwachokoza viongozi, hasa tunapohisi kwamba kuna kiza katika kutekeleza mradi wowote wa serikali. Na kawaida yetu hatuombi msamaha.