Kiunjuri: Dereva wa lori aliyegeuka mwanasiasa shupavu nchini
ALIPOJITOSA katika siasa, Festus Mwangi Kiunjuri alionekana na wengi kama limbukeni tu. Lakini hii iligeuka kuwa tofauti.
Katika chuo kikuu alikuwa kiongozi shupavu wa wanafunzi, jambo ambalo pengine liliunda ushujaa wake wa baadaye katika kisiasa.
Kiunjuri alisomea Shahada ya Kwanza ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Egerton na kuhitimu mwaka wa 1994. Ingawa alifundisha kwa miaka michache baada ya kuhitimu, mawazo yake yalikuwa yameelekezwa kwenye jambo lingine.
Baada ya muda alinunua lori kuukuu na kujitosa katika biashara ya usafiri katika Mji wa Nanyuki, akifanya kazi kama dereva na makanga. Aliendesha gari kutoka kituo kikuu cha mabasi cha Nanyuki ambapo alitumia muda wake mwingi wa mapumziko kujadili siasa na wenyeji.
Kuanzia hapa ndipo alipoanza kuchangamkia wazo la kujiunga na siasa za kitaifa.Kwa sababu alijulikana sana Nanyuki, alipata imani ya wenyeji wengi katika eneo hilo.
Hakuzungumza lugha yao pekee bali pia alichanganyikana nao kwa uhuru licha ya kuwa na elimu ya chuo kikuu. Huenda hilo lilitokana na malezi yake. Babake alifanya kazi katika zahanati katika eneo la Msitu wa Kahurura huko Kieni, Kaunti ya Nyeri, huku mamake akiwa mama wa nyumbani ambaye aliyejishughulisha na ukulima.
Kwa hakika, Kiunjuri, mtoto wa 11 kati ya 12, alivaa jozi lake la kwanza la viatu alipofika Darasa la Nne. Kiunjuri alizaliwa Aprili 29, 1969 na kusomea Shule ya Msingi ya Kahura na baadaye akajiunga na Shule ya Wavulana ya Dkt Kiano na Shule ya Upili ya Kangema kwa elimu ya sekondari. Katika miaka yake yote shuleni, alijulikana kwa kufanya kazi kwa bidii kwani aliazimia kuleta mabadiliko katika maisha yake.
Akiwa mwanafunzi wa chuo kikuu alikuwa akifanya biashara ya kuuza nguo na mboga. Alipata mboga hizo kutoka Kinangop, ambako zilikuwa za bei nafuu na kwa zilipatikana kwa wingi na kuziuza huko Githurai jijini Nairobi. Hii ilimsaidia kufadhili elimu yake. Biashara ya usafiri ilikuwa tu onyesho lingine kwamba haogopi kazi ngumu.
Kuongeza ujuzi wake wa kuongea na umilisi wa lugha ya Gikuyu — si ajabu wenyeji wa Nanyuki waliona ndani yake kiongozi chipukizi.Hata hivyo, wanasiasa wakongwe na wenye uzoefu zaidi huko Laikipia walimkataa kutokana na ulimbukeni wake na kumchukulia kama makanga tu ambaye hakuwa na nafasi ya kuingia katika siasa.Ilikuwa ni jambo lisilowezekana kwao kwamba makanga angeweza kuwa Mbunge.
Wakati huo, chama cha Democratic Party kilikuwa maarufu sana katika eneo la Mlima Kenya na vigogo wa kisiasa walitaka Mwai Kibaki, kiongozi wa chama aingilie kati ili Kiunjuri asipate tikiti ya chama hicho. Lakini walikuwa wamepuuza azma ya Kiunjuri, jambo ambalo liligeuka kuwa kosa kubwa.
Baadaye, aliwajibu wapinzani wake hivi: “Niliposhinda tiketi ya DP (katika mchujo), matajiri walitaka Mwai Kibaki asikubali. Walipopeleka malalamishi yao kwake, Kibaki aliwaambia kwamba ikiwa Nanyuki ilikuwa na makanga wengi, ilikuwa ni haki kwamba mmoja wao awawakilishe. Hivyo ndivyo nilivyoingia bungeni.”
Kiunjuri alitupa kofia yake katika ulingo wa kisiasa mwaka wa 1997. Wapinzani wake walikuwa na nguvu ya kifedha huku yeye akiwa masikini. Hakuweza hata kumudu Sh50,000 zilizohitajika kama ada ya uteuzi na alilazimika kuuza lori lake ili kupata pesa hizo.
Alipitia mazingira magumu ya kisiasa kwa ushupavu. Wananchi wa eneobunge la Laikipia Mashariki walimtuza kwa kumchagua Bungeni kwa tikiti ya Chama cha DP. Alikuwa na umri wa miaka 28 tu.
Alikuwa mzuri sana katika kujieleza hivi kwamba mnamo 2017 Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi, alisema: “Niliwahi kumwambia Rais, ‘Ikiwa kuna mtu mmoja tunaweza kutegemea kueneza habari kwa watu wetu, kwa sharti kwamba haongei Kiswahili wala Kiingereza, ni Mwangi Kiunjuri. Mtu huyu ana kipaji. Mpe kipaza sauti na azungumze kwa Gikuyu. Mheshimiwa Rais, mtu huyo ni mzuri.’”
Bungeni Kiunjuri alijitofautisha kama mdadisi asiye na woga, akipambana bila huruma na wanasiasa wenye uzoefu zaidi. Mnamo 2002 na 2007 alichaguliwa tena kuwa Bunge, wakati huo alikuwa amejipambanua kama mzito wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya.
Mwanamume ambaye alikuwa amepuuzwa sana mwanzoni mwa taaluma yake ya kisiasa akawa mtu wa kushawishi katika siasa za eneo la Kati mwa Kenya. Katika muhula wa kwanza akiwa mbunge aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji.
Mwanasiasa machachari, Kiunjuri alijijenga akawa katika kundi la wanasiasa ambao wanaweza kushawishi umati wa watu kwa maneno matupu bila kutoa njia yoyote ya kutekeleza ahadi zake.
Ujuzi wake wa kuzungumza na nguvu za ushawishi zilionekana kuwa zote alizohitaji ili kujijenga kisiasa. Hata hivyo, sifa hizi hazimkumfaa mwaka wa 2013, alipogombea ugavana Kaunti ya Laikipia kwa tiketi ya Chama cha Grand National Union Party. Wakati huo alikuwa nje ya mawimbi ya kisiasa kwani chama cha Uhuru Kenyatta cha The National Alliance (TNA) kilikuwa na nguvu kubwa katika eneo hilo. Alishindwa katika kinyang’anyiro hicho na Joshua Irungu, mgombeaji wa TNA.
Kiunjuri baadaye alisema, “Nilikuwa nishinde kiti cha Laikipia siku chache kabla ya uchaguzi. Kisha Uhuru akatua na chopa zake nyekundu na mambo yakabadilika haraka sana.”
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA