Maseneta walivyopuuza kuugua ghafla kwa Gachagua na kuendeleza mchakato wa kumtimua
MASENETA Alhamisi walikataa kumhurumia Naibu Rais Rigathi Gachagua na kuendelea na mchakato wa kumtimua mamlakani licha ya kufahamishwa kuwa aliugua ghafla na kulazwa hospitalini.
Hadi wakati wa kuandika taarifa hii Alhamisi usiku, maseneta walikuwa wakiendelea kujadili mashtaka dhidi ya Bw Gachagua aliyekuwa amelazwa hospitalini.
Maseneta hao walikosa kumhurumia licha ya mawakili wake kufahamisha Seneti kwamba alilalazwa hospitalini baada ya kuugua ghafla na hangeweza kufika kuhojiwa na mawakili wa Bunge la Kitaifa.
Maseneta hao walipokuwa wakijiandaa kupiga kura jana usiku, familia ya Gachagua iliruhusu daktari wake kuthibitisha kuwa alikuwa amelazwa hospitalini akiwa na maumivu ya kifua.
“Naibu Rais yuko hapa. Alilazwa mwendo wa saa tisa mchana akilalamikia maumivu ya kifua na kwa sasa anafanyiwa vipimo,” akisema Dkt Dan Gikonyo wa Hospitali ya Karen, Nairobi.
Wabunge na washirika wake wa karibu waliofika katika hospitali, akiwemo mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba walisema hawakuruhusiwa kumuona Bw Gachagua hospitalini.
Bw Gachagua alikabiliwa na mashtaka 11 ambayo wiki jana yalipitishwa na Bunge la Kitaifa kwa kuungwa na wabunge 282.
Awali, mwendo wa saa kumi na moja alasiri, bila chembe ya huruma, maseneta walikataa hoja ya kuahirisha kikao hadi Jumamosi kumpatia muda wa kupata nafuu na wakaendelea na mchakato wa kumtimua wakisema ulikuwa ni muda uliowekwa na katiba.
Spika wa Seneti Amason Kingi alikuwa amewataka maseneta kuamua iwapo walitaka kuahirisha kikao au kuendelea na mchakato na kuukamilisha jana.
Mawakili wa Bw Gachagua, wakiongozwa na Paul Muite walikataa kuendelea na kikao jana alasiri bila uwepo wa Bw Gachagua maseneta walipokataa kuahirisha kikao hivyo nao wakaondoka.
Kikao cha adhuhuri kilivurugika kwa saa kadhaa baada ya Bw Gachagua kukosa kufika kuhojiwa na mawakili wa Bunge la Kitaifa wakiongozwa na Bw James Orengo na Otiende Amollo.
Hali hiyo ambayo haikutarajiwa ilimfanya Spika Amason Kingi kuahirisha kikao hadi saa kumi na moja jioni kuruhusu mawakili wa Naibu Rais, wakiongozwa na wakili mkuu Paul Muite, kumtafuta mteja wao.
“Ukweli wa kusikitisha ni kwamba, Naibu Rais ameugua na hivi ninavyozungumza yuko hospitalini, pendekezo langu ni kwamba, mnipe muda niangalie hali yake na nirudi hapa saa kumi na moja jioni baada ya kumuona,” aliongeza.
Bunge liliporejelea kikao saa kumi na moja jioni, Bw Muite aliomba kikao hicho kiahirishwe hadi Jumanne wiki ijayo, akisema Naibu Rais alikuwa na maumivu makali ya kifua na alihitaji kupumzika kwa sasa.
“Niliweza kuwasiliana na madaktari wa Hospitali ya Karen wanaomhudumia Naibu Rais, kutokana na hali yake, sikuweza kuzungumza naye moja kwa moja kwa ushauri wa daktari wake,” Bw Muite alisema.
Mawakili wa Bunge la Kitaifa walihoji kuwa kutokuwepo kwa Bw Gachagua hakungeweza kuzuia mchakato uliowekewa muda kikatiba hadi Jumanne walivyoomba mawakili wa naibu rais.
Walisisitiza kuwa mchakato wa kumuondoa mamlakani ni wa kisiasa na sio lazima madai dhidi ya Naibu Rais yathibitishwe kikamilifu.
“Kusikilizwa si lazima kuwe kwa maneno. Kanuni za Bunge hili zinaruhusu wanaoshtakiwa kuwakilishwa, kuonekana kibinafsi au kuwasilisha hati,” alisema wakili wa Bunge la Kitaifa Eric Gumbo.
“Mchakato huu sio kuhusu hali ambayo Naibu Rais amejipata, ni kuhusu Seneti kuzingatia masharti ya Katiba ambayo lazima ifanye uamuzi ndani ya muda fulani,” aliongeza Wakili Orengo.
Hata hivyo, ushawishi wa hali ya juu wa kisiasa na idadi kubwa ya maseneta waliounga mchakato huo ulizima nyota ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kukataa kumhurumia licha ya kufahamishwa alikuwa mgonjwa na wakaunga kutimuliwa kwake ofisini na Bunge la Kitaifa.
Gachagua alikabiliwa na mashtaka kumi na moja katika hoja iliyowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Bw Mwengi Mutuse yakiwemo kubagua baadhi ya jamii na maeneo kwa kudai serikali ni ya wenye hisa, kupuuza kiapo cha afisi, kutumia vibaya afisi na mamlaka yake, ufisadi na ulanguzi wa fedha.
Mengine ni kudharau na kukinzana na rais, kuingilia ugatuzi kwa kupinga kuhamishwa kwa wafanya biashara jijini, utovu wa nidhamu uliokithiri, ikiwa ni pamoja na kushambulia Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi, kuwatisha maafisa wa umma, na kushawishi vitendo vya ufisadi na uhalifu wa kiuchumi.