Mbadi ateta Uhuru alimtupa Raila
Rais William Ruto alipokuwa akimtembeza mtangulizi wake Uhuru Kenyatta katika Ikulu Ijumaa, mjadala uliibuka kuhusu ikiwa rais huyo mstaafu bado ana ushawishi wa kisiasa wa kuathiri matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2027.
Waziri wa Fedha, Bw John Mbadi, ndiye aliyeanzisha mjadala huo kwa kusema kuwa Bw Kenyatta hawezi kumshauri yeyote kuhusu uchaguzi, akidai alimuacha Kiongozi wa ODM Raila Odinga katika wakati mgumu kwenye uchaguzi wa Agosti 2022.
Mbadi alisema kwamba ni vyema chama cha ODM kiendelee kushirikiana na UDA bila kumhusisha Bw Kenyatta katika mazungumzo ya kisiasa.
Aliendeleza hoja hiyo kwa kusema kuwa Kenyatta hana uwezo wa kumfanya Waziri Mkuu wa zamani kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, akimlaumu kwa kuwadanganya wafuasi wa ODM kwa matumaini ya uongo walipokuwa karibu sana kisiasa kutwaa urais kupitia handisheki.
“Alituhadaa kwamba atatupa urais alipokuwa na mamlaka yote ya nchi. Lakini mbele ya macho yetu, alimkabidhi mamlaka Rais Ruto,” alisema Bw Mbadi.
Akizungumza Ijumaa wakati wa harambee ya kusaidia wajasiriamali wa jua kali huko Ndhiwa, Kaunti ya Homa Bay, Bw Mbadi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa ODM kwa muda mrefu alidai kuwa wanasiasa kutoka Mlima Kenya wamekuwa wakitelekeza wagombeaji wa urais kutoka eneo la ziwa, hasa Bw Odinga.
Aliwataka wakazi wa Nyanza kuunga mkono serikali ya Kenya Kwanza.“Sisi tumeunda ushirikiano na ndugu zetu (UDA). Hatuna nia ya kuachana nao hata baada ya 2027.
Wameonyesha kuwa ni watu wanaoweza kutuunga mkono,” alisema.Kwa mujibu wa Mbadi, rais mstaafu Kenyatta amekuwa akiwasiliana na Bw Odinga na timu yake akiahidi kuwasaidia kushinda urais.
Alidai kuwa Kenyatta ameahidi kuhakikisha Bw Odinga anashinda urais.Lakini alisema ahadi hiyo haina uzito wowote kwa kuzingatia historia ya kisiasa.
“Alikuwa na mamlaka lakini hakutupa urais. Atawezaje kufanya hivyo sasa ambapo Ruto ndiye mwenye mamlaka?” alihoji.Mbadi alisisitiza kuwa serikali jumuishi itaendelea kuwepo hadi uchaguzi ujao na baadaye.
“Watu wetu wafahamu kuwa ODM na UDA zinashirikiana, na hatutarajii kikwazo chochote. Tutaendelea kushirikiana hadi baada ya 2032, na wakati pekee ambapo hatutamuunga mkono Rais Ruto ni iwapo ataamua mwenyewe kuachia Raila kiti hicho, kwa kuwa yeye ndiye wa mwisho kutoa uamuzi,” alisema Mbadi.
Harambee hiyo iliwaunganisha viongozi kutoka maeneo mbalimbali ya eneo la ziwa.Waliohudhuria ni pamoja na Kiranja wa Wachache Bungeni Millie Odhiambo, Martin Owino (Ndhiwa), Lilian Gogo (Rangwe), Samuel Atandi (Alego Usonga), James Nyikal (Seme) na Johana Ngeno wa UDA kutoka Emurua Dikir – wote wakiahidi kumuunga mkono Rais Ruto.
Bi Odhiambo alisema kuwa ODM inaunga mkono serikali, lakini bado wanapima iwapo wataendelea na msimamo huo hadi uchaguzi wa 2027.
Mbunge huyo wa Suba Kaskazini alisema ushirikiano wao na Rais Ruto haujasema rasmi utaendelea baada ya uchaguzi wa 2027.Alisema ODM inaweza pia kumwidhinisha mgombeaji wake wa urais katika uchaguzi ujao.
Alimtaja Bw Odinga kama mgombeaji wao kutokana na juhudi zake za kuhakikisha taifa linabaki na uthabiti wakati wa misukosuko.
“Tulipitia nyakati ngumu na niliona Raila Odinga akiwa karibu kuuawa. Hakuna anayeweza kumlaumu kwa kufanya uamuzi wa kuweka nchi mbele ya chochote kile. Tumekubaliana kuwa kwa ajili ya kuleta uthabiti wa taifa, tusimame na mpango huu wa serikali jumuishi hadi 2027,” alisema Bi Odhiambo.
Mbunge huyo aliongeza kuwa chama cha ODM kinaweza pia kumuomba Rais Ruto kumuunga mkono Bw Odinga katika uchaguzi ujao wa urais.“Ni suala la majadiliano,” alisema.Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022, Bw Odinga na Bw Kenyatta walikuwa washirika wa karibu dhidi ya Dkt Ruto, aliyekuwa Naibu Rais wakati huo.
TAFSIRI: BENSON MATHEKA