Mikakati ya upinzani kukabili Ruto yaiva
VIGOGO wa muungano wa upinzani wako mbioni kuupanua zaidi, kumtangaza mgombea mmoja wa urais mapema, kupinga maamuzi ya serikali kandamizi mahakamani, na kuimarisha ujumbe wa kupinga serikali kwa kuwasilisha sera mbadala zenye msingi wa kweli kama sehemu ya mkakati wa kushawishi Wakenya mwaka huu.
Kwa kutambua kwamba uchaguzi si tu kuhusu kupiga kura, na kutokana na shambulio la mara kwa mara la Rais William Ruto kwamba wapinzani wake hawana lolote bali maneno tu yasiyo na maana, vigogo wa muungano huo wanaonekana kupanga kampeni zao mapema.
Kwa viongozi wa upinzani, mwaka wa 2026 ni wa kuamua iwapo utafaulu au kushindwa 2027 wakiangazia mshikamano, uthabiti na mkakati vitakavyobainisha iwapo Rais Ruto atakabiliana na tishio halisi katika uchaguzi wa mwaka ujao.
Huku Dkt Ruto akisisitiza kwamba mwaka huu utakuwa wa utoaji wa huduma na utekelezaji wa miradi, upinzani unasema badala yake mwaka huu utaanika kile wanachoita urais uliojengwa juu ya ukwepaji sheria, miradi iliyoongezewa bei na udhaifu wa taasisi za umma.
Wachambuzi wa siasa wanasema ni mkakati na si maneno tu utakaobainisha umuhimu na nguvu za upinzani.
Rais Ruto amekuwa akiwasawiri wapinzani wake kama watu waliopoteza akili na wasio na ajenda.
Lakini mahojiano na viongozi wakuu wa upinzani na wachambuzi wa yanaashiria kuwa vinara hao wana mpango wa kina unaolenga kudhoofisha hadithi za ufanisi za serikali huku ukipanga upinzani kama serikali inayosubiri kutwaa mamlaka katika uchaguzi wa 2027.
Mpango wa upinzani wa mwaka 2026 unategemea mshikamano wa mapema, nidhamu katika ujumbe wanaowasilisha, mapambano ya kisheria na uwezo wa kutafsiri hasira za wananchi kuwa maono ya serikali mbadala yenye msingi wa kweli.
Taifa Jumapili imebaini kwamba upinzani umeweka hatua kuu zikiwemo; mapambano makali ya kisheria mahakamani dhidi ya kile wanachoita maovu ya serikali, kuhamasisha wananchi kuanzia wadi hadi ngazi ya taifa, na kuchambua ufisadi uliofichuliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Mdhibiti wa Bajeti.
Kuu katika mkakati wao, ni kutangaza mapema mgombea mmoja wa urais, ikifuatiwa na kampeni ya kitaifa iliyoratibiwa kumvumisha mgombea huyo.
Baadhi ya wanasiasa wa upinzani wamependekeza wazo la mkutano wa viongozi wa juu wa upinzani mwanzoni mwa mwaka 2026, kuwaleta pamoja viongozi muhimu wa upinzani, wakiwemo wale walioko nje ya Muungano wa Upinzani kama Jaji Mkuu mstaafu David Maraga, Seneta wa Busia Okiya Omtatah na kiongozi wa Safina Jimi Wanjigi.
“Ni muhimu kuleta upinzani wote chini ya mwavuli mmoja,” alisema mmoja wa vigogo hao.
Aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua ambaye sasa anachukuliwa kama kiongozi wa upinzani anasisitiza kwamba Muungano wa Upinzani hautaruhusu Rais Ruto kuwaamulia ajenda.
“William Ruto hawezi kutushauri jinsi ya kumtoa madarakani, na hatuwezi kumruhusu atuamulie ajenda. Anapaswa kushangilia kwa kusema hatuna ajenda, tumepotea na hatuna akili,” alisema Gachagua katika mahojiano na Taifa Jumapili.
Aliongeza: “Watu kama hawa hawatutishi, na mtu anaweza kujiuliza kwa nini wanahangaika na watu wasio na maana.”
Kiongozi wa chama cha Democratic Party, Justin Muturi, mmoja wa viongozi wa Muungano wa Upinzani, alisema “Tutamtangaza mgombea wetu wa urais hivi karibuni.”
Kauli yake ilifuata ya kiongozi wa Wiper Patriotic Front (WPF) Kalonzo Musyoka kwamba Muungano wa Upinzani utamtangaza mgombea wake wa urais kufikia Machi mwaka huu.
“Ninaweza kusema bila woga kwamba mgombea wetu wa urais atajulikana hivi karibuni. Ni suala tulilokuwa tukilijadili. Huenda bado hatujaafikiana kuhusu tarehe ya kumtangaza lakini tuko mwelekeo sahihi,” alisema Muturi.
Aliongeza: “Maslahi ya taifa lazima yawe ya kwanza, na lazima tuwe tayari kutema maslahi yetu binafsi ili kuokoa nchi hii.”
Viongozi wa upinzani wanakiri kwamba kutegemea hasira za wananchi pekee hakutoshi na kwamba watatoa ruwaza yao ya uchumi.
Sehemu wanazozingatia ni gharama ya maisha, ushuru, usimamizi wa deni na kuunda ajira.
“Serikali inatueleza kuhusu utulivu wa uchumi, lakini wananchi hawauoni,” alisema mmoja wa wanamikakati wa Muungano wa Upinzani. “Kazi yetu mwaka 2026 ni kuonyesha kuwa maumivu haya si bahati mbaya, ni matokeo ya chaguo mabaya.”
Wachambuzi wanasema muda ni kila kitu.
“Iwapo mazungumzo ya mshikamano yatachukua hadi mwisho wa 2026, uharibifu tayari utakuwa umefanyika,” alisema Prof Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multimedia. “Upinzani haushindwi uchaguzini kwa sababu ya idadi. Ni kwa sababu ya kutokuwa na mshikamano.”
Zaidi ya mshikamano, mpango wa upinzani unalenga kuonyesha maumivu ya wananchi. Badala ya kujadili ukuaji wa Pato la Taifa au usimamizi wa fedha, viongozi wa upinzani wanapanga kupeleka hoja zao katika kaunti, masoko, hospitali na shule.
Seneta wa Kitui Enoch Wambua wa Wiper Patriotic Front alipuuza madai ya Rais kwamba upinzani huna mwelekeo.
“Iwapo mambo yangekuwa bora, Wakenya wangeyahisi,” alisema. “Hatuwezi kuambiwa uchumi unaonekana kuimarika.”
Hata hivyo, Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru anapuuza mipango ya upinzani.
“Hauonekani kuwa na mpango makini zaidi ya ukosoaji na tamaa ya kubadilisha serikali ya sasa. Kwa upande mwingine, Serikali ya Kenya Kwanza inaonekana kuwa na mpangilio wa kina kuhusu uchumi, afya, kilimo, miundombinu na elimu, masuala yanayowaathiri zaidi wapiga kura wa Kenya,” alisema.