Jamvi La Siasa

Mikakati yasukwa kumzima Gachagua kuelekea 2027

Na  MWANGI MUIRURI July 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MIONGONI mwa viongozi wa upinzani walioungana wakilenga kumwondoa Rais William Ruto mamlakani baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 2027, hakuna anayekumbwa na upinzani mkali kama aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Rais Ruto mwenyewe, naibu wake Profesa Kithure Kindiki, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Bw Kimani Ichung’wa, baadhi ya mawaziri, pamoja na marafiki wa karibu wa Rais, wote wanapambana na Gachagua kisiasa.

Gachagua amejiunga na viongozi wa upinzani akiwemo kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i, kiongozi wa chama cha People’s Liberation Party Martha Karua, na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, kuunda muungano kuelekea 2027.

Uhasama dhidi ya Gachagua kutoka kwa Rais Ruto na hata wandani wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta umefikia kiwango cha juu kiasi cha kumfanya Gachagua kutoa kilio cha dharura.

Akizungumza kupitia Pacific TV akiwa Amerika ambako yuko hadi Agosti, Gachagua alisema: “Mtu mmoja anaandamwa na vikundi zaidi ya kumi.”

Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi alikosoa ziara hiyo ya Gachagua Amerika, akiitaja kuwa “ukabila uliosafirishwa nje ya nchi, ambako anawahutubia watu kwa lugha ya mama”.

Lakini Gachagua alisisitiza kuwa “mtu yule yule waliyemtimua ofisini mwezi Oktoba mwaka jana amekataa kuzama kama walivyotamani, na sasa wanahangaika kunivunja kisiasa”.

Amedai kuwa eneo la Mlima Kenya kuna shughuli zinazoratibiwa kupambana naye.

Eneo hilo, ambalo lilimpigia kura Rais Ruto kwa asilimia 87 mwaka wa 2022, sasa limechaguliwa kama uwanja wa kupambana na Gachagua, jambo ambalo linatafsiriwa kama juhudi za kulirejesha kambi ya Ruto.

Gachagua, kwa upande wake, anajaribu kuunganisha eneo la Mlima Kenya na pia kuanzisha ushirikiano na maeneo mengine ili kuhakikisha Rais Ruto anahudumu muhula mmoja tu wa miaka mitano, badala ya miaka 10 inayoruhusiwa na Katiba.

Rais Ruto na serikali yake ndio walio hatarini zaidi endapo Gachagua atafaulu na Serikali imeanzisha mikakati ya kumdhibiti Gachagua, ikiwemo kuhusisha wanachama wa Jubilee, kupanga wafuasi wa Ruto, kugawanya kura, na kuhusisha Wizara ya Usalama.

Pia, wanablogu wameachiliwa kumuumbua Gachagua, huku baraza la mawaziri, wanamuziki, wachekeshaji na hata baadhi ya viongozi wa dini wakihusisha kumpiga vita.

“Ni kweli tuna mpango wa kumkabili Bw Gachagua. Mpango huo umekuwa kwenye majaribio kwa miezi miwili, lakini kuanzia Agosti mtauona ukiungwa mkono na pande zote,” alisema Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri.

Aliendelea: “Hii si chuki, bali ni mashindano ya kisiasa ya kuhakikisha Rais Ruto atashinda tena 2027. Hatutakubali serikali tuliyoipigania ivunjwe na tamaa ya Gachagua.”

Chama cha Jubilee kimejitokeza waziwazi kupambana na Gachagua, ikiwemo kujaribu kumvuta Dkt Matiang’i kutoka kwa kambi ya Gachagua.

Kwa mujibu wa Ngunjiri Wambugu, “kupambana na Gachagua ni ajenda halisi ya ukombozi dhidi ya udikteta wa mtu mmoja na chama kimoja.”

Wambugu, ambaye aliwahi kuwa mshirika wa karibu wa Gachagua, amekuwa akitilia shaka uwezo wa Ruto kushinda tena 2027, na kusema kuwa Gachagua anasukuma chama chake cha Democracy for Citizens na kuwa yeye tu ndiye atakayeamua mwelekeo wa Mlima Kenya.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, alisema kuwa chama hicho kinamuunga mkono Dkt Matiang’i kumshinda Ruto, ingawa Matiang’i amesema bado mazungumzo ya kuunda muungano wa upinzani yanaendelea.

“Watu wanaeneza porojo za kugawanyika kwetu, lakini sisi bado tuko pamoja,” alisema Matiang’i.Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya alisema: “Juhudi zote zinaelekezwa kumkabili Gachagua kama injini ya upinzani.”

Aliongeza kuwa kuna njama zinazohusisha pesa, propaganda, mashtaka ya kisiasa, na usalama ili kumuangusha Gachagua.

Seneta wa Nyandarua John Methu alisema kuwa washirika wa Gachagua wamepata fununu kuhusu mipango ya kuwakamata viongozi wa upinzani zaidi, akiwemo Gavana Natembeya, Mbunge wa Naivasha Jayne Kihara na Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji.

“Hata makanisa yameingizwa kwenye vita hivi. Baadhi ya wachungaji wameanza kubaguliwa kwa kuwapokea washirika wa Gachagua,” alisema.

Mwakilishi wa Wanawake Kirinyaga, Njeri Maina, alisema: “Mitandao ya kijamii imejaa wanablogu, wanamuziki na wachekeshaji waliolipwa kumchafua Gachagua.”

“Mashambulizi hayo yamefadhiliwa na watu wanaojulikana walioko ndani ya serikali ya Ruto,” alisema.