Jamvi La Siasa

Mizimu ya kubadilisha katiba kuwa silaha

Na  John Kamau August 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 4

Huku kukiwa na wito wa kufanyia Katiba ya Kenya marekebisho, mizimu ya jamhuri ya mapema inazidi kutanda. Marais wa kwanza wawili – Mzee Jomo Kenyatta na Daniel arap Moi – walichukulia Katiba si kama mkataba mtakatifu wa utawala, bali kama hati inayoweza kurekebishwa ili kukidhi mahitaji yao binafsi.

Kwao, mabadiliko hayakuwa kuhusu maslahi ya taifa kwa ujumla, bali yalikuwa silaha na kinga: mapanga dhidi ya wapinzani, silaha ya kukinga washirika, na njia ya kujinusuru kisiasa.

Kenya ilipopata uhuru mwaka 1963, mfumo wa majimbo ulilenga kulinda mizani ya kikabila iliyokuwa dhaifu. Mfumo huo uligawa mamlaka kwa mabunge ya maeneo, ili kuondoa hofu ya kutawaliwa na makabila makubwa. Kwa Mzee Kenyatta, majimbo yalikuwa kizingiti. Alitamani kuwa na taifa moja lenye serikali kuu –kuwa na serikali moja, kituo kimoja cha mamlaka, na rais mmoja: yeye mwenyewe.

Mara tu baada ya kushika hatamu za uongozi, serikali yake ilianza kuvunja Katiba ya majimbo kwa kudhoofisha mabunge ya mikoa na kuhamisha mamlaka yao kwa serikali kuu. Hatimaye, majimbo yakawa historia. Ili kufanikisha hilo, Mzee alificha nia yake halisi kwa kizingizio cha umoja. Lakini lengo kuu lilikuwa ni kuimarisha mamlaka yake: kuangamiza wapinzani, kuimarisha wafuasi, na kuhakikisha nguvu zote zinaelekezwa Ikulu.

Mnamo Mei 1965, alizika rasmi mfumo wa majimbo. Mikoa ikabadilishwa kuwa majimbo ya kiutawala, mabunge ya mikoa yakashushwa hadhi kuwa mabaraza ya miji bila mishahara, na udhibiti wa ardhi ukahamishwa kutoka maeneo ya mashinani. Alichovumisha kama suluhu ya umoja, kiligeuzwa kuwa mfumo wa rais mwenye mamlaka makubwa – jambo ambalo liliibua kilio kilichozaa Katiba ya 2010.

Mwaka 1966, Jaramogi Oginga Odinga na washirika wake walipojiondoa KANU na kuunda chama cha Kenya People’s Union (KPU), jibu la Mzee halikuwa kuvumilia bali kujihami. Marekebisho ya Katiba ya Tano mnamo Aprili 1966 yaliwalazimu wabunge waliotoroka chama kutafuta tena kura kutoka kwa wananchi. Hili lilikuwa na unafiki kwani miaka miwili kabla, Jomo aliwapokea watoro kutoka KADU bila kubadilisha sheria. Mambo yalipomgeukia, Katiba ilirekebishwa haraka usiku mmoja kumlinda rais na mamlaka yake. Bunge liliidhinisha marekebisho kwa wingi na uchaguzi mdogo uliotokana nayo haukuwa jaribio la demokrasia, bali mtego wa kuangamiza upinzani.

Mzee aliendelea mbele, akikusudia kuweka vyombo vyote vya serikali mikononi mwake. Marekebisho ya Nne na ya Saba ya mwaka 1966 yalikuwa ya kihistoria. Watumishi wa umma walipokonywa uhuru wao wa taasisi na wakawa kama viungo vya Ikulu.Wakati huohuo, Seneti – ambayo ingetoa upinzani hata kwa kiwango kidogo – ilivunjwa, na hivyo kuondoa kizuizi cha mwisho dhidi ya urais.

Baada ya Jaramogi kuunda KPU, serikali ya Mzee ilirudia kutumia silaha za wakoloni kukomesha upinzani. Walipata msaada kupitia Sheria ya Ulinzi wa Usalama wa Umma ya mwaka 1966. Ingawa iliwasilishwa kwa lugha ya usalama wa taifa, ndani yake kulijifichwa muundo wa ukandamizaji. Ilipatia serikali mamlaka ya ajabu – kuwazuia watu bila kuwashtaki kortini, kuweka amri ya kutotoka nje, kudhibiti vyombo vya habari, kunyamazisha wapinzani, na kudhibiti uhuru wa wananchi.

Hizi hazikuwa sheria za haki, bali sheria kugeuka kuwa silaha dhidi ya watu waliopaswa kuzilindwa. Baada ya msafara wa Mzee kupigwa mawe mwaka 1969, viongozi wa KPU walifungwa bila mashtaka. Mamlaka yaliyokuwa yakitumiwa dhidi ya waasi wa Shifta Kaskazini sasa yalielekezwa kwa wapinzani wa kisiasa.

Zaidi ya hayo, marekebisho ya Katiba yaliyoambatana nayo yalifanya uamuzi wa rais wa kumzuia mtu usiwe ukiukaji wa haki za kikatiba. Sheria ziliandikwa upya ili kuhalalisha ukandamizaji. Katiba – iliyoandikwa wakati wa uhuru kama hati ya uhuru – ikawa ngome ya mamlaka ya rais. Haikulinda tena wananchi, bali ililinda utawala dhidi ya wananchi.

Kufikia miaka ya 1970, Katiba ilikuwa kama zana ya kibinafsi ya Jomo. Udanganyifu mkubwa zaidi ulitokea mwaka 1975 kupitia Marekebisho ya 15. Paul Ngei, mshirika wa Kenyatta, alipoteza kiti chake cha ubunge baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya uchaguzi. Rais alikataa kumwachilia. Kwa siku mbili tu, Bunge lilipitisha marekebisho yaliyompa rais uwezo wa kusamehe wahalifu wa uchaguzi. Jomo alitumia haraka kipengele hicho kumrejesha Ngei bungeni na serikalini. Sheria ilipotishia rafiki yake, ilibadilishwa.

Kulikuwa na mpango wa mwaka 1978 kubadilisha Katiba ili kumzuia Moi kurithi urais moja kwa moja. Hili lilizimwa na Mwanasheria Mkuu Charles Njonjo aliyempendelea Moi kwa sababu ya maslahi yake binafsi.

Kama Kenyatta alitumia Katiba kuimarisha mamlaka, Moi – baada ya kuchukua madaraka mwaka 1978 – alikamilisha sanaa ya utawala wa kibinafsi. Mwaka 1982, Marekebisho ya 19 yaliingiza Kifungu cha 2A: “Kutakuwa na chama kimoja tu cha siasa nchini Kenya, Chama cha KANU.” Kenya ikawa taifa la chama kimoja kwa mujibu wa sheria.

Washirika wa Moi walitetea hatua hiyo kwa uzalendo, wakidai kuwa ilikuwa ni kuthibitisha hali halisi kwani KANU haikuwa na upinzani wa kweli. Kwa vitendo, kifungu hicho kilifanya upinzani kuwa kosa la jinai. Vyama pinzani na dhana ya vyama vingi vilipigwa marufuku. Upinzani haukuwa tena maoni, bali uhaini.

Moi pia alitumia Katiba kulipiza kisasi binafsi. Mwaka 1986, Marekebisho ya 22 yalifuta ofisi ya Katibu Mkuu iliyokuwa inashikiliwa na Simeon Nyachae baada ya tofauti kati yao. Pia yalinyang’anya Mwanasheria Mkuu na Mkaguzi Mkuu usalama wa ajira, wakawa wanamhudumu kwa hisani ya rais.

Miaka miwili baadaye, mwaka 1988, marekebisho mengine yalifuta usalama wa kazi kwa majaji. Hili halikuhusiana na utawala bali ugomvi wa kibinafsi kati ya Jaji Mkuu Miller na jaji Mzungu kuhusu uhamisho. Moi aliposhindwa kumfuta kazi, alibadilisha Katiba. Marekebisho yalipopita, jaji alifutwa kazi mara moja. Kisha, mwaka 1990, Bunge hilo hilo lilirejesha usalama wa kazi kwa majaji, Mwanasheria Mkuu, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Tume ya Huduma za Umma. Kile kilichofutwa kwa haraka kilirejeshwa kimyakimya.

Kufikia wakati huo, Bunge lilikuwa limegeuzwa kuwa kama chombo cha kupitisha maamuzi ya rais bila upinzani. Katiba haikuwa tena ngao ya haki; ilikuwa kama chombo cha rais kucheza nacho.

Wakati pendekezo lililetwa kurefusha muda ambao polisi wanaweza kumzuia mshukiwa wa kosa la mauaji – kutoka saa 24 hadi siku 14 – wachache waliopinga walitoka kwa viongozi wa kidini na wanasheria mashuhuri. Kasisi mchanga wa Baptist, Mutava Musyimi – ambaye baadaye aliongoza harakati za kanisa dhidi ya serikali – alikuwa miongoni mwa wa kwanza kupaza sauti.

Wanasheria mashuhuri kama Kiraitu Murungi, Gitobu Imanyara, Paul Muite, Kamau Kuria na John Khaminwa pia walipinga mswada huo. Lakini ndani ya Bunge, woga ulitawala. Wanasiasa, kwa kuogopa hasira ya rais, walipiga kura kwa kauli moja.

Hata hivyo, kufikia miaka ya 1990, utawala wa kiimla wa Moi ulianza kuyumba. Ghasia za ndani, shinikizo kutoka nje, na uondoaji wa misaada kutoka nchi za Magharibi vilimlazimisha alegeze msimamo. Mnamo Desemba 1991, Kifungu cha 2A kilifutwa na siasa za vyama vingi zikarudishwa. Lakini hata mabadiliko haya yalikuwa ya kuokoa hali. Moi alikubali dakika ya mwisho tu, baada ya kutengwa na mataifa ya nje.

Mabadiliko ya baadaye ya IPPG mwaka 1997 yalileta mageuzi muhimu, ikiwemo kuondolewa kwa sheria ya kuwazuia watu bila mashtaka na mageuzi ya sheria za uchaguzi. Lakini haya hayakutokana na ukarimu wa rais, bali yalikuwa ni matokeo ya majadiliano ambapo Moi alijaribu kubaki madarakani huku akiepuka kusambaratika kisiasa.

Kutoka kwa Kenyatta hadi Moi, Katiba haikuwahi kuchukuliwa kama mkataba mtakatifu. Iliumbwa upya, ikapindwa na kutumika kulinda mamlaka ya mtu binafsi. Wote wawili walidai kutenda kwa jina la umoja, utulivu au maendeleo. Lakini ukweli ni kwamba, marekebisho yao ya Katiba yaliwalinda wao na marafiki zao, huku yakidhoofisha taasisi zilizopaswa kuwalinda wananchi.