Mlima waomba msamaha kwa ‘kuchukua mwelekeo mbaya’ 2022
WAKAZI wa Mlima Kenya Ijumaa, Desemba 27, 2024 waliandaa maombi makubwa ya kusaka msamaha kwa kumchagua Rais William Ruto mnamo 2022 huku wakishutumu utekaji nyara na mauaji yanayoshuhudiwa nchini.
Wakitazama Mlima Kenya, waumini hao walimlilia mwenyezi Mungu ili awanusuru vijana ambao wametekwa nyara huku wakishutumu utawala huu kwa usaliti wa kisiasa na utekaji nyara.
Ibada hiyo ilifanyika eneo la Samson Corner, Kaunti ya Kirinyaga.
Eneo hilo kwa sasa linatikiswa na mawimbi makali ya kisiasa baada ya kigogo wao Rigathi Gachagua kuondolewa kwenye wadhifa wake kama naibu rais miezi miwili iliyopita.
Bw Gachagua ambaye kwa sasa ana uhasama mkubwa na serikali, aliondolewa mamlakani mnamo Oktoba 18 kupitia hoja iliyowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi.
Maombi ya jana yalilenga kuomba msamaha wakati ambapo Mlima Kenya upo upinzani licha ya kuwekeza pakubwa kwenye kampeni za urais za William Ruto mnamo 2022.
Wakili Ndegwa Njiru ambaye ni kati ya wale ambao walimwakilisha Bw Gachagua mahakamani na alihudhuria maombi hayo, alisema ibada hiyo ililenga kuhakikisha kabisa hawafanyi kazi tena na Rais William Ruto.
“Maombi haya ndiyo huweka jamii yetu pamoja na yalikusudia kuomba msamaha kwa makosa ambayo tulifanya 2022 kwa kufanya kazi na mtu ambaye ni adui wa jamii yetu. Hatua hiyo haikufurahisha wenzetu ambao wametangulia mbele za haki,” akasema Bw Njiru katika mahojiano na Taifa Leo.
“Katika imani yetu tunaamini kuwa watu waliokufa kutokana na dhuluma na ukatili lazima wanafuatilia yanayoendelea na hawakufurahishwa na hatua tulizochukua kisiasa.
“Sisi 2022 tuliamua kufanya na kazi na watu waliotudhulumu katika ghasia za 2007 ndiposa tunapitia mahangaiko haya ya kisiasa.
Tumeomba tukiangalia Mlima Kenya ili kuomba msamaha na tuongozwe tusihadaiwe kurejea katika njia hiyo tena,” akaongeza.
Wakili huyo alimhusisha Rais Ruto na masaibu ya jamii hiyo akisema baada ya kuombea eneo hilo sasa wapo tayari kuanza safari na mwana ‘wao’ Bw Gachagua.
“Tulikosea na tumeomba tusamehewe kwa sababu tulienda kinyume na kushirikiana na watesi wetu. Changamoto zote zinazokabili mlima ziwe za kisiasa, kutekwa nyara kwa vijana wetu na za kiuchumi ambazo zimeletwa na utawala huu, zimefanya tuanze safari mpya,” akaongeza.
Waumini walioshiriki ibada hiyo walivalia mavazi meupe huku wakiwa wamejifunga riboni za samawati, mavazi ambayo huzingatiwa kama yaliyotakatifu wakati wa ibada.
Mzee Samuel Kamitha, alisema kuwa Kenya ipo katika mkondo ambao sheria haiheshimiwi tena ambao utekaji nyara na mauaji sasa yanaelekea kuwa kama mambo ya kawaida.
Aidha waumini hao walitangaza vita vya kiroho dhidi ya changamoto ambazo zinakabili nchi ikiwemo utekaji nyara na masaibu ya Mlima Kenya kisiasa.
“Tunashutumu mauaji hayo na kutekwa nyara kwa vijana. Kupitia maombi tutavishinda vita hivi,” akasema Bw Karanja Mwangi, muumini.
Mzee Kamitha alisema wamekuwa wakitekeleza maombi wakizunguka Mlima Kenya mara saba kila mwaka na ibada ya mwaka huu imekuja wakati wa changamoto nyingi ndiposa lazima watubu.
Wakati wa ibada hiyo, wao hutoa kafara kwa Mwenyezi Mungu na kabla ya kuelekea mlimani, waumini wakinyunyiziwa maji matakatifu.
Waumini hao waliotoka dini za Kiislamu, Kikristo na wale wanaobudu kwa njia za kitamaduni, walitoa ushuhuda kuwa maombi hayo yamezaa matunda miaka nyuma na hata ya mwaka huu, yatafanikiwa.
“Kupitia maombi hayo, wengi wamepona magonjwa na biashara za watu zimenawiri. Maombi haya pia yameleta amani nchini na hatutakoma hadi changamoto za sasa zitokomee,” akasema muumini mwengine.
Awali, waumini hao walivua viatu na kuomba kando ya vichaka huku wakimlilia Mungu akubali dua zao wakianza kuzunguka mlima. Baadhi walionekana kutokwa na machozi huku wengine wakiongea kwa ndimi.
“’Kila mwaka tarehe kama hii huwa tunakongamana hapa na kumwomba Mungu atupee amani na kuwalinda watoto wetu kutoka kwa mwovu sheteni na kupata msamaha,” akaongeza.
Pia waumini hao waliwaombea vijana ambao wamelemewa na uraibu wa kutumia dawa za kulevya.
Kuhusu utekaji nyara, Bw Ndegwa alidai kuwa kuna kundi ambalo limeundwa na linaongozwa na maafisa wa DCI na NIS ambalo limetenga vyumba ambavyo wanaotekwa wanazuiliwa.
Alimwondolea Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja makosa, akisema hahusishwi katika mpango ambao unaendeshwa na kikosi ambacho si ndani ya idara ya polisi.