Moi aliongoza muungano wa Afrika kwa mihula miwili
RAIS wa pili wa Kenya Daniel Toroitich Arap Moi alihudumu kwa mihula miwili mfululizo kama Mwenyekiti wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (1981-1983), akiwa rais wa pekee kuwahi kuhudumu kwa muda mrefu zaidi katika wadhifa huo.
Alichukua msimamo mkali dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, akilaani dhuluma dhidi ya raia wa Afrika Kusini na nchi nyingine za kusini mwa Afrika.
Mnamo Desemba 1981, baada ya majeshi ya utawala wa ubaguzi wa rangi kuvamia Lesotho, Moi alisema “Utawala wa kibaguzi wa Pretoria unaendelea kuvamia bila kuadhibiwa mataifa jirani kusini mwa Afrika kwa kisingizio kwamba mataifa haya yanawahifadhi wapinzani wa utawala wa ubaguzi wa rangi. Tunaamini kwamba utawala wa kibaguzi wa Pretoria hautawahi kuheshimu maadili ya sheria ya kimataifa. Kwa hiyo, jumuiya ya kimataifa lazima ianzishe hatua za kuiadhibu.”
Jukumu la Moi la kulinda amani Afrika lilianza mwaka wa 1979 aliporuhusu wanajeshi wa Kenya kujiunga na Kikosi cha Jumuiya ya Madola nchini Zimbabwe (CMFZ) hadi 1980.
Hii ilikuwa ni kuhakikisha mpito mzuri kuelekea Uhuru katika nchi hiyo. Mnamo Juni 1981 baada ya Moi kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa OAU katika mkutano jijini Nairobi, alihusika katika kulinda amani nchini Chad wakati ambao mzozo kati ya Rais Goukouni Wedeye na kiongozi wa waasi Hissen Habre ulikuwa umechukua mkondo hatari.
Kenya ilishiriki amani Chad kati ya 1981 na 1982 na zaidi ya operesheni zingine 20 barani Afrika, Asia na Ulaya. Kenya ilichangia waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Msumbiji, Angola, na Liberia miongoni mwa nchi zingine.
Lakini ni juhudi za amani Sudan na Somalia ambazo zilijulikana zaidi. Nchini Sudan, Moi aliongoza mazungumzo ambayo hatimaye yalipelekea kura ya maoni iliyomaliza vita kusini mwa Sudan na kusababisha kuundwa kwa Taifa jipya – Sudan Kusini. Nchini Somalia, alianza mchakato ambao uliishia kwa kuunda serikali ya sasa.
Alituma wanajeshi wa Kenya kama sehemu ya vikosi kadhaa vya kulinda amani ndani na nje ya Bara la Afrika, ambazo ni Chad, Uganda, Namibia, Msumbiji, Morocco, Liberia, Sierra Leone na Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo barani Afrika na Iran/Iraq, Kuwait, Yugoslavia, Serbia/Croatia na Timor ya Mashariki
Pia alihusika katika kusaidia kuzima migogoro katika nchi kadhaa za Eritrea/Ethiopia, Rwanda na Burundi.
Aliwahi kuwa Mwenyekiti wa (Preferential Trade Area PTA) (1989-1990), COMESA (Soko la Pamoja la Afrika Mashariki na Kusini) (1999-2000 na mashirika mengine kadhaa.
Rais Daniel arap Moi alikuwa miongoni mwa viongozi wachache duniani walitawala nchi kwa falsafa akisisitiza amani, upendo na umoja.. Alipoingia mamlakani alianza kutumia msemo wa Kiswahili ‘ fuata ‘nyayo,’ katika kuendeleza kauli mbiu ya mtangulizi wake Kenyatta ya “harambee”.
Ujumbe huo uliwasilishwa katika mikutano ya hadhara kote nchini. Aliwataka watu wote wa Kenya kuweka kando ushindani wao wa muda mrefu na kuishi kama kitu kimoja.
Rais huyo wa pili na aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi Kenya atakumbukwa kwa jinsi alivyohimiza umoja wa kitaifa na kuhakikisha nchi iepuka mitego ya migogoro ya ndani katika eneo ambalo liliathiriwa na machafuko.
Pia alifanya juhudi kueneza falsafa yake ya mapenzi katika bara la Afrika. Katika kipindi chake kama mwenyekiti wa Umoja wa Umoja wa Afrika, alihubiri amani, upendo, na umoja kwa mataifa yanayopigana na yaliyogawanyika kama vile Chad, Libya, Ethiopia na Uganda. Juhudi zake zilipata heshima barani Afrika na aliweka wazi kuwa Kenya haijihusishi na visa hivyo. Alikuwa akijigamba Kenya ilikuwa kama kisiwa cha amani katika eneo lililogubikwa na mizozo.
Katika kipindi cha miaka 24 akiwa madarakani, Rais wa pili wa Kenya alisimamia hatua nyingi muhimu ambazo ziliweka msingi wa ukuaji endelevu wa nchi kama vile ujenzi wa Wadi za Nyayo katika hospitali nyingi za wilaya.