Jamvi La Siasa

Msisimko wa urejeo wa Gachagua ulivyozimwa

Na BENSON MATHEKA August 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JAPO alitarajiwa kusisimua upinzani ambao ulikuwa baridi akiwa nje ya nchi, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alizimwa na serikali na akalazimika kubadilisha mipango yake baada ya kurejea kutoka ziara ya Amerika.

Wakenya wengi walitarajia kiongozi huyo wa chama cha DCP angewahutubia wafuasi wake kwa hotuba kali baada ya kurudi nchini kutoka Amerika ambako alikuwa akishambulia serikali.

Hata hivyo, kilichowashtua wengi ni ukimya wake alipowasili na msafara wake kushambuliwa na wahuni huku polisi wakipangwa kumzuia asifike uwanja wa Kamukunji alikotarajiwa kuhutubia wafuasi wake.

Gachagua alinyamaza hadi Ijumaa usiku alipotoa kauli kali akilaumu serikali kwa kusambaratisha mipango ya mapokezi ya kurejea kwake nchini.

Gachagua amemshutumu Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen kwa kuonyesha unafiki na kudai kuwa anachunguza vurugu zilizoshuhudiwa wakati wa kurejea kwake, ilhali alikuwa miongoni mwa walizipanga.

“Mpango wa vurugu zile ulikuwa wa kina. Ulijumuisha ufuatiliaji kutoka angani, wahuni waliolipwa na maafisa wa polisi, pamoja na wandani wa Rais Ruto,” alisema Gachagua.Kulingana na Gachagua, mpango wake ulikuwa awasili uwanja wa ndege, kuhutubia waliofika kumpokea, kisha kuelekea barabara ya Ladhies, Gikomba na Kamukunji.

Hata hivyo, anadai serikali ilifanya kila juhudi kuhakikisha hilo halifanyiki.Kulikuwa na tetesi mitaani na kwenye vikao vya kisiasa kwamba huenda Gachagua alitulia kufuatia vitisho vya kumkamata kutokana na matamshi aliyotoa akiwa Amerika akihusisha viongozi wakuu wa serikali ya Kenya na vitendo haramu.

Baadhi ya duru za kisiasa zilidai kuwa kuna mazungumzo ya siri yaliyofanyika wakati wa ziara yake Amerika, ambapo huenda alishauriwa kupunguza makali yake ya kisiasa, hasa baada ya kuonekana kupingana na baadhi ya misimamo ya Rais William Ruto na wandani wake wa karibu na kupandisha joto la siasa.

“Nimejifunza mengi kutoka kwenu na ninarudi nyumbani nikiwa nimefaidika zaidi na maoni yenu,” Gachagua alisema akiwaaga raia wa Kenya wanaoishi Amerika.

Gachagua anasisitiza alikutana na Wakenya wanaoishi Amerika kuwaeleza ukweli wa hali ya siasa nchini na wakaahidi kumuunga mkono.Gachagua alikatiza ziara yake ya Amerika akisema alitaka kurejea nchini kuongoza chama chake cha DCP kwa maandalizi ya chaguzi ndogo zijazo.

“Kuna uwezekano mkubwa kwamba Gachagua anapanga kujiweka sawa kwa mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini kwa maandalizi ya siasa za 2027,” asema mchanganuzi wa siasa Beth Kimani.Gachagua alikatiza ziara yake ya Amerika akisema alitaka kurejea nchini kuongoza chama chake cha DCP kwa maandalizi ya chaguzi ndogo zijazo.

Washirika wake wanasema hajanyamaza bali anapumzika kwa muda kabla ya kuanza siasa.“Gachagua sio wa kunyamazishwa. Kama hakuogopa alipovuliwa wadhifa wake wa naibu rais na kushambuliwa hadharani mara kadhaa na wahuni waliolipwa anaweza kuogopa nini sasa. Atarudi uwanjani karibuni. Tegea,” alisema mmoja wa wandani wake aliyeomba tusitaje jina kwa sababu zake za kibinafsi.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa kuna dalili za mgawanyiko mkubwa ndani ya upinzani na kimya cha Gachagua kinaweza kuwa jaribio la kupima joto la kisiasa kabla ya kutoa mwelekeo mpya.

Hata hivyo, Gachagua anasisitiza kuwa sasa yuko kikamilifu katika upinzani ulioungana, akiwa pamoja na viongozi wengine walivyotangaza awali.“Kwa wale wanaopenda kuleta mkanganyiko, nataka nieleweke – mimi ni mwanachama kamili wa upinzani ulioungana. Sasa tunakaribia kuzindua mipango itakayotutambulisha,” alisema.

Gachagua alifichua kuwa wakati wa ziara yake Amerika, alielezea Wakenya wanaoishi huko hali halisi ya mambo ndani ya serikali ya Ruto.Kwa sasa, asema Kimani, Wakenya wanasubiri kuona iwapo Gachagua na upinzani wana mikakati ya kutetemesha siasa nchini anavyodai.