Jamvi La Siasa

Mwambieni Ruto mimi ni mteja, sipatikani ng’o, Kalonzo aambia wahubiri

Na  PIUS MAUNDU September 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, jana aliwashambulia baadhi ya wachungaji wakuu wanaohudumu eneo la Ukambani, akiwalaumu kwa kutumiwa kisiasa na Rais William Ruto huku ushindani wa kura milioni 1.7 za eneo hilo ukizidi kupamba moto kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Akifahamu umuhimu wa kanisa wakati wa kampeni zake za uchaguzi, Rais Ruto amekuwa akilitumia kuimarisha ushawishi wake eneo la Ukambani ambalo ni ngome ya kisiasa ya Bw Musyoka.

Hata hivyo, Makamu huyo wa Rais wa zamani amejitokeza wazi kujaribu kuzima juhudi hizo, akitaka kanisa kujiunga na upinzani kumpinga Rais Ruto.

Rais Ruto alifichua kuwa aliteua kundi la maaskofu wakuu kutoka Ukambani kujaribu kumbembeleza Bw Kalonzo kuungana naye, hatua ambayo iliwakasirisha viongozi wa upinzani.

Katika matamshi yaliyotafsiriwa kumlenga Askofu Mkuu Timothy Ndambuki wa kanisa la African Brotherhood Church (ABC), Askofu Abraham Mulwa wa African Inland Church (AIC), na Meja Leonard Kasyoka wa Salvation Army, wote wanaojulikana kuunga mkono juhudi za Rais Ruto, Bw Kalonzo alisema viongozi hao wa kidini wanahatarisha heshima yao kwa kuingilia siasa za upande wa upinzani.

“Msidanganyike na mtego wa William Ruto wa kutumia maaskofu wakuu wa hapa nyumbani. Anawaita Ikulu, anawapa helikopta, halafu anataka wanishawishi. Wasijisumbue. Wapendwa hawa wanapaswa kuheshimu waumini wao. Wakazi wanajua haki zao za kikatiba. Maendeleo ni haki yao ya kuzaliwa. Hatupaswi kuomba omba,” alisema Bw Kalonzo.

Alisema hayo alipohutubia waumini katika kanisa la Calvary Christian Church, Mutituni, Kaunti ya Machakos, huku Rais Ruto akihudhuria mchango kwa chuo cha Eastern Kenya Integrated College, ambacho kinahusishwa na kanisa la ABC huko Mitaboni.

Rais Ruto alifichua kuwa alianza kushirikiana na viongozi wa kidini Ukambani baada ya wakazi kupinga baadhi ya miradi yake kama ujenzi wa masoko na makazi nafuu.

“Awali, walikuwa wanasema hawataki nyumba za bei nafuu wala masoko. Niliwaita maaskofu hawa nikawaambia: Ukambani ni sehemu ya Kenya. Hauwezi kuwa upinzani kupita hata upinzani wenyewe. Leo hii miradi hiyo ipo Ukambani kwa sababu viongozi wa dini walisaidia,” alisema Rais Ruto.

Askofu Ndambuki, aliyemkaribisha Rais Ruto, alikosoa wanasiasa wa Ukambani kwa kujitenga na serikali ya Kenya Kwanza, akisema “Wengine wanalia kuwa tumetengwa, lakini sisi wenyewe tunajitenga.

”Askofu huyo, ambaye hapo awali alikuwa mshirika wa karibu wa Bw Kalonzo, sasa anatumia kanisa kuhimiza jamii kuunga mkono serikali ya Ruto hatua ambayo haijapokewa vyema na Bw Kalonzo ambaye anashutumu makanisa kwa kufumbwa macho na misaada ya Rais.

Hivi majuzi, Rais Ruto alitangaza kuwa alilipa mishahara ya mwaka mzima wahadhiri wa chuo cha Scott Christian University kinachomilikiwa na AIC, akikitaja kama fahari ya jamii ya Wakamba na Wakalenjin.

Katika mkutano wa Ikulu mnamo Mei, Askofu Ndambuki, Askofu Mulwa, Meja Kasyoka na Askofu wa Dayosisi ya Katoliki ya Machakos, Norman King’oo, waliahidi kutumia ushawishi wao kumshawishi Kalonzo na wafuasi wake kumuunga mkono Rais Ruto.

Hata hivyo, aliyekuwa Naibu wa Rais, Rigathi Gachagua, aliyetembelea Machakos pamoja na viongozi wa upinzani Eugene Wamalwa na Justin Muturi kuungana na Kalonzo jana, alipuuza mbinu ya Ruto kutumia kanisa kisiasa.