Mwangaza alivyojipata gizani
SAFARI ya miaka miwili ya Askofu Kawira Mwangaza kuokoa wadhifa wake kama gavana wa tatu wa Kaunti ya Meru ilifikia mwisho jana, Mahakama Kuu ilipoidhinisha hatua ya seneti ya kumuondoa ofisini.
Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye aliamua kwamba kubanduliwa kwa Mwangaza na Seneti kulitimiza viwango vya kikatiba vinavyohitajika, na kwamba hakutoa sababu za kuwezesha mahakama hiyo kuingilia uamuzi huo.
Kuondolewa kwake kunatoa nafasi kwa naibu wake, Bw Isaac Mutuma, kuwa gavana wa nne wa Meru.
“Mchakato wa kumuondoa ofisini ulifanyika kwa mujibu wa Katiba. Madai ya mlalamishi, yanayojumuisha shutuma zake za ukiukaji wa taratibu, ukosefu wa ushirikishaji wa umma, na ukaidi wa maagizo ya mahakama, hayana msingi,” alisema Jaji Mwamuye.
Maseneta waliidhinisha uamuzi wa Bunge la Kaunti ya Meru wa kumtimua Bi Mwangaza mnamo Agosti 21 mwaka jana, baada ya jaribio la tatu la kumuondoa madarakani.
Jumla ya maseneta 26 walipiga kura kuunga mkono mashtaka matatu dhidi yake, lakini alikimbilia mahakama siku hiyo hiyo na Jaji Mwamuye akasitisha utekelezaji wa uamuzi wa Seneti wa kumwondoa kazini.
Baada ya kubaki ofisini kwa miezi sita kwa agizo la mahakama, Bi Mwangaza hakuwa na bahati tena jana kwani Jaji Mwamuye aliidhinisha uamuzi wa Seneti wa kumtimua.
“Ombi lililorekebishwa la Desemba 23, 2024 halijatimiza vigezo vya kisheria vinavyohitajika ili mahakama hii ifute uamuzi wa Seneti,” alisema Jaji.
Gavana Mwangaza alipinga kuondolewa kwake kwa misingi kadhaa, kama vile madai ya ukiukaji wa taratibu, haki ya kusikilizwa, na ushirikishaji hafifu wa umma.
Mwangaza alikuwa mmoja wa magavana saba wa kike waliochaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022, ambapo alipata kura 209,148 na kumshinda aliyekuwa gavana Kiraitu Murungi na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi.
Wawili hao walionekana kuungana na gavana wa kwanza Peter Munya dhidi ya Mwangaza.
Askofu Mwangaza alishinda ugavana akiwa mgombeaji huru lakini baadaye alijiunga na chama cha UDA cha Rais William Ruto.
“Tangazo la Gazeti Rasmi No. 10351 Vol. CXXVI-No 130 la Agosti 20, 2024 lililochapishwa Agosti 21, 2024 na lililotolewa kuwasilisha uamuzi wa Seneti wa kumwuondoa mlalamishi katika wadhifa wa Gavana wa Kaunti ya Meru kwa njia ya kumng’oa ofisini linaidhinishwa kwa madhumuni ya kesi hii,” alisema Jaji Mwamuye.
Gavana huyo aliwasilisha kesi mahakamani akidai kuwa uamuzi wa kumuondoa ulitokana na misingi isiyo na uzito wa kisheria. Kupitia mawakili wake Elisha Ongoya na Elias Mutuma, Bi Mwangaza alidai kuwa hakupata fursa ya kujitetea mbele ya Seneti kwa sababu ya vurugu zilizotokea na kuharibu mchakato mzima.
Hata hivyo, Jaji alisema hakuna ushahidi wa vurugu na kwamba Bi Mwangaza alipewa nafasi ya kujitetea.Jaji aliongeza kuwa Seneti haikufanya uamuzi kwa kudharau agizo la mahakama ya Meru, kwani haikuwa mshiriki katika kesi hiyo na kwamba Bi Mwangaza hakuwasilisha mashtaka yake ipasavyo kwa Seneti.
Mahakama Kuu ya Meru ilipata Bunge la Kaunti na viongozi wake waliendesha mchakato wa kumtimua Mwangaza licha ya agizo la kuwazuia kufanya hivyo.Jaji Mwamuye alisema msingi huo hauwezi kubatilisha mchakato wa kumwondoa madarakani uliofanywa na Seneti.Wakati wa kujadili suala hilo, Seneti ilisema Bi Mwangaza alipewa nafasi ya kusikilizwa, na mahakama haipaswi kuingilia mchakato huo.
Baadaye, Jaji Mwamuye alikataa kusitisha uamuzi wake akisema hakukuwa na kosa katika maamuzi yake.Bi Mwangaza aliomba mahakama kusimamisha uamuzi huo ili akate rufaa, lakini jaji alikataa ombi hilo, akisema hakuna hoja nzito zilizotolewa ambazo zingefanya mahakama isitishe uamuzi huo.
Jaji alisema Katiba imeweka taratibu sahihi za kuhakikisha usimamizi wa kaunti unaendelea hata kama gavana hayupo.
“Mahakama hii haiwezi kujitathmini yenyewe. Mara tu mahakama inapotoa uamuzi wake, haina mamlaka ya kuupitia tena,” alisema jaji.