• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Kiraitu Murungi arejea serikalini

Kiraitu Murungi arejea serikalini

NA MERCY KOSKEI

RAIS William Ruto amemteua aliyekuwa Gavana wa Meru Kiraitu Murungi kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Kitaifa la Mafuta la Kenya.

Kulingana na Notisi ya Gazeti Rasmi la Serikali iliyochapishwa Aprili,20, Bw Kiraitu atashikilia wadhifa huo kwa muda wa miaka mitatu.

Murungi ametwaa nafasi ya Mhandisi Patrick Obath, ambaye alikuwa ameteuliwa na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta.

“Mimi, William Samoei Ruto nimemteua Kiraitu Murungi kuwa mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Kitaifa la Mafuta la Kenya kwa muda wa miaka mitatu kuanzia Aprili 20, 2023,” notisi ya gazeti la serikali ilibainisha.

Bw Murungi, mwanasiasa mkongwe kutoka Meru, alipoteza kiti chake cha ugavana katika uchaguzi wa Agosti 2022 kwa Kawira Mwangaza.

Baada ya uchaguzi, chama cha Murungi, Devolution Empowerment Party (DEP) kilijiunga na Muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Rais Ruto.

Mwanasiasa huyo amekuwa nje ya serikali tangu kushindwa kwake katika kiti cha ugavana Meru mwaka jana, hadi alipopata uteuzi huu.

Murungi, 71, pia amewahi kuhudumu katika baraza la mawaziri la Rais mstaafu marehemu Mwai Kibaki, katika Wizara ya Kawi.

Walioteuliwa pia ni aliyekuwa mgombea urais na kiongozi wa chama cha Agano, Bw David Mwaure Waihiga ambapo aliteuliwa kuwa mwenyekiti  wa Trustees of the National Environment Trust Fund board kwa muda wa miaka mitatu.

Richard Cheruiyot aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa Mamlaka ya Maeneo ya Uzalishaji Bidhaa za Nje, huku Kimathi Mbogori Kigatiira akipata uteuzi kuwa  mwenyekiti mpya wa bodi ya Taasisi ya Uzalishaji wa Chanjo za Mifugo ya Kenya.

Rais pia amemteua aliyekuwa Gavana wa Tharaka Nithi Samuel Ragwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao kwa kipindi cha miaka mitatu.

Aliyekuwa naibu gavana wa Makueni Adelina Mwau, naye ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya Kenyatta International Convention Centre (KICC).

Wakili wa UDA Adrian Kamotho Njenga ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa  Capital Markets Authority (CMA), huku Ndirangu Gichinga akiteuliwa kuwa mwenyekiti wa Insurance Tribunal.

 

  • Tags

You can share this post!

Joho: Nikipata nafuu nitaongoza maandamano ya Azimio 

Wakenya 3 wateuliwa kujiunga na muungano wa madaktari...

T L