Jamvi La Siasa

Nani anamiliki wahuni, Serikali au Upinzani?

Na BENSON MATHEKA July 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MAANDAMANO ya kitaifa yaliyoongozwa na kizazi cha Gen Z mnamo Juni 25, 2025 yameacha vifo vya raia, uharibifu mkubwa wa mali ya umma na ya kibinafsi, uporaji wa maduka, na kushambuliwa kwa vituo vya polisi na mahakama.

Lakini zaidi ya hayo, hali hii imetoa jukwaa la lawama kati ya serikali na upinzani kuhusu nani anamiliki wahuni wanaozua ghasia hizi.

Katika kipindi cha wiki moja, taifa limegawanyika kuhusu chanzo cha vurugu hizi zilizochafua maandamano yaliyokuwa yamepangwa kuwa ya amani huku Rais William Ruto akidai kulikuwa na njama ya kupindua serikali nao viongozi wa upinzani wakilaumu serikali kwa kufadhili wahuni kuvuruga maandamano ya amani.

Katika kile kinachoonekana kama hatua kali zaidi kutoka kwa serikali dhidi ya maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen Z, Rais Ruto aliagiza polisi watumie nguvu ikiwa ni pamoja na kuwapiga risasi mguuni wavamizi biashara au vituo vya polisi.

“Mtu yeyote anayechagua kuvamia biashara ya mtu au kituo cha polisi apigwe risasi mguuni. Baadaye apelekwe mahakamani na tuone itakuwaje,” alisema Rais Ruto.

Matamshi haya yalitolewa taifa likiendelea kukumbwa na majonzi kufuatia maandamano ya Saba Saba yaliyosababisha vifo vya watu 31 kufikia Julai 7, 2025, kwa mujibu wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR).

Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Dkt Raymond Nyeris, alithibitisha kuwa kufikia saa moja jioni ya Julai 8, KNCHR ilikuwa tayari imerekodi vifo, majeruhi na visa vya kukamatwa kwa waandamanaji katika maeneo mbalimbali.

Kauli ya Rais ya kuagiza polisi ‘kupiga risasi mguuni’ imeibua wasiwasi miongoni mwa watetezi wa haki za binadamu, wanasheria na wanaharakati ambao wanaiona kama agizo linaloweza kukiuka katiba, kuhalalisha matumizi mabaya ya nguvu, na kuhatarisha maisha ya raia.

Kiongozi wa chama cha Democratic Action Party (DAP-K) Eugene Wamalwa, alielekeza kidole kwa serikali.

“Kutumia wahuni kupora na kuunda taswira ya kisiasa sio tu kuwaumiza wafanyabiashara waaminifu bali pia kunakiuka matarajio ya serikali yoyote. Hizi ni siasa za zamani ambazo haziwezi kufanikiwa katika demokrasia ya kisasa,” aliandika Wamalwa kupitia ukurasa wake rasmi wa X, Juni 26, 2025.

Wamalwa alidai kuwa uporaji wa maduka kama QuickMart OTC katikati ya jiji la Nairobi, ulifanyika chini ya ulinzi wa polisi, jambo linaloashiria uwezekano wa ushirikiano wa maafisa wa usalama na wahuni, kwa lengo la kuhujumu maandamano.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, alipuuzilia mbali madai hayo akisema kile kilichoshuhudiwa ni jaribio la uasi unaojificha nyuma ya madai ya mabadiliko ya kisiasa.

“Kwa wapangaji wa ghasia na vurugu, hatutangoja mtekeleze matendo yenu maovu. Tutawashughulikia kama tunavyoshughulikia magaidi,” alisema.

Kuna video kadhaa zilizosambaa mitandaoni zikionyesha polisi wakisimama kando huku kundi la wahuni likipora na kuchoma mali.

Katika baadhi ya maeneo kama Githurai, Karatina, na Nyandarua, walioshuhudia walisema wahuni walipewa muda wa zaidi ya saa tano kuvunja na kupora maduka bila hatua za polisi kuwazuia.

Ripoti nyingine zilieleza kuwa baadhi ya wahuni waliokuwa wakiranda maeneo ya miji walikuwa wakisafirishwa kwa malori yasiyo na nambari za usajili.

Wahuni wamekuwa wakivuruga mikutano ya upinzani na wanaharakati hata kabla ya maandamano.

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambaye sasa ni anaongoza chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), alivamiwa mara kadhaa na wahuni wakati wa uzinduzi wa chama hicho baada ya kundi la takriban watu 100 kuvamia eneo la tukio na kuanza kurusha mawe, huku walinzi wa chama na polisi wakifyatua risasi hewani kuwatimua.

“Wahuni waliokuwa wamejihami walivamia mkutano wangu. Hii siyo njia ya kuendesha siasa.Demokrasia lazima iheshimiwe,” alisema Gachagua baada ya kuokolewa na maafisa wa usalama.

Wiki jana, viongozi wa upinzani pia walivamiwa na wahuni huku Chwele, kaunti ya Bungoma wakiwa katika ziara yao Magharibi mwa Kenya.

Kundi la akina mama walioandaa mkutano wa wanahabari kulalamikia mauaji ya watoto wao pia walivamiwa na wahuni katika ofisi za Shirika la Haki za Binadamu Kenya (KHRC).

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ambaye alikuwa katika msafara wa upinzani Chwele alikanusha vikali madai ya kuwa upinzani unafadhili maandamano ya ghasia, akisisitiza kuwa harakati hizo ni halali na zimechochewa na hali ngumu ya maisha na utawala usiohusisha wananchi.

Wakati haya yote yakijiri, ripoti rasmi kutoka kwa Waziri wa Usalama, Kipchumba Murkomen, zinasema kuwa zaidi ya maafisa 300 wa polisi walijeruhiwa wakati wa maandamano na kwamba wahuni walivamia vituo vya polisi kama Dagoretti na Gachui, wakijaribu kuiba silaha.

“Wahalifu hawa walikuwa wakilenga hifadhi za silaha na sare za polisi. Bunduki tano ziliibwa kutoka Kituo cha Polisi cha Dagoretti, huku nyingine nne zikichomwa moto Gachui,” alisema Murkomen.

Kwa mujibu wa serikali, maandamano haya yalikuwa sehemu ya jaribio la “mapinduzi ya kisiasa” yanayolenga kupindua utawala halali kupitia fujo na propaganda.

“Mamlaka ya kisiasa hayawezi kupatikana kupitia fujo. Katiba imeweka wazi muda wa utawala. Wanaotaka kuniondoa madarakani wasubiri uchaguzi. Badala ya kutaka kunipindua, walete sera bora,” alisema Ruto.

Lakini hoja hiyo haikuwashawishi wabunge wa upinzani ambao walihoji ni kwa nini polisi hawakuzuia uporaji, kama kweli wahuni hawakuwa sehemu ya mipango ya serikali kuharibu maandamano.

“Wahalifu walipata saa zaidi ya tano kupora maduka Githurai bila polisi kuingilia kati. Kulikuwa na maagizo ya wazi ya kutowatuma maafisa katika baadhi ya maeneo. Hii ni thibitisho kuwa baadhi ya wahuni walikuwa ‘wanamilikiwa’ na serikali,” alisema Mbunge Kamande Mwafrika.