Nderitu Gachagua alinusurika Seneti 2016, hivyo Rigathi pia aombea nyota ishuke kumuokoa
FAMILIA ya Naibu Rais Geoffrey Rigathi Gachagua si geni kwa hoja ya kutimuliwa mamlakani katika Seneti kwa kuwa marehemu kakake James Nderitu alikabiliana nayo miaka minane iliyopita alipokuwa Gavana wa Nyeri.
Marehemu Gavana Nderitu, ambaye aliaga dunia kutokana na saratani ya kongosho mnamo Februari 24, 2017, alikuwa ameondolewa na madiwani 35 kati ya 47 wa Bunge la Kaunti ya Nyeri mnamo Septemba 2, 2016—na hivyo kufika Seneti kujitetea mnamo Septemba 15.
Miaka minane baadaye, kakake mdogo, Rigathi, anajitetea dhidi ya kuondolewa mamlakani kama Naibu Rais wa Kenya.
Bw Nderitu alipokuwa akijitetea Seneti, alikuwa na umri wa miaka 62, Rigathi amefika katika Bunge hilo kujitetea akiwa na umri wa miaka 59.
Japo Bw Nderitu alitakaswa makosa yoyote na Seneti, hatima ya Bw Rigathi haijulikani, huku wafuasi wake wakisubiri matokeo baada ya maseneta kupiga kura Alhamisi.
Ndugu hao wawili walizaliwa katika kijiji cha Hiriga Kaunti ya Nyeri wakiwa watoto wa Bw Gachagua Reriani na Martha Kirigo—wapiganiaji wa uhuru wa Mau Mau katika msitu wa Mlima Kenya.
Baba yao alipokuwa akiwahudumia askari wa Mau Mau, mama yao alisaidia kuwalisha kwa siri, pamoja na kuwapelekea silaha.
Kulingana na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, “hii ni familia ambayo ilibarikiwa kuwa na talanta za uongozi lakini inavyotarajiwa, maadui wa baraka hiyo wamekuwa wakijaribu kuiangamiza”.
Bw Kahiga mnamo Oktoba 16, 2024 aliambia Taifa Leo kuwa “kama baba wa sasa wa Kaunti ya Nyeri, naweza kuapa kwamba hakuna ubaya katika familia ya Gachagua, ni kwamba nyota yake ya uongozi inatatizwa na wale wanaofurahia kuangusha talanta.”
Nderitu alitimuliwa na bunge la kaunti yake, kufuatia hoja iliyowasilishwa na diwani wa Mathari Baragu Mutahi.
Kuhusu kuondolewa kwa mashtaka ya Rigathi, Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse aliwasilisha Oktoba 1, 2024 akiibua mashtaka 11, na wabunge 291, wakiwemo takriban wabunge wote kutoka eneo la Mlima Kenya, waliungana dhidi yake.
Kabla ya kuondolewa mamlakani, Bw Nderitu aliomba msamaha wakazi wa Nyeri kwa kuruhusu suala hilo kuzidi hadi kuwa mjadala wa kitaifa.
Kadhalika, Bw Rigathi, ameomba msamaha kwa Rais William Ruto, Bunge na wananchi wa Kenya kwa mchakato wa kumuondoa mamlakani.
Hata hivyo, maombi yote mawili ya msamaha, hayakufanya kazi na michakato ya kuwashtaki ilifikia Seneti.
Mnamo Septemba 15, 2016, Bw Nderitu alikabiliana na Seneti ambapo iliamuliwa kuwa mashtaka dhidi yake hayajatimiza kiwango cha kuondolewa mamlakani.
Alikuwa ameshutumiwa kwa kumteua Alice Wachira kama kaimu Katibu wa Kaunti licha ya, kulingana na madiwani, hakutimiza mahitaji ya majukumu ya kazi hiyo.
Bunge lilikuwa limependekeza kutimuliwa kwake ofisini mnamo Julai 2016 kwa misingi kwamba hakuwa ametimiza sifa zinazohitajika, ikiwa ni pamoja na kukosa uzoefu wa miaka 10 katika nafasi ya usimamizi.
Vile vile, madiwani walikuwa wamedai kwamba Bw Nderitu alikuwa amefuja Sh1.7 bilioni.
Wawakilishi hao wa wadi pia walikuwa wamemlaumu gavana huyo kwa kukiuka Katiba kwa kuendesha kaunti bila Baraza la Mawaziri, huku wakidai kuwa serikali yake ilitenga Sh740 milioni kutoka kwa maendeleo hadi shughuli za kawaida bila kufuata utaratibu uliowekwa.
Seneti ilipata madai hayo kuwa hayakuthibitishwa.
Huku Rigathi akikabiliana na Seneti, na kusubiri uamuzi wake Alhamisi, atakuwa na matumaini ya kuwa na bahati ya marehemu kaka yake itamuokoa.
Miongoni mwa madai ya Mutuse ni kwamba Bw Rigathi alihujumu wosia wa Nderitu wa kuwanyima warithi halali wa mali ya marehemu, jambo ambalo limeshuhudia wosia wa kibinafsi ‘kufichuliwa’ na kuwa hati ya umma.
“Kimsingi, Wosia wa marehemu ni miongoni mwa sababu zilizowasilishwa kushinikiza kuondolewa kwa naibu rais…hivyo aombe kwa bidii ili roho ya kaka yake ishuke na kusimama naye kwenye dhoruba inayomkumba,” anasema Wakili wa Mahakama Kuu Timothy Kariuki.