Ndoa kamili ya Raila na Ruto 2027 yasukwa
Chama cha ODM kinapanga mkakati wa kuhakikisha utekelezaji kamili wa mkataba wa makubaliano (MoU) wa vipengele 10 kilichotia saini na chama cha UDA cha Rais William Ruto, mpango ambao unaweza kupelekea ushirikiano rasmi wa kabla ya kura ya 2027.
ODM, chini ya uongozi wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, kinatumia mkakati wa kimya kimya kuimarisha ushirikiano wake na serikali ya Kenya Kwanza kupitia utekelezaji wa MoU iliyotiwa saini Machi 7, jambo linaloweza kubadilisha kabisa mazingira ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Ingawa Rais Ruto na Bw Odinga walikuwa mahasimu wakuu kwenye uchaguzi wa 2022, duru kutoka Ikulu, ODM na UDA zimefichua kuwa pande hizo mbili sasa zinaelekea kwenye ushirikiano wa kisiasa kwa msingi wa utekelezaji wa makubaliano hayo.
Bw Odinga tayari amekana tetesi kuwa ana mpango wa kujiondoa mapema kutoka kwa serikali ya umoja, akisisitiza kwamba ataendelea kushirikiana na Rais Ruto hadi 2027.’
Tumesema tuko katika serikali hii jumuishi hadi 2027. Mengine zaidi ya hapo ni mambo ambayo yataamuliwa na wanachama wa chama, si Odinga peke yake,’ alisema Odinga kwenye mahojiano ya hivi karibuni.
Aliongeza kuwa suala la urais si la mihula bali uamuzi wa wananchi kupitia kura.“Si suala la muhula mmoja au miwili. Ni wananchi wanaamua kwa kura. Hata kama ni nusu muhula, watu ndio wenye uamuzi,” alisema.
Ajenda kuu 10 za mkataba huo ni pamoja na utekelezaji kamili wa ripoti ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (NADCO), kulinda na kuimarisha ugatuzi, uwekezaji wa kiuchumi kwa vijana, uongozi wa maadili na uadilifu, kukomesha matumizi ya kifahari serikalini. Duru zinaeleza kuwa tayari timu ya ODM na UDA imeandaa ramani ya pamoja ya kutekeleza makubaliano hayo.
Bw Odinga pia anasukuma kufanyika kwa mazungumzo ya kizazi kwa kizazi yanayolenga vijana wa Gen Z kuhusu uongozi, ajira, ushiriki wa kisiasa, na uwajibikaji.
Mkutano huo utafuatia kongamano kubwa la kitaifa litakalowakutanisha viongozi wa kisiasa, kidini, vijana, na mashirika ya kijamii kabla ya uchaguzi wa 2027.Katika suala la ajira, Rais Ruto anazingatia nafasi za ajira za vijana kupitia ujenzi wa nyumba nafuu, ubunifu wa kidijitali, na hazina ya kuendeleza ajira.
Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki, ambaye pia ni naibu kiongozi wa UDA, alisema ushirikiano wa Raila na Ruto hauwezi kushindwa.“Ruto, mimi, na sasa Raila kuwa pamoja kunamaanisha hakuna mtu wa kutushinda,” alisema Kindiki.
Kiongozi wa Wengi Bungeni, Kimani Ichung’wah, alimpongeza Bw Odinga kwa kusimama na Rais Ruto “kuimarisha utulivu wa nchi.”Mbunge wa Alego Usonga, Bw Sam Atandi, alisema ODM itaungana na UDA 2027 na kumsaidia Ruto kupata muhula wa pili wa urais.
“Tutashirikiana na UDA na kuhakikisha Rais Ruto anachaguliwa tena kwa muhula wa pili, alisema Atandi.
Profesa Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multimedia alisema ODM haipo tena katika upinzani,
Wakati ODM ilikaa meza moja na Ruto na kusaini makubaliano, upinzani ulimalizika. Huo mkataba wa vipengele 10 si mkataba wa umoja wa upinzani, bali ni makubaliano ya kugawana mamlaka yaliyojifichwa katika lugha ya mageuzi,” alisema Prof Naituli.
TAFSIRI: BENSON MATHEKA