Ndoa ya kisiasa ya Raila na Ruto ni telezi
MKATABA wa ushirikiano wa kisiasa kati ya United Democratic Alliance (UDA) na Orange Democratic Movement (ODM) ambao Rais William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga walitia saini Ijumaa haujajikita katika msingi wa kisheria na katiba huku ripoti wanayoazimia kutekeleza ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (NADCO) ikikosolewa vikali.
Wadadisi wa siasa wanafananisha mkataba huo wa ushirikiano kama ndoa isiyo rasmi kwa kuwa vyama vyao vingali wanachama wa miungano ya kisiasa ambayo haijavunjwa rasmi na havijajiondoa rasmi kuweza kuunda muungano mpya.
Wachambuzi wa siasa wanahisi kwamba hii ndio sababu vinara hao hawakuweza kutangaza muungano rasmi wakati wa kutia saini mkataba wa ushirikiano.
“Ieleweke kuwa hii ni MoU wala sio muungano kati ya ODM na UDA. Lakini utekelezaji wa yaliyomo unaweza kuishia katika kuundwa kwa muungano ambao utaendelea kuleta utulivu nchini katika miaka ijayo,” Bw Odinga alifafanua.
ODM ni chama tanzu cha muungano wa Azimio la Umoja One Kenya na UDA ni mwanachama wa muungano tawala wa Kenya Kwanza. Mikataba ya miungano hiyo miwili imewekwa kwa msajili wa vyama.
“ODM haiwezi kuingia Kenya Kwanza kwa kuwa ingali mwanachama wa Azimio la Umoja. Kisheria, inahitajika kujiondoa kuweza kuwa na muungano wa baada ya uchaguzi na UDA. Ilivyo kwa sasa, ndoa ya kisiasa ya ODM na UDA sio rasmi,” akasema mdadisi wa siasa Musa Koli.
Bw Koli anasema kulingana na tamko la Bw Odinga, kuna uwezekano vinara hao wanasubiri utekelezaji wa mfumo wa kisheria kabla ya kutangaza muungano rasmi mwaka wa 2027.
Kiongozi wa chama cha Wiper Democratic Movement, Kalonzo Musyoka, ambaye ni kinara mwenza katika muungano wa Azimio, alitaja mkataba wa Raila na Ruto kama ‘usaliti mkubwa kwa Wakenya’.
Ingawa Raila na Ruto waliafikiana kutekeleza ripoti ya NADCO ambayo ni matunda ya mazungumzo ya pande mbili katika Bomas of Kenya mwaka 2023, wadadisi wanasema walivyosuka ndoa yao kunafanya ipingwe kwa kuwa wanaonekana kujifaidi binafsi na washirika wao.
“Utekelezaji wa ripoti hiyo ulilemazwa Raila alipokuwa akiwania wadhifa wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) kwa kuwa haingemfaidi binafsi. Kwa vile amerudi katika siasa za humu nchini sasa wamekubaliana itekelezwe,” asema Koli.
Miongoni mwa mapendekezo ya ripoti hiyo ni kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu ambao inasemekana kupangiwa Bw Odinga.
Seneta wa Busia, Okiya Omtatah, amepinga vikali makubaliano hayo, hasa kuhusu utekelezaji wa ripoti ya NADCO. “Yeyote anayepigia debe NADCO anapaswa kuondolewa katika ulingo wa umma. Raila Odinga na William Ruto wametangaza vita dhidi ya mustakabali wa nchi hii,” alisema.
Wadadisi wanasema kuwa utekelezaji wa baadhi ya mapendekezo ya NADCO utahitaji kura ya maamuzi na kutumia njia ya mkato kupitia bunge, kunaweza kufanya wazimwe na mahakama.
“Kwa sasa, sidhani Ruto anaweza kukubali kura ya maamuzi hasa baada ya kutofautiana na aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua. Atakuwa akialika vita vya ubabe ambavyo vinaweza kuacha nchi pabaya,” akasema Koli.
Ruto na Odinga wanasisitiza kuwa makubaliano yao si kwa ajili ya kugawana nyadhifa serikalini bali ni kuweka msingi wa mashauriano kuhusu masuala yanayowakumba Wakenya.
Odinga alisema kuwa makubaliano hayo ‘yataisaidia nchi yetu kupunguza mvutano’ na kwamba upinzani umetambua kuwa haitoshi ‘kusimama kando na kulaumu tu.’
Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanasema Raila na Ruto wametambua kuna kizingiti cha kisheria katika kutekeleza maazimio yao ya kuungana na ndio sababu walisuka makubaliano ya ndoa ya kisiasa isiyo rasmi.