Nenda basi uungane na Gachagua, ODM wamfokea Kalonzo
GAVANA wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyong’o Jumapili alimshutumu vikali Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka kwa kudai kuwa Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga aliusaliti Muungano wa Azimio kwa kuingia serikalini.
Bw Odinga na Rais William Ruto waliingia kwenye ukuruba wa kisiasa mnamo Ijumaa, makubaliano ambayo yatasababisha wawili hao wagawane nyadhifa serikalini.
Bw Musyoka aliwaongoza viongozi wengine wa Azimio kudai Bw Odinga ameusaliti muungano huo, akisema kuwa hakushauriana nao kabla ya kuanza mazungumzo na Rais Ruto.
“Kalonzo amekuwa akikutana na kila mtu akiwemo Rigathi Gachagua bila kushauriana na mtu yeyote lakini hatukulalamika. Tulikubali hiyo ilikuwa haki yake ya kidemokrasia,” akasema Profesa Nyongó kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.
“Iwe ametia saini makubaliano nao si hoja kwetu kwa sababu hatukumfuatilia,” akaongeza Profesa Nyongó.
Kiongozi huyo alimkaripia Bw Musyoka, akimtaka asome makubaliano kati ya ODM na UDA na kuelewa yaliyomo kabla ya ‘kupayuka’ hadharani.
“Makubaliano haya yana msingi wa demokrasia na yanasisitizia umoja wa nchi. Bado Kalonzo ana mwanya wa kuongea na Rais Ruto na Bw Odinga ili aungane nao kuamua mustakabali wa taifa letu,” akaongeza.
Akiongea baada ya muafaka kati ya Raila na Rais Ruto kutiwa saini, Bw Musyoka alilaumu ODM kutokana na kifo cha Azimio akisema wanatafakari kuenda kortini ili chama hicho kiachilie nyadhifa za kamati mbalimbali za bunge.
Alidai kuwa nyadhifa ambazo ODM inashikilia bungeni ni za upinzani na hawawezi kuhudumu kwenye nafasi hizo baada ya kuungana na serikali.
“Wiper imekuwa na subira sana kwa Azimio na tuliwashauri lakini hawakutusikia. Sasa wameungana na serikali na si vyema iwapo wataendelea kushikilia nafasi ambazo zimetengewa upinzani,” akasema Bw Musyoka.
Makamu huyo wa rais wa zamani alimlaumu Raila akisema kuwa amesaliti maisha ya walioandamana barabarani kutaka haki kuhusu uchaguzi wa 2022, wengine wakiuawa kikatili.