Jamvi La Siasa

Nitaunga mkono mgombea urais mwingi ikiwa atateuliwa kisayansi na njia “inayokubalika”

Na CHARLES WASONGA November 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa zamani wa Usalama  Fred Matiang’i amefichua yuko tayari kuunga mkono mtu mwingine atakayeteuliwa na Umoja wa Upinzani kupeperusha bendera kwenye kinyang’anyiro cha urais 2027 kufanikisha lengo leo la kupata ushindi.

Dkt Matiang’i, ambaye ni mgombeaji wa urais wa chama cha Jubilee, hata hivyo, alipendeza kuwa sharti upinzani uibue mbinu ya kisayansi, na itakayokubalika, kuendesha uteuzi wa mgombeaji huyo atakayepambana na Rais William Ruto debeni.

“Ndio kuna mwafaka miongoni mwetu kama vinara wa upinzani kwamba tunapaswa kuwa na mgombeaji mmoja wa urais ili tufaulu katika ajenda yetu ya kuiondoa serikali ya sasa mamlakani,” akasema Jumatano asubuhi kwenye mahojiano katika kipindi cha ‘Fixing The Nation” kwenye runinga ya NTV.

“Ikiwa mgombeaji huyo hatakuwa Fred Matiang’i nitamuunga mkono kwa heshima ya uamuzi wa Umoja wa Upinzani wenye mpango mmoja,” akasema Dkt Matiang’a, akijibu swali na Bishar Miriam mmoja wa wasimamizi wa kipindi hicho.

Lakini alitetea ufaafu wake katika mgombeaji wa urais kwa misingi kuwa anaelewa changamoto zinasibu taifa hili baada ya kuhudumu kama Waziri kwa miaka 10, chini ya utawala wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Mnamo Oktoba 30, mwaka huu, chama cha Jubilee kinachoongozwa na Bw Kenyatta, kilimwidhinisha rasmi Dkt Matiang’i kuwa mgombeaji wake wa urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Akiongea katika Mkutano wa Karaza Kuu la Kitaifa (NEC) ya chama hicho uliofanyika Nairobi, Katibu Mkuu Jeremiah Kioni alithibitisha kuwa waziri huyo wa zamani aliwasilisha ombi la kutaka kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho “na ombi lake likaidhinishwa kwa kauli moja.”

“Tumepokea na kukubali rasmi ombi kutoka kwa Dkt Fred Matiang’i kuhusu ndoto yake ya urais,” akasema.

Bw Kioni ambaye ni mbunge wa zamani wa Ndaragua, pia alitangaza kuwa NEC ilimteua Dkt Matiang’i kuwa Naibu Kiongozi wa Jubilee na mwakilishi wake katika mikutano ya Umoja wa Upinzani.

“Kwa sababu kiongozi wetu wa chama hatakuwa akipatikana kwa urais, Dkt Matiang’i, kama naibu wake ndiye atakuwa akiwakilisha Jubilee katika majukwaa ya upinzani.” akaeleza.

Akijibu swali kuhusu madai ya uwepo wa mgawanyiko katika mrengo wa upinzani, haswa baada ya kiongozi wa DCP kutaja Jubilee kama “wilbaro nyekundu”, Dkt Matiang’i alipuuzilia mbali madai hayo.