Raila alivyozima migawanyiko ODM
BAADA ya kurejea nchini kufuatia kushindwa kwake katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC), Raila Odinga alichukua hatua ya kuzima mgawanyiko uliokuwa umekumba chama chake cha ODM kuhusu ushirikiano na Rais William Ruto.
Hatua yake ilileta muafaka miongoni mwa viongozi wa chama hicho waliokuwa wakishikilia misimamo kinzani kuhusu iwapo ODM inapaswa kushirikiana na serikali ya Kenya Kwanza au la.
Mnamo Ijumaa, mirengo iliyokuwa imeibuka ndani ya chama hicho iliungana kushuhudia Raila akitia saini mkataba wa ushirikiano na Rais Ruto.
Hatua hiyo, ilitafsiriwa na wachambuzi wa siasa kama uamuzi wa kuimarisha ODM na kudhibiti malumbano yaliyokuwa yakihatarisha mshikamano ndani ya chama hicho.
Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, ambaye awali alikuwa ameapa kutoshirikiana na serikali ya Rais Ruto, ndiye aliyesoma makubaliano hayo, akisisitiza kuwa yalipitishwa na kamati zote kuu za chama.
Pia, Gavana wa Kisumu, Peter Anyang’ Nyong’o, ambaye alikuwa ameungana na Sifuna kupinga ushirikiano huo, alihudhuria hafla hiyo, ishara kwamba walikuwa wamelegeza misimamo yao.
“Mkataba huu unaonyesha ramani ya kushughulikia changamoto za kijamii, kiuchumi na kisiasa za Kenya. Zaidi ya hayo, tumetambua umuhimu wa kuanzisha jukwaa pana la ushirikiano kati ya mirengo yote za kisiasa,” alisema Nyong’o.
Mchanganuzi wa siasa, Lawrence Igambi, anasema kulegeza msimamo kwa Sifuna na Nyong’o kulionyesha kuwa ODM ni chama kinachomilikiwa na Raila Odinga kwa kiwango cha kwamba wafuasi wake lazima wafuate amri zake.
“Raila ndiye mwenye ODM na wengine ni sawa na wafanyakazi wake. Lazima wafuate amri zake, na ndio sababu Sifuna na Nyong’o walilegeza misimamo,” alisema Bw Igambi.
Aidha, wadadisi wa siasa wanasema makubaliano yaliyosomwa katika Ukumbi wa Kimataifa wa Kenyatta (KICC) yalizingatia maoni ya Sifuna na kundi lake zaidi ya wale waliokuwa wakishinikiza ushirikiano kwa maslahi yao binafsi.
Bw Igambi anasema Raila alitumia uzoefu wake wa kisiasa kuwaingiza boksi waliokuwa wakipinga ushirikiano wake na Rais Ruto huku akidumisha umoja chamani.
Raila alionekana kucheza karata ndani ya chama kwa kutozima kabisa tofauti zilizoendelea kati ya viongozi wakuu alipokuwa akiwania wadhifa wa AUC.Alionekana kuacha hali ya suitafahamu ndani ya chama kwa kile ambacho wadadisi wa siasa wanasema ni kupata faida za kisiasa kutoka kwa pande zote mbili.
Baadhi ya makubaliano yake na Ruto ni kushirikiana kutoa na kujenga uwekezaji wa kiuchumi na ujumuishaji wa vijana katika sekta za kiuchumi mbali na kulinda na kuheshimu katiba na utawala wa sheria, kukomesha utekaji nyara, kukomesha ukandamizaji na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari, maovu ambayo Sifuna na mrengo wake wamekuwa wakiibua.
“Watu walikuwa wakishangaa ni kwa nini Raila alikuwa akinyamaza wanachama wa ODM wakitofautiana hadharani lakini alijua alichokuwa akikifanya. Kwa sasa, ametumia maoni ya mirengo yote miwili kujinufaisha. Kwanza, kwa kuonyesha Rais Ruto kwamba anatambua mchango wake na kushukuru kwa kumuunga mkono katika azma yake ya AUC na pili katika kujisawiri kama mtetezi wa raia katika hatua yake ya kushirikiana na serikali,” alisema mdadisi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.
Migawanyiko iliyovuma huku baadhi ya wanachama wakitaka Sifuna avuliwe wadhifa wake wa katibu mkuu wa ODM imetulia. Hata hivyo, Sifuna alisisitiza kuwa alikuwa akitekeleza maagizo ya Raila.
Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa hatua ya Raila Odinga kutoingilia moja kwa moja mivutano ya ODM ilikuwa mkakati wa kusawazisha maslahi yake binafsi na ya kisiasa. .Huku hali ikionekana kutulia kwa sasa, bado kuna maswali mengi kuhusu mustakabali wa ODM na ushirikiano wake na serikali.
Je, ODM itatoa mgombea urais katika uchaguzi mkuu ujao au itaungana na Kenya Kwanza?“Lakini ieleweke kuwa huu ni mkataba (MoU) wala sio muungano kati ya ODM na UDA. Lakini utekelezaji wa yaliyomo unaweza kuishia katika kuundwa kwa muungano ambao utaendelea kuleta utulivu nchini katika miaka ijayo,” Bw Odinga alifafanua.