Jamvi La Siasa

Raila amekuwa ‘rais- mwenza’ wa Ruto kupitia mkataba

Na BENSON MATHEKA,CHARLES WASONGA March 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga jana walitia saini rasmi Mkataba wa Maelewano (MoU) kujumuisha chama cha Orange Democratic Movement (ODM) katika utawala wa Kenya Kwanza.

Makubaliano hayo yaliashiria rasmi ushirikiano wa viongozi hao wawili kama vinara serikalini huku wakiahidi kushauriana na kushirikiana katika kufanya maamuzi muhimu.

“Hivyo basi; Sisi Mheshimiwa Rais Dkt William Samoei Ruto, CGH, na Mheshimiwa Raila Odinga, EGH, tukiwa viongozi wa vyama vikubwa zaidi vya kisiasa nchini Kenya, na kubeba jukumu kubwa zaidi la kisiasa, tunatambua haja ya kuweka jukwaa pana la ushirikiano na mashauriano kati ya mirengo ya kisiasa na wadau wengine katika jamii ya Kenya ili kukabiliana na changamoto za muda mrefu zinazotishia taifa letu,” wawili hao walisema katika mkataba wao.

Japo walisema hawakuwa wakiunda serikali ya muungano, makubaliano yao na utekelezaji, yalionyesha watakuwa wakishauriana katika masuala yanayohusu maslahi ya kitaifa kama vinara wenza.

“Hivyo basi, viongozi hawa wawili wanajitolea na kuazimia kushirikiana kwa kufanya mashauriano mapana baina yao kuhusu masuala muhimu,” yalisema makubaliano yao waliyotia saini katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta, Nairobi na kushuhudiwa na maafisa na wabunge wa vyama vyao.

“Tutakuwa tukifanya mashauriano ya kila mara huku tukiwaelekeza wataalamu kutoka mirengo ya ODM na UDA katika kuendesha serikali,” akasema.

“Lakini ieleweke kwamba hii ni MOU wala sio muungano kati ya ODM na UDA. Lakini utekelezaji wa yaliyokomo unaweza kupelekea kuundwa kwa muungano ambao utaendelea kuleta utulivu nchini katika miaka ijayo,” Bw Odinga akafafanua.

Masuala hayo ni utekelezaji kamili wa ripoti ya Kamati ya Mdahalo ya Kitaifa (NADCO). Walisema masuala katika NADCO watakayopatia kipaumbele ni gharama ya maisha, ukosefu wa ajira kwa vijana, kuanzisha mfumo wa utekelezaji wa kanuni ya kijinsia ya thuluthi mbili, ushirikishaji katika nyanja zote za maisha ya umma na kulinda na kuimarisha ugatuzi.

“Ugatuzi lazima uendelee kulindwa, na juhudi zaidi lazima ziwekwe katika kusambaza fedha zote zinazotengewa kaunti, kuongeza mgao wa bajeti kwa kaunti na kuhakikisha utoaji fedha zilizogatuliwa kwa wakati,” walisema.

Ruto na Raila pia walikubali kuongeza ushirikishaji miongoni mwa Wakenya bila kujali dini zao. Kulingana na viongozi hao, kuimarika kwa ujumuishaji kutaboresha fursa kwa Wakenya wote katika uteuzi wa umma.

Walikubali kushauriana kufanikisha ushirikishaji katika nyanja zote za maisha ikiwemo katika mgao wa bajeti na uteuzi wa nyadhifa serikalini

Katika MoU iliyosomwa na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, akishirikiana na mwenzake wa UDA Hassan Omar, Raila na Ruto pia walikubali kukuza uongozi na uadilifu na kutoa mfumo wa kisheria wa kushughulikia migogano ya maslahi ndani ya taasisi za serikali.

Viongozi hao wawili pia walikubaliana kulinda na kuendeleza utawala wa sheria na kuzingatia Katiba.

“Ushirikiano kati ya viongozi hao wawili utaafikia malengo yake kwa kufanya mashauriano ya mara kwa mara kuhusu masuala muhimu ya

maslahi kwa watu wa Kenya; kubadilishana utaalamu na taarifa kuhusu uzoefu katika utawala wa Jamhuri ya Kenya,” walisema katika mkataba wa ushirikiano wao.

Zaidi ya hayo, katika makubaliano hayo, pia walitoa wito kwa serikali kuheshimu haki ya kuandamana kwa amani.

Rais Ruto na Bw Odinga pia walikubaliana kukagua deni la taifa na kuelezea jinsi kila deni lililochukuliwa na Kenya lilivyotumika.

“Viongozi hao walikubaliana kukomesha ufisadi nchini na kukomesha ufujaji wa rasilimali za umma, hasa na viongozi ndani ya serikali. Chini ya Serikali Jumuishi, wawili hao pia walikubaliana kulinda ugatuzi kama inavyohitaji Katiba ya 2010 iliyoruhusu kuanzishwa kwa Kaunti 47,” mkataba wao ulisema

Mkataba huo ulijiri siku moja baada ya waziri mkuu huyo wa zamani kuhitimisha ziara yake ya mashauriano ya wiki mbili kote nchini huku akitafuta maoni ya Wakenya kuhusu mwelekeo wa kisiasa.

Viongozi hao wawili pia walikubaliana kushirikiana kutoa na kujenga uwekezaji wa kiuchumi na ujumuishaji kwa vijana na kulinda mamlaka na kuheshimu katiba na utawala wa sheria, kukomesha utekaji nyara, kukomesha ukandamizaji na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari.