Raila anapanga nini kukosoa vikali Ruto
KWA mara nyingine tena kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ametofautiana na Rais William Ruto akikosoa vikali mpango wa nyumba za bei nafuu ambao kiongozi wa nchi amekuwa akitetea.
Licha ya wawili hao kuwa na mkataba wa ushirikiano serikalini, Bw Odinga anaendelea kutofautiana na Rais Ruto kuhusu baadhi ya masuala yenye umuhimu kwa taifa huku maswali yakiibuka kuhusu anacholenga.
“Kuna kitu ambacho Raila analenga. Ukosoaji wake wa Rais huku wakila meza moja sio wa bure,” asema mdadisi wa siasa Muli Koli.
Raila amekuwa na msimamo tofauti na rais kuhusu Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge na Hazina ya Ukarabati wa Barabara za Mashinani anazosema zinapaswa kuwa chini ya magavana.
Hii ni tofauti na Rais Ruto ambaye amewaambia magavana waache kushinikiza hazina hiyo akisema ikiwa chini ya Serikali ya Kitaifa miradi itatekelezwa kwa ufanisi na bila kuchelewa.
Ijumaa, Bw Odinga alikosoa mradi muhimu zaidi wa Rais Ruto wa nyumba za bei nafuu akidai unapaswa kusimamiwa na serikali za kaunti badala ya serikali kuu.
Akizungumza katika mazishi ya Francis Ngaru, mume wa aliyekuwa Meya wa Thika Mumbi Ngaru, Raila alisisitiza umuhimu wa ugatuzi na kuhimiza kuongezwa kwa mamlaka na rasilmali kwa kaunti.
“Na kuhusu nyumba za bei nafuu? Wacheni kaunti zijenge zenyewe!” Raila alisema.
Mpango wa Nyumba Nafuu ni mojawapo ya miradi mikuu ya serikali ya Rais Ruto inayolenga kukabiliana na upungufu wa nyumba nchini kwa kujenga nyumba 200,000 kila mwaka, na kufikia nyumba milioni moja ifikapo mwaka 2027.
Kauli ya Raila inajiri siku moja baada ya Rais Ruto, katika hotuba yake ya wakati wa maadhimisho ya Leba Dei kupigia debe mpango wa nyumba za bei nafuu akisema umesaidia kuunda nafasi zaidi ya 150,000 za ajira.
Raila pia alishinikiza kuongezwa kwa mgao wa fedha kwa serikali za kaunti kutoka asilimia 15 hadi kati ya 35 na 40, akisema kiwango cha sasa hakitoshi kuleta maendeleo ya maana mashinani.
Aidha, alitaka serikali kuu iachane kabisa na ujenzi wa barabara za kaunti na kuvunjwa kwa mamlaka za KURA na KeRRA, akisema barabara ni huduma iliyo chini ya ugatuzi.
“Barabara pia zimegatuliwa. Hamhitaji KURA na KERRA. Serikali kuu iwe tu na KeNHA kushughulikia barabara kuu za kimataifa, barabara kuu za kitaifa na zile za kuunganisha maeneo,” alisema.
Alitoa mfano wa barabara jijini Nairobi, akimtetea Gavana Johnson Sakaja akisema hawezi kulaumiwa kwa masuala ya barabara iwapo kazi hiyo bado iko chini ya serikali kuu.
“Tukikubali ugatuzi ufanye kazi na kuongeza mgao wa fedha kwa kaunti, ndipo tunaweza kulaumu magavana wasipofanya kazi. Lakini hauwezi kulaumu Gavana Sakaja kwa barabara za Nairobi zisizo chini yake,” aliongeza.
Raila amekuwa mstari wa mbele kutetea ugatuzi, akipinga jaribio lolote la kupokonya kaunti mamlaka yao.
Amewahi pia kuwaonya wabunge na wagombea wa chama cha ODM kuwa msimamo wao kuhusu masuala ya ugatuzi utazingatiwa wakati wa uchaguzi wa chama.
Wachanganuzi wanahisi kuwa Raila anamshinikiza Ruto kutimiza makubaliano ya mkataba wa ushirikiano kati ya UDA na ODM waliotia saini Machi 7 mwaka huu.
“Naona Raila yuko ndani ya mkataba wake wa maelewano na Rais Ruto kwa kuwa walikubaliana kuimarisha ugatuzi. Hii ndiyo sababu anahimiza serikali ikome kukwamilia majukumu ya serikali za kaunti kama barabara na ujenzi wa nyumba,’ anasema mchambuzi wa siasa Arnold Otieno.
Raila na Ruto walikubaliana kuhamishia kaunti majukumu yote yaliyogatuliwa ikiwa ni pamoja na kuongeza mgao kwa kaunti, kuwezesha vijana na fursa za kiuchumi, kuhakikisha maadili na heshima serikalini, kulinda haki za kukusanyika na kuandamana kwa amani, kuheshimu demokrasia ya vyama vingi na mjadala kuhusu ushirikiano wa kitaifa.
Kulingana na mchanganuzi wa siasa, Dkt Isaac Gichuki huenda Raila analenga kuonyesha Wakenya kwamba mkataba wake na Ruto haukuwa tu wa uhusiano mwema.
“ Tatizo ni kwamba ukuruba wake na serikali umepaka tope sifa zake na sasa anaweza kuamua kutumia wakati huu kujikomboa,” asema.