Raila anavyotumiwa na kutupiliwa mbali
KWA miaka mingi, Raila Odinga amekuwa mtu anayezua joto na midahalo katika siasa za Kenya, hasa katika eneo la Mlima Kenya.
Kwa wakati huu wakosoaji wake wanamlaumu kwa usaliti kwa kushirikiana na mahasimu wake wa kisiasa ambao katika kura za urais huwa wanajitenga na mrengo wake.
Hata hivyo, wachanganuzi wa siasa wanasema ni Raila ambaye amekuwa akisalitiwa na kutumiwa na tabaka la wanaotawala na kujitenga naye hakusaidii mustakabali wa Kenya.
“Kukataa kumuunga mkono Raila, hasa na wakazi wa Mlima Kenya, mara nyingi kumeelezwa kama upinzani dhidi ya sera zake au uongozi wake. Hata hivyo, hoja hii inapuuza historia na ukweli ambao umedhihirika hivi karibuni kwamba huwa anatumiwa wakati wa kampeni na baada ya uchaguzi,” asema mchanganuzi wa siasa Morris Kago
Anarejelea kauli za mfanyabiashara S. K. Macharia, aliyefichua wiki iliyopita kuwa kila uchaguzi unapofanyika, Raila huwa ananyimwa ushindi kura za urais.
“Hili linatulazimisha kukabiliana na ukweli wa kihistoria. Jaribio la Raila la kuingia Ikulu halifeli kwa sababu ya kukosa maono au mvuto wa kitaifa, bali kwa sababu ya mifumo thabiti ya mamlaka, inayoungwa mkono na wale wanaomshutumu kwa usaliti,” asema.
Raila amelaumiwa kwa kusaliti washirika wake katika miungano ya kisiasa anayounda kabla ya kila uchaguzi mkuu.
Dhana kwamba Raila husaliti washirika wake haina mantiki. Ikiwa kuna mtu ambaye anaweza kudai kusalitiwa, ni Raila mwenyewe. Handisheki yake mwaka wa 2018 na Uhuru Kenyatta, ambayo iliweka mbele umoja wa kitaifa kuliko tamaa zake binafsi, ilizua ghadhabu kutoka kwa washirika wake waliosema aliwatenga. Na sasa, ushahidi wa udanganyifu uchaguzini uliofichuliwa na Macharia unaonyesha kuwa ni Raila anayesalitiwa.
Ingawa tabaka la watu wenye ushawishi mkubwa Mlima Kenya, kwa muda mrefu limemsawiri Raila kama tishio kwa utulivu, viongozi hao hao humtafuta washirikiane kutimiza maslahi yao ya kibinafsi.

Handisheki, ambayo ilituliza nchi baada ya uchaguzi wa 2017, ilipangwa na viongozi wa Mlima Kenya ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakimtaja Raila kama tishio. Vile vile, Rais William Ruto, ambaye alijijenga kisiasa kwa kumpinga Raila, alimkaribisha kwenye mazungumzo kupitia Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (Nadco) na sasa wanashirikiana katika serikali.
Wanasiasa hawa hutumia jina la Raila kuwachochea wafuasi wao, kisha kimyakimya wanamsihi ajiunge nao wanapohisi utawala wao unayumba.
“Raila hutajwa kama adui wa taifa hadi pale ambapo mtaji wake wa kisiasa unahitajika ili kuhalalisha sera tata au kuleta utulivu serikalini. Mpango wa Maridhiano (BBI), ulioungwa mkono na Uhuru na Raila, ni mfano bora wa hili,” asema Kago.
Mpango huo ulisukwa na Uhuru kuthibiti serikali yake alipotofautiana na naibu wake William Ruto katika muhula wa pili wa utawala wa Jubilee.
Ruto naye aliunda Nadco serikali yake ilipotikiswa na akamwendea Raila vijana walipoandamana na alipotofautiana na naibu wake Rigathi Gachagua. Alisaidiwa na Raila kumtimua Gachagua ofisini. Licha ya kumshambulia vikali wakati wa kampeni na alipokuwa serikali, Gachagua alimrushia Raila chambo alipotimuliwa waungane dhidi ya Ruto. Raila amekataa.
“Wanasiasa huchochea chuki dhidi ya Raila wakati wa uchaguzi, wakimtaja kama tishio kwa maslahi ya umma. Lakini kweli ni kwamba ni tabaka tawala linalomsaliti kwa kumnyima nafasi ya kutawala kisha linamtumia hali ikiharibika,” asema mdadisi wa siasa Musili Koli.
Anasema kwamba ushawishi wa Raila hauwezi kupuuzwa katika siasa za Kenya. “Ni kiongozi aliye na ufuasi mkubwa katika Nyanza, Magharibi, na Pwani, na hakuna serikali inayoweza kuwa thabiti bila kushirikiana na maeneo haya,” asema.