Raila atakavyoamua mshindi wa urais 2027
KIONGOZI wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga huenda akatekeleza wajibu wa kuamua mshindi wa urais katika uchaguzi mkuu wa 2027, mmoja wa maafisa wakuu wa chama hicho amedokeza.
Naibu Kiongozi wa ODM Godfrey Osotsi, kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, amefichua kuwa azma ya Odinga ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) haitabadili hadhi yake kama kiongozi wa ODM na hata mwaniaji wake wa urais.
Lakini Bw Osotsi, ambaye ni Seneta wa Vihiga aliongeza kuwa Bw Odinga anaweza kuketi “kando ya uwanja na kutekeleza wajibu wa kocha” katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Anaeleza kuwa Waziri huyo Mkuu wa zamani anaweza kurejelea nafasi yake ya mnamo 2002, alipotamka “Kibaki Tosha” na kumwezesha Hayati Mwai Kibaki kuibuka mshindi. Ushindi huo ulitamatisha utawala wa miaka 40 ya chama cha Kenya African National Union (Kanu).
“Wafaa kujua kuwa Raila akiwa kocha yeye ni hatari zaidi kuliko wakati ambapo yeye ni mchezaji. Uliona 2002 aliposema Kibaki Tosha na kujitwika wajibu wa kocha na ukaona jinsi alishinda uchaguzi kwa kishindo.
“Kwa hivyo nataka kuwaambia wanachama wetu kote nchini kwamba kiongozi wetu wa chama akiwa mwenyekiti wa AUC atakuwa na manufaa makubwa kwa chama kuliko vile watu wengine wanasema kwani atakuwa ataitumia nafasi hiyo kuifaidi ODM hata zaidi,” Bw Osotsi akasema.
Wandani wa Bw Odinga wanaoshikilia nyadhifa za uwaziri katika serikali ya Rais Ruto wamejitokeza katika watetezi sugu wa serikali ya Rais Ruto. Baadhi yao hata wamedokeza kuwa wataunga mkono juhudi zake za kutaka kuhifadhi kiti chake katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Na wiki jana, kaimu kiongozi wa ODM Profesa Anyang Nyong’o alisema kuwa ingawa chama hicho hakitaki kuonekana kuwa duni au kuendeleza masilahi ya vyama vingine vya kisiasa anaelewa hitaji la chama hicho kubuni ushirikiano wa “kimkakati” na vyama vingine.
Profesa Nyong’o ambaye ni Gavana wa Kisumu alionekana kuashiria uwezekano wa ODM kuweka mkataba wa ushirikiano na chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Rais William Ruto.
“Kama chama cha kisiasa, tunaeleza manufaa ya kuingia katika ushirikiano na vyama vingine. Nyakati fulani tunaweza kuamua kubuni miungano na vyama vingine au makundi yenye malengo na maono sawa nasi kuhusu namna ya kuendesha Kenya,”
Profesa Nyong’o akaongeza hivi: “Miungano au ushirikiano aina hii sio vitendo vya kutumikia vyama vingine lakini juhudi za kimakusudi za kufikia lengo letu la kimsingi wa kutwaa mamlaka ya kisiasa ili kubadilisha maisha ya Wakenya.
Kauli ya kaimu huyo wa kiongozi wa ODM inaonekana kuhimili kaunti za Bw Osotsi.