Jamvi La Siasa

Rais azongwa na mlima wa kesi, Gachagua aonekana ‘kuchelewesha’ kuondoka kwake

Na JUSTUS OCHIENG October 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto anazongwa na mizozo mingi ya kisheria na kisiasa inayoongezeka kila uchao kesi kuhusu kuondolewa kwa naibu wake Rigathi Gachagua zikiwa za hivi punde.

Hata baada ya kushinda kesi ya ushuru wa Nyumba Mahakama Kuu ilipoamua Jumanne kuwa sheria iliundwa kikatiba, mzozo huo unaonekana kuelekea katika mahakama ya Rufaa baada ya Dkt Magare Gikenyi na walalamishi wengine kuapa kupinga uamuzi huo.

Wiki iliyopita, jaji alilazimika kuahirisha kusikilizwa kwa kesi ya kupinga mipango ya serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Ruto kukodisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kampuni ya Adani Group baada ya watu kuvamia kikao cha mtandaoni wakipiga kelele “Adani lazima aende!” na ‘JKIA haiuzwi.’

Uzinduzi wa Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF) pia bado haujakamilika huku Mahakama Kuu ikitarajiwa kuamua iwapo itausimamisha kwa muda, hatua ambayo inaweza kuwa pigo kubwa kwa mpango huo.

Mnamo Jumapili Rais Ruto alihakikisha kwamba katika muda wa wiki mbili, SHIF itakuwa ikifanya kazi vyema, na kuongeza kwamba wafanyikazi wa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) hawatapoteza kazi zao.

Mapema mwezi huu, rais alipata pigo baada ya Mahakama Kuu kusimamisha kwa muda muundo mpya wa ufadhili wa elimu wa vyuo vikuu baada ya mashirika matatu kuupinga kwa msingi ulikuwa kinyume cha katiba.

Rais pia anakabiliwa na shinikizo kutoka kwa wabunge kuhusu kuwekwa katika katiba Hazina ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneobunge ya Serikali (NG-CDF) baada ya Mahakama Kuu kutangaza kuwa ni kinyume cha katiba.

Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA