Jamvi La Siasa

Rigathi anavyojiongezea bei kuhusu tiketi ya urais

Na BENSON MATHEKA September 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Tangazo la aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kwamba atagombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2027 limetajwa na wachambuzi wa siasa kama mbinu ya kujiongezea bei kisiasa katika majadiliano na vinara wenzake wa upinzani.

Ingawa Gachagua alitimuliwa kutoka kwa wadhifa wake mnamo Oktoba 2024, hatua yake ya kutangaza azma ya kugombea urais imewaacha wengi vinywa wazi, huku wengine wakisema ni mkakati wa kukita sauti yake katika mustakabali wa siasa za kitaifa.

Kisheria, mtu akitimuliwa ofisini kupitia mchakato wa bunge hawezi kugombea kiti au kushikilia wadhifa wa umma kwa kipindi cha miaka kumi iwapo hataondolewa lawama na mahakama. Gachagua amewasilisha kesi kortini ambayo haijaamuliwa na baadhi ya wachambuzi wa siasa wanasema hii inamwezesha kugombea.

“Mwaka 2027 nitakuwa kwenye debe,” alisema wiki hii akiwa Karatina japo awali alikuwa amesema eneo la Mlima Kenya haliwanii kutoa mgombea urais katika uchaguzi mkuu ujao akisisitiza kuwa lengo lake ni kuunganisha upinzani umfanye Rais William Ruto kuhudumu kwa muhula mmoja pekee.

Kabla ya tangazo lake wiki jana, Gachagua aliwahi kunukuliwa akisema kuwa eneo la Mlima Kenya halina tamaa au ukabila kwamba haliwezi kuunga mgombea urais kutoka maeneo mengine.

Kauli yake kwamba atagombea imechochea mijadala mikali katika safu za kisiasa, huku wachambuzi wakisema ni mkakati wa kujenga ushawishi kujadiliana na vinara wa upinzani, na kuwa na usemi mkubwa katika maamuzi ya mustakabali wa taifa iwapo watafaulu kumshinda Rais William Ruto.

Gachagua anatoka katika eneo la Mlima Kenya, mojawapo ya maeneo yenye idadi kubwa ya wapiga kura nchini. Katika uchaguzi mkuu wa 2022, eneo hilo lilichangia zaidi ya kura milioni 5.4, sawa na karibu asilimia 32 ya kura zote nchini, kulingana na takwimu za IEBC.

Kura hizi ziligawanyika katika maeneo ya kaunti kama Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Embu, Meru, Tharaka Nithi na Laikipia.Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa Gachagua anatumia mbinu kadhaa za ujanja wa kisiasa ikiwemo kuondolewa madarakani kama kisingizio cha kuwa alidhulumiwa na sasa kutangaza atawania urais ili kuongeza mtaji wake katika siasa za upinzani na kufurahisha ngome yake ione kwamba ina usemi katika muungano wa upinzani.

“Hii humfanya apate huruma na ufuasi kutoka kwa wale wanaoamini kuwa serikali haikuwa na haki kumtimua, eneo lake lisimame nyuma yake na kutenga vyama vingine vyenye mizizi eneo la Mlima Kenya,” asema mchanganuzi wa siasa Peter Warukira.

Mbinu ya Rigathi Gachagua ya kutangaza kugombea urais imegeuka kuwa kitovu cha mazungumzo ya kisiasa nchini. Kwa kuzingatia uzito wa Mlima Kenya kisiasa, kauli za vinara wa upinzani, na matarajio ya kura milioni 5.4 kutoka eneo hilo, ni wazi kuwa Gachagua anachora ramani ya kisiasa kwa ustadi mkubwa.Haijalishi iwapo atakuwa mgombea urais kwa sasa, Gachagua anajiweka kama mmoja wa watu wa kuzingatiwa katika safari ya kuelekea 2027.

Bw Gachagua ameahidi kurudisha nchi pale ambapo hayati Mwai Kibaki aliiacha akichaguliwa kuwa rais.Akizungumza katika ibada ya kanisani huko Nyeri , Septemba 14, 2025, Gachagua aliwaambia waumini kuwa alikuwa amerudi nyumbani kuomba baraka kabla ya kuanza safari yake ya kuzunguka taifa akitafuta uungwaji mkono wa azima yake ya urais.

“Nimerudi nyumbani kuomba baraka kabla ya kuanza safari hii. Nilihitaji baraka kutoka nyumbani kabla ya kuanza safari hii,” alisema.Aliongeza kuwa jambo la pekee atakalofanya ni kuirudisha nchi pale ambapo marehemu Rais Mwai Kibaki aliiacha mwaka 2013.

Aidha, aliahidi kufufua mfumo wa huduma za afya, akisema kuwa serikali yake itahakikisha hospitali zina dawa za kutosha na mpango wa bima ya afya unafanya kazi ipasavyo.

“Sitaki kuambia nchi uongo kwamba nitajenga barabara, mabwawa au miradi ya umeme endapo Wakenya watanichagua kuwa rais. Sitaki kutoa ahadi za uongo kwa watu wa Kenya,” alisema.

“Ninachotaka tu ni kuirejesha Kenya pale Mwai Kibaki aliiacha. Na baadhi ya mambo tunayonuia kufanya ni pamoja na kufufua mfumo wa afya ili tukienda hospitalini, dawa zipatikane; na pia kurejesha elimu bila malipo kama alivyoacha Kibaki,” aliongeza.

Pia aliahidi kurejesha heshima ya mshahara (payslip), akisema kuwa wafanyakazi wengi wa Kenya kwa sasa hawana uwezo wa kutumia mishahara yao kwa sababu ya ushuru mkubwa unaokatwa.

“Rigathi Gachagua anataka kurejesha heshima ya payslip. Wakenya wengi wameporwa mishahara yao kiasi kwamba hawana tena uwezo wa kununua bidhaa,” alisema.Haya yanajiri wakati ambapo muungano wa upinzani umekuwa ukifanya mikutano ya mara kwa mara kuamua ni nani atakuwa mgombea wao wa urais atakayekabiliana na Rais William Ruto mwaka 2027.

“Na sasa Wakenya wameniambia baada ya kupima wameona dawa ya kufukuza Kasongo ni Riggy G, kwa hivyo Wakenya wameniambia nipiganie kiti cha urais wa Jamhuri ya Kenya.

”Haya yanajiri siku chache baada ya Gachagua kuwaambia wafuasi wake wampigie kura mgombea yeyote atakayeteuliwa na upinzani, hata kama si yeye.Akizungumza katika ibada ya kanisani huko Nyandarua Septemba 7, 2025, aliwataka wakazi wa Mlima Kenya wamchague yeyote ambaye muungano wa upinzani utaamua kumpa tiketi ya kuwania urais.

Kwa mujibu wa Gachagua, licha ya kuwa yeye pia ni miongoni mwa wanaotaka kuwania urais, wamekubaliana kama vinara wa muungano wa upinzani kuwa wakati ukifika, wataafikiana kumuunga mkono mgombea mmoja na kuacha tamaa zao binafsi.“

Na tumekubaliana tutatoa mwaniaji mmoja; tukiamua ni Kalonzo, tutampigia yeye kura; tukisikizana ni Matiang’i, sisi tutampigia kura; iwe ni Eugene, Martha Karua na mimi pia tutampigia kura.”