Rigathi avamia ngome ya Naibu Rais Kindiki
HUKU tarehe anayotarajiwa kuzindua chama chake cha kisiasa ikikaribia, aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua ameanza kutandaza mizizi yake katika eneo la Mlima Kenya Mashariki, hatua inayochukuliwa na wachambuzi wa siasa kama pigo kwa ushawishi wa mrithi wake Profesa Kithure Kindiki anayetoka eneo hilo.
Bw Gachagua, ambaye kwa muda sasa amekuwa akijitokeza kama kiongozi mwenye ushawishi mkubwa wa kisiasa ndani ya eneo la Mlima Kenya, ameendeleza mikutano ya mashauriano na viongozi wa maeneo mbalimbali, mtindo unaotafsiriwa kama mikakati ya kisiasa ya kujenga mtandao mpya wa uungwaji mkono.
Mnamo Ijumaa, Gachagua aliandaa kikao cha mashauriano katika makazi yake ya Wamunyoro na ujumbe wa viongozi kutoka Kaunti ya Embu, wakiongozwa na Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji.
Ingawa kikao hicho kilielezewa kuwa ni cha kusikiliza matatizo ya wananchi, wachanganuzi wanasema ni hatua ya makusudi ya kisiasa inayolenga kujiimarisha katika ngome za Profesa Kindiki ya Mlima Kenya Mashariki ambayo inajumuisha kaunti tatu za Embu, Meru na Tharaka Nithi.
Profesa Kindiki anatoka Tharaka Nithi na amekuwa akijitahidi kuimarisha ushawishi wake katika eneo hilo.Baada ya kukutana na ujumbe kutoka Embu, Bw Gachagua alisema, “Nimesikia kilio cha watu wa Embu. Nitakuwa pamoja nanyi kila hatua ya safari hii kuelekea Kenya bora ambapo hakuna yeyote atakayeachwa nyuma.”
Mnamo Jumatano, Gachagua alikutana waliokuwa mawaziri Mithika Linturi na Justin Muturi katika kile kinachoonekana kujiimarisha katika eneo la Mlima Kenya Mashariki. Linturi anatoka Meru na Muturi anatoka Embu.Wiki moja kabla ya mkutano huo, Gachagua alikuwa amekutana na viongozi kutoka Kaunti ya Meru, akiwemo Linturi.
Linturi, ametangaza kuvunja uhusiano wake na Kenya Kwanza. Wiki jana, Bw Gachagua alitangaza kuwa waziri huyo wa zamani wa kilimo atashikilia wadhifa wa juu katika chama kipya cha kisiasa anachotarajia kuzindua Mei 15.
Duru zinasema Muturi na Linturi wameanza kushiriki vikao vya kisiasa vya faragha vinavyoongozwa na Gachagua, wakijaribu kujijenga upya baada ya kutengwa serikalini.
“Ushirikiano wa Muturi, Linturi na Gachagua unaleta sura mpya ya kisiasa inayoibuka katika Mlima Kenya, ambapo viongozi waliokuwa waaminifu kwa Rais Ruto sasa wanaelekea upinzani.
Ushawishi wa Linturi na Muturi eneo la Mlima Kenya Mashariki hauwezi kupuuzwa,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt James Waciara.
Anasema wawili hao na Bw Gachagua walikuwa katika msitari wa mbele kumpigia debe Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027. Wiki hii, viongozi wa Meru walikataa mwaliko wa Rais Ruto ikulu kwa sababu ya kutotimizwa kwa miradi ya maendeleo.
Dkt Waciara anasema anayepoteza katika mpangilio mpya wa kisiasa ni Profesa Kindiki ambaye akiwa kiongozi anayeshikilia wadhifa wa juu serikalini kutoka eneo la Mlima Kenya Mashariki anatarajiwa kuliunganisha nyuma yake na Rais Ruto.
“Kilicho wazi ni kuwa Gachagua anaendelea kuvamia maeneo yanayopaswa kuwa chini ya ushawishi wa Kindiki. Gachagua anaonyesha wazi kuwa analenga kuunganisha Mlima Kenya mzima nyuma yake na hii ni pigo kwa Kindiki,” asema.
Gachagua amekuwa akidai Rais Ruto analenga kugawanya Mlima Kenya ili kupunguza ushawishi wa eneo hilo katika uchaguzi.Hata hivyo Profesa Kindiki anasisitiza wakati wa siasa haujafika.
“Wakati wa siasa utakuja. Sio kwamba hatujui siasa; tunajua kwamba kila jambo lina wakati wake. Huu ni wakati wa kujenga barabara, masoko na kupeleka stima kwa wananchi,” alisema akiwa kaunti ya Nyandarua Ijumaa.
Aliongeza: “Wanaotaka siasa wasubiri 2027; tutakutana uwanjani. Kazi yangu ni kusaidia Rais kutekeleza miradi ya maendeleo, kuboresha bei za mazao na kuhakikisha kila sehemu ya nchi inapata maendeleo.”