Jamvi La Siasa

Ruto akanyaga barabara telezi kurejea Mlimani

Na  MWANGI MUIRURI March 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KATIKA kile ambacho wachambuzi wengi wa siasa wanatafsiri kama kitendo cha ujasiri wa hali ya juu, Rais William Ruto anapanga kuzuru Mlima Kenya ambako anakabiliwa na upinzani mkubwa.

Hata hivyo, tarehe ya ziara yake ya siku sita bado haijathibitishwa, kwani washauri wake wanasema kuwa utekelezaji wa mpango huo utategemea hali—kimazingira na kisiasa.

Eneo hilo limebadilika kutoka kuwa ngome thabiti ya Ruto katika miezi sita iliyopita hadi kuwa moja ya ngome zake kali za upinzani, hali iliyochochewa na hatua ya kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua mnamo Oktoba 2024.

Gachagua aliondolewa mamlakani baada ya kuhudumu kwa miaka miwili pekee na nafasi yake kuchukuliwa na Profesa Kithure Kindiki, kutoka Kaunti ya Tharaka Nithi—hatua ambayo bado haijaponyesha vidonda vya kisiasa katika eneo hilo lenye idadi kubwa ya wapiga kura.

Ni katika muktadha huo ambapo ziara inayotarajiwa ya Rais inazua hisia tofauti, huku baadhi wakimtaka kuwa mwangalifu na wengine wakimsukuma kukabili hali hiyo moja kwa moja.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa siasa, John Okumu, Rais anaweza kutumia ushawishi wa mamlaka yake kurejesha umaarufu wake katika eneo hilo.

‘Anachopaswa kufanya ni kutumia hulka ya Gachagua ya kuzungumza sana na makosa yake mengi ili kuwafanya wafuasi wake wachoke naye na hatimaye waachane naye,’ alisema.

Bw Okumu anasema tishio kubwa kwa Rais katika Mlima Kenya ni Bw Gachagua, ‘ambaye kila siku anakaribia kutimiza lengo lake kuu la kuhakikisha serikali hii haichaguliwi tena.’

Anapendekeza Rais Ruto awekeze zaidi kwa wanasiasa waliobobea kutoka eneo hilo ambao wana uhusiano wa karibu na wananchi na rekodi ya kustahimili siasa za Mlima Kenya.

‘Ana wanasiasa wazuri upande wake,watu kama Rais wa zamani Uhuru Kenyatta, ambaye alikutana naye Ichaweri mwezi Desemba mwaka jana. Pia ana wanasiasa jasiri wanaojulikana kwa kusimama imara dhidi ya mawimbi ya kisiasa kama vile William Kabogo na Mwangi Kiunjuri,’ alisema.

Aliongeza kuwa Rais Ruto anapaswa kufuatilia kwa umakini ziara kwa Kenyatta na kugeuza mkutano wao wa mwisho Ichaweri kuwa faida yake katika Mlima Kenya.

Mchanganuzi wa siasa, Profesa Peter Kagwanja, anahisi kuwa Rais anapaswa kutafuta njia ya kurejesha imani ya wananchi kwa kutekeleza mambo muhimu kwao.

‘Anapaswa kuweka wazi mapema kuwa hatakuja Mlima Kenya kwa siasa za 2027. Ni lazima aende huko akionyesha ushahidi dhahiri kuwa anatekeleza mkataba wa kiuchumi aliotia saini na wananchi wa eneo hilo,’ alisema Prof Kagwanja.

Kwa mujibu wa Prof. Kagwanja, Mlima Kenya unategemea sera thabiti za uchumi wa kitaifa ambazo zinafungua fursa za biashara kote nchini.

‘Hii inamaanisha kuwa Rais anaweza kujipendekeza kwa Mlima Kenya kwa kurekebisha uchumi wa taifa, kupunguza ushuru mkali, na kulipa madeni ya serikali yaliyocheleweshwa akiwa Ikulu tu,’ alisema.

Kwa mtazamo huo, washauri wa Rais Ruto wanahisi wanaweza kupindua ushawishi wa Gachagua na kuimarisha tena umaarufu wa Rais katika eneo hilo.

Hata hivyo, Seneta wa Nyandarua, John Methu, ambaye ni mwandani wa Gachagua, anasema hiyo ni ndoto tu, kwani aliyekuwa Naibu Rais anaendelea kupata nguvu zaidi.

Bw Methu anasema Rais ‘amejitengea kitanda cha misumari katika Mlima Kenya, na lazima alale juu yake.’

‘Upuuzi,’ anajibu Mbunge wa Laikipia Mashariki, Mwangi Kiunjuri.

‘Bado kuna nafasi ya Rais kurejesha Mlima Kenya. Hatutakubali kuonekana kana kwamba kumuunga mkono na kumkaribisha Rais Ruto ni kosa,’ alisema Bw Kiunjuri.

Bw Kiunjuri anasema itakuwa kosa kubwa kwa wananchi wa eneo hilo kumdhalilisha Rais wakati wa ziara yake.

“Kuna maeneo mengine yanayomhitaji. Tusijifanye wajinga tusiojua jinsi rasilimali zinavyogawanywa kupitia ushawishi wa mamlaka ya juu,” alisema kiongozi wa chama cha The Service Party (TSP).

Lakini Seneta wa Murang’a, Joe Nyutu, ambaye ni mshirika wa Gachagua, anasema Rais Ruto anapanga ziara hiyo ili kuokoa sura yake kisiasa.

“Anajua wazi kuwa ametangaza vita vya kisiasa dhidi yetu kutoka Mlima Kenya. Katika Bunge la Kitaifa na Seneti, amekuwa akiwaondoa wandani wetu kwenye nyadhifa na kuwabadilisha na wafuasi wake kutoka maeneo mengine,”alisema Bw Nyutu.

“Watu wa kweli wamwambie Rais kuwa kumtimua Gachagua ilikuwa sawa na kutangaza vita dhidi ya Mlima Kenya—kitendo ambacho, iwapo tungalikuwa jeshini, kingetafsiriwa kama tamko la vita.”