Ruto alivyofaulu kuepuka aibu Mlimani
ZIARA ya siku sita ya Rais William Ruto katika maeneo ya Mlima Kenya ilipangwa kwa umakini ili kuepuka matukio yoyote ambayo yangeleta aibu, hasa katika maeneobunge yaliyo na upinzani mkubwa dhidi yake.
Rais aliepuka baadhi ya maeneobunge hasa Nyeri, Murang’a, Laikipia na Embu, ambapo aliogopa kukumbana na upinzani kutoka kwa wakazi na viongozi wenye ushawishi, kama vile aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua.
Ziara hii ilijiri wakati ambao Gachagua amepata umaarufu katika eneo hilo, na Rais Ruto alilazimika kupanga mikakati ya kuhakikisha alikaribishwa kwa shangwe, huku akiepuka maeneo ambayo angepata upinzani.
Moja ya maeneobunge aliyohepa ni Mathira, Kaunti ya Nyeri, ambako wakazi walimchagua kwa wingi wa kura katika uchaguzi wa 2022, lakini aliepuka kutembelea kwa sababu ya uhasama kati yake na Gachagua.Bw Gachagua aliongoza kampeni za Rais katika uchaguzi mkuu wa 2022 ambapo alizoa kura 63,715 kutoka Mathira.
Hata hivyo, Rais aliepuka kutembelea Mathira licha ya kuwa ni eneo lililompigia kura kwa wingi, kwa kuepuka uhasama na maoni hasi kutoka kwa wafuasi wa Gachagua.
Mbunge wa sasa wa Mathira, Eric Wamumbi, alikuwemo katika msafara wa Rais lakini hakuruhusiwa kuzungumza mbele ya umati katika miji ya Nyeri na Othaya, kuzuia aibu iliyoshuhudiwa Kiongozi wa Wengi, Kimani Ichung’wah, alipokejeliwa na wakazi Ol Kalou, Kaunti ya Nyandarua, mbele ya Rais.
“Katika hali kama hiyo, aliona ni bora kumzuia Wamumbi kuzungumza ili kuepuka hali ya aibu,” alisema mmoja wa washirika wa Rais.Rais aliepuka pia baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo haikuwa imepata fedha, kama vile eneo la Viwanda, Kaunti ya Laikipia, ili kuepuka aibu ikiwa miradi hiyo ingeonekana kuwa imetelekezwa na serikali.
Akiwa Nanyuki, Rais alizuru maeneo matatu pekee: Shule ya Msingi ya Nanyuki DEB kuzindua ujenzi wa madarasa, kukagua soko la Nanyuki lililo karibu mita 100 kutoka hapo, kisha kuelekea katika mradi wa Nyumba za Bei Nafuu kwa chini ya dakika tano.
Awali, kulikuwa na mipango ya Rais kutembelea Likii Estate, eneo la mabanda, kutoa hatimiliki za ardhi na kuzindua ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi ya Thingithu.
Hata hivyo, mpango huo ulifutwa kwa sababu barabara ya kuelekea maeneo hayo ingempitisha karibu na kituo kikuu cha magari mjini Nanyuki – eneo lenye msongamano mkubwa na lisilotabirika.
Badala yake, wapangaji wa ziara walichagua maeneo yaliyodhibitiwa ambapo watu waliokuwa wamepangwa pekee waliruhusiwa kuingia, huku ‘wapinzani’ na ‘wahalifu’ wakitambuliwa kwa urahisi.
Jaribio la watu wachache kupiga kelele wakisema “uongo” wakati Rais alipohutubia mkutano nje ya Soko la Nanyuki halikufua dafu, sauti zao zilizimwa na shangwe kubwa kutoka kwa vijana waliokuwa wamepangwa.
Rais Ruto pia aliepuka maeneobunge ya Gichugu na Kirinyaga ya Kati, ngome za kisiasa za kiongozi wa People’s Liberation Party, Martha Karua. Wakazi walisema Rais aliepuka maeneo hayo kwa kuhofia kuzomwa kufuatia kuondolewa kwa aliyekuwa Naibu Rais, Bw Gachagua.
“Watu wa maeneo haya hawakuwa tayari kumpokea Rais kwa sababu aliruhusu mwana wetu Gachagua kuondolewa. Rais alijua wenyeji ni wakali na alihofia kuaibishwa,” alisema mkazi mmoja, Bw Njiru Njuki.
Wakazi pia walieleza kuwa miradi mingi ya maendeleo katika maeneo hayo ilikuwa imetelekezwa, na Rais aliepuka kujibu maswali magumu kuhusu hali hiyo.Hali kama hiyo ilijirudia Embu, ambako Rais alikwepa kutembelea eneobunge la Manyatta, ngome ya mkosoaji wake Gitonga Mukunji. Badala yake, alitua tu mjini Embu, ambako alikumbana na mapokezi baridi.
Profesa Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multimedia amesema kuwa ziara hiyo, ambayo ilitegemea umati uliopangwa badala ya uungwaji mkono wa asili, ni ishara kuwa Rais Ruto amepoteza ushawishi mkubwa katika eneo hilo.
“Ruto hakuongea na wananchi katika maeneo ya wazi kama zamani wakati wa kampeni. Hii inapaswa kuwa funzo kwake – zamani hakuhitaji kupanga watu, alipojitokeza tu walijitokeza kwa wingi. Sasa mambo yamebadilika,” alisema Prof Naituli.