Ruto alivyoibuka mfalme wa abautani, leo hiki kesho kile
RAIS William Ruto amejitokeza kama bingwa wa kwenda kinyume na kauli alizotoa kuelekea uchaguzi mkuu uliopita na hata miaka miwili baada ya kuingia afisini, hali inayomfanya kuonekana kama kiongozi asiye na msimamo thabiti.
Dkt Ruto amejikanganya kuhusiana na sera anazotoa akiwa mamlakani, wakati mwingine akifanya hivyo miezi miwili baada ya kuzitoa, na hivyo msimamo wake kutiliwa shaka.
Kufikia sasa Rais amejikanganya kuhusu shughuli za Wakfu wa Ford nchini, kudhulumiwa kisiasa kwa naibu wake Rigathi Gachagua, madai ya kutekewa nyara kwa wakosoaji wa serikali yake ya Kenya Kwanza, ukiukaji wa maagizo ya mahakama, kuwaingiza serikalini viongozi wa upinzani miongoni mwa mambo mengine aliyoapa kutoruhusu kufanyika wakati wa utawala wake.
Wakati huu Bw Gachagua anakabiliwa na vitisho vya kung’olewa mamlakani kupitia hoja inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni na wandani wa Dkt Ruto.
Naibu Rais pia amelalamika kuwa anahujumiwa kimakusudi na maafisa wa ngazi za chini serikalini. Aidha, Bw Gachagua amedai asasi za usalama zinatumika kumtisha pamoja na wandani wake.
“Matumizi ya maafisa wa asasi za usalama kama silaha katika vita vya kisiasa ni mbinu iliyopitwa na wakati. Rais Ruto na mimi, baada ya kuingia afisini, tuliwaahidi Wakenya kwamba maafisa wa usalama hawatatumiwa katika vita vya kisiasa. Naaibika kuwa tumerejelea tulipokuwa zamani,” Bw Gachagua akasema Alhamisi.
Alidai kuna mipango ya kuwawekelea mashtaka bandia wafanyakazi watatu katika afisi yake na wandani wake, Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya na Benjamin Gathiru (Embakasi ya Kati).
Wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022, Dkt Ruto aliapa kutoruhusu naibu wake kupitia mateso aliyopita baada ya kutofautiana na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
“Sitaruhusu Naibu Rais chini ya utawala wangu kuteswa namna makamu wa raia wa zamani waliteswa na jinsi nimekuwa nikidhulumiwa na kukosewa heshima,” akasema.
Kwenye mahojiano mengine katika runinga ya NTV, Dkt Ruto alisema hivi: “Nataka kukuambia kwamba haitatendeka. Nataka nikwambie kuwa sitaruhusu naibu wangu adhulumiwe na wafanyakazi wa vyeo vya chini”.
Vile vile, wiki hii akiwa jijini New York Amerika Rais Ruto alimiminia sifa Wakfu wa Ford kwa mchango wake katika ukuzaji demokrasia nchini Kenya kupitia ufadhili wake.
Lakini miezi miwili iliyopita alisuta wakfu huo kwa kufadhili maandamano ya vijana wa Gen Z yaliyomlazimu kuondoa Mswada wa Fedha na kisha kuwafuta mawaziri wake 21.
“Kenya inathamini zaidi kujitolea kwa Wakfu wa Ford katika kukuza demokrasia yetu na kuunga mkono harakati za Kenya za kutaka mageuzi katika asasi za kiuchumi ulimwenguni, mikakati ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na teknolojia ya kisasa. Nilifanya mazungumzo na Rais wa Wakfu wa Ford Darren Walker jijini New York,” Dkt Ruto akasema Jumanne kupitia ukurasa wake wa mtandano wa X.
Lakini mnamo Julai mwaka huu, Dkt Ruto alidai wakfu huo ulihusika katika visa vya kusababisha machafuko na kuvuruga mafanikio ambayo Kenya imefikia katika mawanda ya kidemokrasia.
“Tunataka Wakfu wa Ford uelezee Wakenya mchango wake katika maandamano ya juzi. Tutawashutumu wale wote wanaolenga kuhujumu demokrasia yetu tuliopata baada ya mapambano makali,” Rais Ruto akasema kwenye mkutano wa hadhara katika eneo la Keringet, kaunti ya Nakuru.
Baadaye Katibu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni Korir Sing’oei aliandikia wakfu huo akiutaka kuelekeza jinsi misaada yake kwa mashirika mbalimbali ya kijamii nchini inavyotumika.
Dkt Sing’oei alidai kuwa mashirika ambayo hupokea ufadhili kutoka kwa wakfu huo ndiyo yalipanga maandamano ya kupinga serikali na kuiondoa mamlakani.
“Mazoea ya Dkt Ruto ya kubadili misimamo yanamsawiri kama kiongozi asiyetabirika, zilivyo sera za serikali,” anasema Profesa David Monda, mhadhiri na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.
Baada ya kuwafuta kazi mawaziri wake 21 Julai 8, mwaka huu Rais Ruto aliamua kuteua viongozi wakuu watano wa ODM katika baraza jipya alilobuni.
Wao ni; Mr Opiyo Wandayi (Waziri wa Kawi na Mafuta), John Mbadi (Fedha), Hassan Joho (Uchimbaji Madini na Uchumi wa Majini), Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika) na Beatrice Askul (Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki).
Lakini Dkt Ruto alitetea hatua hiyo, akifahamu kuwa ni kinyume cha ahadi yake kabla ya uchaguzi wa 2022, akisema ililenga kupalalia umoja nchini na kufanikisha shughuli za maendeleo.