Ruto arejea kwa mama mboga na bodaboda kujaribu kuwavutia tena kama 2022
RAIS William Ruto sasa anaonekana kurejelea mtindo wake wa 2022 akionekana kulenga mahasla ili kuimarisha nafasi yake ya kusalia mamlakani mnamo 2027.
Kiongozi wa nchi anaonekana kuzinduka baada ya Wakenya wa mapato ya chini kulalamikia sera hasi za utawala wake ambazo walidai zinawakandamiza kiuchumi.
Kando na michango ya kupiga jeki makundi ya Mama mboga na wahudumu wa bodaboda, Rais Ruto pia amekuwa akiendeleza mikutano katika ikulu ya Nairobi ambapo viongozi wa nyanjani kutoka kaunti mbalimbali huhudhuria.
Aidha maafisa wa serikali sasa wamejukumiwa kuhakikisha kuwa miradi mbalimbali mashinani inaharakishwa kama ile ya usambazaji na kuunganishwa kwa umeme kwenye maboma mbalimbali na mipango ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.
Mnamo 2022, Rais alipata mamlaka baada ya kujisawiri kama kiongozi wa Wakenya wenye mapato madogo na wafanyabiashara ambao hawana hawanani.
Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki amekuwa sura ya mikutano ya kuinua makundi ya akina mama na tayari ametembelea maeneobunge 180.
Kambi ya Profesa Kithure Kindiki inapanga kuhakikisha kuwa wametembelea maeneobunge yote 290 kufikia Mei mwaka ujao.
Profesa Kindiki huwa anaandaa mikutano kwenye makazi yake ya Karen na Tharaka-Nithi na pia hutembelea maeneobunge mawili kila siku kuwachangishia akina mama na vijana.
Rais naye amekuwa akiendeleza mikutano sambamba ambapo amekuwa mwenyeji wa wahudumu wa bodaboda, viongozi wa mashinani na makundi ya vijana wa Gen Z ikulu ya Nairobi.
Mnamo Jumatano wiki jana, Rais alikutana na zaidi ya wakazi 6,000 kutoka Kiambu ambapo aliwaahidi miradi ya Sh30 bilioni pamoja na masoko mapya 30.
Ijumaa aliandaa mkutano sawa na huo na viongozi wa Kaunti ya Meru ikuluni. Mapema mwezi huu aliwapa vijana pikipiki za umeme na vifaa vingine vya kufanyia biashara kwa vijana wa Nairobi.
“Hii nchi si ya matajiri pekee bali pia ni ya watu wa matabaka ya chini, katikati na wale wa juu. Wakenya wa matabaka yote huwa wanahusika na ustawi wa kiuchumi wa nchi,” akasema Rais Ruto.
Mnamo Agosti 9, Rais Ruto alikuwa mwenyeji wa vijana 1115 kutoka maeneobunge 17 ya Kaunti ya Nairobi.
Profesa David Monda ambaye ni mhadhiri na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa anasema baada ya kupoteza uungwaji mkono wa Mlima Kenya, Rais Ruto ana kibarua cha kupata kura nyingi jinsi alivyopata 2022.
“Ana Nyanza ambayo eneo la Gusii limeenda na Fred Matiangí na Magharibi ana uungwaji mkono vuguvugu. Pia Pwani hajakuwa akishabikiwa sana kwa hivyo Rais anakibarua kikubwa sana kinachomkabili 2027,” akasema Profesa Monda.
Mchanganuzi huyo alidai mikutano ya michango ambapo Rais na Profesa Kindiki wanashiriki unatoa tu mwanya wa kuporwa kwa pesa za umma na ushuru wa raia.
Naye Naibu Gavana wa Machakos Francis Mwangangi anasema kuwa michango hiyo ni mbinu ya zamani iliyotumika na KANU kusaka uungwaji mkono.
“Wanataka kuhakikisha kuwa umaskini unaendelea ndipo wanunue watu wawapigie kura. Watu wamewagundua na hata wanajua kuwa pesa zinazotolewa ni zile ambazo zimeibwa,” akasema Bw Mwangangi.
Kiongozi huyo alisema utawala wa sasa umelemewa kutimiza ahadi ilizotoa kwa Wakenya na unashiriki maovu kama kuwatoza Wakenya ushuru wa juu, utekaji nyara na Wakenya waliopunguziwa mshahara.
“Kwao ni sawa kutumia mabilioni ya pesa kwa michango lakini watatize ugatuzi ambao unaeneza maendeleo hadi kijijini,” akaongeza.
Ingawa hivyo, Profesa Kindiki amesisitiza kuwa michango inayoendelezwa ni ya kuwasaidia Wakenya ambao hawajiwezi.