Jamvi La Siasa

Sababu za Uhuru kupangua upya uongozi wa Jubilee

Na BENSON MATHEKA January 25th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

HATUA ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kupangua na kupanga upya uongozi wa chama cha Jubilee imezua mjadala mpana wa kisiasa, huku wachanganuzi wakitafsiri mabadiliko hayo kama ishara ya mkakati wa kina baada ya kudhoofika vibaya tangu Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Wanasema kuwa Uhuru anaandaa chama kwa mabadiliko akilenga kujiondoa na kumkabidhi hatamu aliyekuwa waziri Dkt Fred Matiang’i.

Kupitia kikao cha Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) kilichoongozwa na Uhuru mwenyewe, Jubilee ilifanya mageuzi makubwa yaliyoondoa Jeremiah Kioni katika wadhifa wa Katibu Mkuu, na badala yake kumpa wadhifa mpya wa Naibu Kiongozi wa Chama anayesimamia operesheni.

Nafasi ya Katibu Mkuu ilichukuliwa na Richard Moitalel Ole Kenta.

Kwa mujibu wa wachanganuzi, hatua hiyo inaonyesha dhamira ya Uhuru ya kuvunja mtindo wa zamani wa uongozi, kurejesha nidhamu, na kujenga upya chama kwa misingi ya ufanisi, si majina au historia ya kisiasa.

Mchanganuzi wa siasa Musa Kauti anasema Uhuru amechukua uamuzi huo kwa sababu Jubilee ilikuwa imebaki kama kivuli cha chama kilichowahi kutawala.

“Uhuru anaelewa kuwa bila kuvunja mfumo wa zamani, Jubilee haiwezi kufufuka na kushindana katika siasa za sasa. Anajiandaa kuondoka na lazima apange chama upya hasa baada ya mizozo iliyotishia kukigawanya baadhi ya watu wakilenga kumpokonya uongozi,” anasema.

Kwa mtazamo wake, nafasi ya Naibu Kiongozi wa Operesheni si njia ya kumdhibiti Kioni kisiasa mbali na kumuandaa kwa wadhifa mkubwa baada yake (Uhuru kujiondoa uongozini).

Mchanganuzi mwingine, David Wafula, anaona mabadiliko hayo kama juhudi za Uhuru kuandaa chama kwa uchaguzi wa 2027 kwa mtazamo wa ushindani wa kweli, hasa baada ya kushuhudia jinsi UDA ilivyofanikiwa kupitia nidhamu na muundo imara.

“Jubilee inataka mpangilio. Uhuru sasa anataka kushamiri, si maneno baada ya kurejeshewa chama na mahakama. Ndio maana Kioni, aliyetekeleza jukumu muhimu kuokoa chama, ameteuliwa kwenye operesheni na Kenta, ambaye ana uzoefu wa kisheria na kiutawala, kuwa msemaji wa chama,” anasema.

Kenta pia anatoka nje ya Mlima Kenya, ngome ya Uhuru na kwa hivyo kuna haja ya kupatia chama sura ya kitaifa kilichokuwa nayo kilipokuwa mamlakani.

Wafula anaongeza kuwa uteuzi wa Moitalel Ole Kenta ni ujumbe kwamba Jubilee ni chama cha kitaifa, si cha kikabila.

Hili, kwa mujibu wake, ni jaribio la Uhuru kupanua mvuto wa chama nje ya ngome yake ya jadi ya Mlima Kenya.

Hatua hii ilifuatia ya kumfanya Dkt Fred Matiang’i kuwa naibu kiongozi wa chama huku akiwa mgombeaji wake wa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao.

“Hatua inayofuata, ni Uhuru kujiondoa na kumkabidhi Matiang’i uongozi kamili wa chama huku Kioni akiwa naibu wake. Uhuru atabaki kuwa mlezi wa chama kimya kimya kwa kuwa hangetaka kuhusika moja kwa moja na siasa za uchaguzi,” alisema Wafula.

Kwa upande wake, mchanganuzi wa masuala ya uongozi Dkt Simon Musau anasema kupanguliwa kwa uongozi wa Jubilee kunatokana pia na hofu ya Uhuru kwamba chama kinaweza kufa kisiasa ikiwa hakitapangwa upya mapema.

Musau anasema uteuzi wa viongozi kama Zack Kinuthia, Yassin Noor Haji na Vincent Mogaka Kimoki kama juhudi za kuingiza damu mpya chamani.

Kwa mujibu wa Jubilee, mageuzi hayo pia yamelenga kurejesha nidhamu ya ndani, kwani chama kimekuwa kikikumbwa na migawanyiko, migogoro ya uongozi na baadhi ya wanachama kujiunga au kushirikiana kwa karibu na serikali tawala.

Wachanganuzi wanasema Uhuru anataka kuondoa suitafahamu mapema na kuanza maandalizi ya uchaguzi huku akiwapa wanachama mwelekeo mmoja.

Kulingana na Musa, Uhuru hakupangua uongozi wa Jubilee kwa bahati mbaya.

“Ni mkakati wa makusudi wa kukijenga upya kitaasisi, na kukiandaa kwa ushindani mkali wa 2027. Ikiwa mkakati huo utafanikiwa au la, itategemea kama viongozi wapya wataweza kuunganisha wanachama, kuvutia wapigakura wapya na kutoa ajenda mbadala inayogusa maisha ya Wakenya wa kawaida,” akasema.