‘Saidia priss’: Gachagua sasa ageukia Jaji Mkuu Martha Koome amuokoe
NAIBU Rais Rigathi Gachagua sasa anamlilia Jaji Mkuu Martha Koome ateue jopo la majaji zaidi ya watatu kuamua kesi aliyowasilisha kupinga mchakato wa kumtimua mamlakani.
Katika ombi alilowasilisha katika Mahakama Kuu, Bw Gachagua ameomba kesi anayopinga kutimuliwa mamlakani na Bunge la Kitaifa ipelekwe kwa Jaji Koome kuteua jopo la majaji watatu au zaidi kuamua uhalali wa bunge kumwondoa enzini.
Jumla ya kesi 22 zimewasilishwa kortini kuhusu kutimiliwa kazini sio tu kwa Bw Gachagua bali pia kwa Rais William Ruto.
Bw Gachagua amekosoa utaratibu uliofuatwa na bunge kumtimua mamlakani akidai umepotoka na kwamba sheria haikuzingatiwa kwa vile alitakiwa kupewa siku 12 kuandaa tetezi zake.
Kupitia kwa wakili mwenye tajriba ya juu Paul Muite, Bw Gachagua amekosoa utaratibu wa bunge wa kutompa muda wa kutosha kuandaa ushahidi wake na kuuwasilisha akijibu madai 11 aliyoshtakiwa.
Bw Muite alisema kupitishwa kwa hoja na Bunge Jumanne ilikuwa tukio la kihistoria.
Aliomba kesi hiyo ipelekwe kwa Jaji Koome ateue jopo ili ushahidi uwasilishwe ndipo mwongozo bora ufikiwe wa kumtimua mamlakani Naibu Rais uwekwe.
Bw Muite alisema wadhifa wa Naibu Rais sio kama ule wa Gavana na kwamba sheria inapasa kufuatwa hoja ya kumfukuza mamlakani inapowasilishwa.
“Naomba hii mahakama ipeleke kesi ya Bw Gachagua kwa Jaji Mkuu Martha Koome ateue jopo la majaji ama watatu, watano au hata saba kuamua masuala mazito ya kikatiba kuhusu kutimuliwa mamlakani kwa Naibu Rais,” Bw Muite alisema.
Wakili huyo alisema utaratibu wa kumtimua uongozini Naibu Rais wapasa kufanywa kwa makini na wala sio njia ya kiholela ambayo itaumiza watakaohudumu katika wadhifa huo siku za usoni.
Aliteta kwamba wananchi walipewa muda mchache kutoa maoni yao kuhusu suala la kumtoa mamlakani Naibu Rais.
“Sheria zinataka mhasiriwa apewe siku 12 kuandaa tetezi na ushahidi kujibu madai anayowekewa,” Bw Muite alimweleza Jaji Lawrence Mugambi.
Jaji Mugambi aliombwa aamuru kesi hiyo ipelekwe kwa Jaji Mkuu Koome ndipo Bw Gachagua ajaribu kunusuru kazi yake.
Lakini Mabunge ya Kitaifa na Seneti yamepinga ombi hilo yakisema “mchakato wa kumtimua Bw Gachagua uongozini haujakamilishwa bado na ikiwa mlalamishi yuko na ushahidi zaidi atapewa fursa kujieleza mbele ya Seneti.”
Mawakili Ben Millimo, Peter Wanyama, Paul Nyamondi, Ann Opola, Mercy Thanji na Eric Gumbo walimweleza Jaji Lawrence Mugambi kwamba mambo bado kwa vile “bunge la Seneti halijatoa uamuzi wake kuhusu kung’atuliwa mamlakani kwa Bw Gachagua.”
Mabw Millimo na Wanyama walimweleza Jaji Mugambi kwamba suala la kumwondoa mamlakani Bw Gachagua bado lasubiri kupigwa msasa na bunge la Seneti kabla ya uamuzi wa mwisho kutolewa.
Mawakili hao walisema suala la kushirikishwa kwa umma sio jambo la kusikilizwa na majaji watatu au zaidi.
“Suala la kushirikishwa kwa umma lapasa kuamuliwa na jaji mmoja tu,” akasema Bw Millimo.
Wakili huyo anayemwakilisha Spika wa Bunge Moses Wetang’ula alisema Bw Gachagua alipewa muda wa kutosha kujitetea.
“Gachagua alikuwa na muda wa kutosha kujitetea. Kama hakuutumia vyema sasa hapasi kulaumu mtu mwingine,” Bw Millimo alisema akiongeza, “Mahakama kuu haina mamlaka kuamua kesi hiyo kwa vile uamuzi wa Bunge la Seneti bado halijatoa uamuzi wake kuhusu kuachishwa kazi kwa Bw Gachagua”
Bw Milimo alimweleza Jaji Mugambi kwamba Bunge lilijadili na kupitisha hoja ya kumtimua kazini Bw Gachagua kwa madai ya ufisadi, utovu wa nidhamu, kueneza ukabila na kudhulumu baadhi ya maafisa wa serikali miongoni mwa madai mengine.
Katika kesi aliyoshtaki Bw Gachagua amesema uamuzi wa kumtimua kazini unakinzana na haki ya watu zaidi ya 7 milioni waliomchagua Rais Ruto pamoja na yeye wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.
Bw Gachagua amesema bunge lilipotoka kufikia uamuzi limng’atue mamlakani likitumia sheria kwa njia isiyofaa.
Amesema sheria na utaratibu wa bunge vyapasa kufuatwa ili haki itendeke.
Jaji Mugambi atatoa uamuzi Ijumaa (Oktoba 11, 2024) ikiwa kesi hiyo itapelekwa kwa Jaji Mkuu kuteua jopo la majaji watatu au zaidi kusikiza malilio ya Bw Gachagua.