Jamvi La Siasa

Shoka linanolewa ili kutema wandani wa Gachagua bungeni?

Na CHARLES WASONGA October 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SIKU chache baada ya wafanyakazi 108 katika afisi ya Naibu Rais aliyeondolea mamlakani Rigathi Gachagua kuagizwa kwenda likizo ya lazima, inasemekana shoka litawageukia wandani wake katika Bunge la Kitaifa na Seneti hivi karibuni.

Mbunge mmoja, ambaye ni mwandani wa Rais William Ruto, anasema mabadiliko yatakayofanywa katika uongozi na uanachama wa kamati za Bunge la Kitaifa na Seneti, wandani wa Bw Gachagua wataathiriwa pakubwa.

“Bila shaka washirika wake katika mabunge haya mawili watapigwa kumbo walivyofanyiwa wafanyakazi waliopelekwa likizo ya lazima juzi. Hatuwezi kuendelea kushirikiana na watu wanaovuta upande tofauti,” anasema Mbunge huyo kutoka Rift Valley, aliyeomba tulibane jina lake.

Mnamo Jumatano Seneta wa Kiambu Karungo Wa Thang’wah alikiri kuhusu uwepo wa kile alichotaja kama “uvumi kwamba viongozi waliopinga hoja ya kumwondoa afisini Gachagwa watatimuliwa kutoka kamati mbalimbali”.

“Ikiwa wanataka kuniondoa kwa kusimama na haki na ukweli, niko tayari,” akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge.

Bw Thang’wah, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Uchukuzi, ni miongoni mwa maseneta wa mrengo wa Kenya Kwanza waliopinga hoja hiyo iliyodhaminiwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.

Wengine walikuwa; Seneta wa Nyandarua John Methu, Seki Lenku Ole Kanar (Kajiado), James Murango (Kirinyaga) na Joe Nyutu (Murang’a).

Seneta Murango, anayehudumu muhula wa kwanza katika Seneti, pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo ilhali Seki anaongoza Kamati ya Seneti kuhusu Biashara.

Seneta Methu ni mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Ardhi ilhali Bw Nyutu anaongoza Kamati ya Seneti kuhusu Elimu.

Isitoshe, maseneta wa chama cha Wiper Enoch Wambua (Kitui), Kavindu Muthama (Machakos), Daniel Maanzo (Kitui) na Shakilla Abdallah (Seneta Maalum)  walipinga hoja kufuatia agizo la kiongozi wa chama hicho, Kalonzo Musyoka.

Katika Bunge la Kitaifa wandani wa Bw Gachagua wanaokabiliwa na hatari ya kuathirika katika mabadiliko hayo ni Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Biashara na Mbunge wa Githunguri Gathoni Wa Muchomba ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Utekelezaji.

Wawili hawa ni miongoni mwa wabunge 44 waliopinga hoja ya kumtimua Gachagua iliyoungwa mkono na jumla ya wabunge 282.

Inasemekana kuwa wiki moja baada sasa, muungano wa Kenya Kwanza utaandaa mkutano wa Kundi la Wabunge na Maseneta wake (PG), mojawapo ya ajenda ikiwa ni mabadiliko katika uongozi na uanachama wa kamati za bunge la kitaifa na seneti.

Kiranja wa wengi katika Seneti Boni Khalwale anasema mkutano huo utafanywa baada ya wabunge kurejea kutoka likizo fupi kuanzia Novemba 5, 2024.

“Bila shaka, kutokana na mabadiliko yaliyofanyika na kilele chake kikawa kutimuliwa kwa Bw Rigathi Gachagua na kuteuliwa kwa Profesa Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais, tutakutana kujadili namna ya kuendesha ajenda ya serikali katika Seneti na Bunge la Kitaifa. Wale ambao wameonyesha wazi kuwa hawako tayari kushirikiana nasi katika mchakato huu bila shaka wataondolewa,” anasema Seneta huyo wa Kakamega.

Wadadisi wanasema kuondolewa kwa kutimuliwa kwa wandani wa Gachagua wanaoshikilia nyadhifa za uongozi wa kamati ya mabunge hayo kutachochea zaidi misukosuko ndani Kenya Kwanza.