Siasa za usaliti zatawala Mlima Kenya
SIASA zinazoshuhudiwa sasa katika eneo la Mlima Kenya zinadhihirisha methali kwamba hakuna rafiki wala adui wa kudumu katika siasa.
Kasi ambayo washirika wa zamani wa kisiasa wanageuka kuwa mahasimu, na wengine wakibadili misimamo yao kwa haraka, imegeuza ulingo wa siasa kuwa kama tamasha la sarakasi.
Bw Rigathi Gachagua alipong’atuliwa na Bunge mwezi Oktoba mwaka jana na kupoteza wadhifa wa Naibu Rais, alianza kuwavuta upande wake baadhi ya washirika wa zamani wa Rais Ruto kutoka eneo hilo. Wakati huo huo, baadhi ya viongozi aliokuwa akitegemea walipokuwa pamoja serikalini sasa wamekuwa wakosoaji wake wakuu. Hata wale waliopinga kutimuliwa kwake awali, sasa wamerejea upande wa Rais.
“Usaliti mkubwa zaidi ulikuwa ule wa Rais Ruto kuidhinisha kuondolewa mamlakani kwa Gachagua. Sikutarajia jambo hilo litokee, na kama lingetokea, nilidhani lingesubiri muhula wa pili,” asema mhadhiri na mchambuzi wa siasa Profesa Macharia Munene.
Profesa huyo anasema, katika hali nyingi za usaliti, ni kama kucheza kamari—matokeo yake yanaweza kuwa ya kushangaza, kama ilivyotokea katika kutimuliwa kwa Gachagua.”
Waziri wa zamani wa Utumishi wa Umma Bw Justin Muturi, ambaye awali aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu kwa kumfanyia kampeni Rais Ruto, sasa amekuwa adui wa serikali hiyo. Alifutwa kazi serikalini baada ya kulalamikia kutekwa kwa mwanawe, akisema wahusika ni maafisa wa usalama wa serikali aliyokuwa akitumikia. Sasa ameungana na Gachagua dhidi ya Rais Ruto.
“Ningependa kumkumbusha Gachagua kuwa aliapa kulinda siri za serikali maisha yake yote, na baadhi ya mambo anayoyasema sasa ni usaliti wa taifa,” alisema Mbunge wa Laikipia Mashariki Bw Mwangi Kiunjuri.
Bw Kiunjuri aliongeza kuwa hali hiyo hiyo inamhusu Bw Muturi, ambaye analalaumiwa kwa kutoa madai yasiyo na ushahidi dhidi ya serikali, rais na maafisa wake.
Hata hivyo, Bw Muturi aliambia Taifa Leo kwamba, “Kiunjuri ni mwalimu na mimi ni mwanasheria,” akidokeza kuwa Kiunjuri hafai kutoa maoni ya kisheria dhidi yake.
“Ninachojua ni kwamba hakuna kiapo cha siri kinachomlazimisha mtu kuficha ufisadi, utekaji nyara, mauaji ya kiholela na watu kupotea kwa kulazimishwa,” alisema.
Mbunge wa Gatanga Bw Edward Muriu, ambaye pia ni mkurugenzi wa masuala ya kisheria katika chama tawala cha UDA, ni mmoja wa washirika wa Gachagua waliotangaza kuzindua chama kipya mwezi Mei ili kuvutia wanachama wa UDA kuhamia upande wake.
“Sina jukumu la kuunga mkono hoja yoyote kwa upofu. Kutimuliwa kwa Gachagua kulikuwa hatua mbaya, sera za serikali hii zinawakera Wakenya, na kuunga mkono hali hii ni kama kusulubisha haki,” alisema Bw Muriu.
Aliongeza kuwa hawezi kuunga mkono mfumo wa ushuru unaowatesa wajasiriamali wa eneo hilo.
Baadhi ya kauli za mafumbo kutoka kwa washirika wa Rais Ruto Mlima Kenya, wakiwemo Mwakilishi wa Wanawake Murang’a Bi Betty Maina na Waziri wa Teknolojia ya Habari B. William Kabogo, zimezua tafsiri tofauti.
Wakizungumza kwa lugha ya Kikuyu katika ziara ya wiki nzima ya Rais Ruto eneo hilo, walidokeza kuwa kwa sasa wako upande wa serikali ili wapate maendeleo, siasa zitasubiri hadi 2027.
Mbunge wa Maragua Bi Mary wa Maua amerejea upande wa Rais Ruto na kusema, “Siwezi kuishi katika hasira ya milele, na hata hivyo si mimi niliyetimuliwa.”
“Mkataba wangu wa utendakazi hauhusu kupigania kutimuliwa kwa viongozi, bali ni kuwawakilisha watu, kutunga sheria na kushawishi maendeleo,” aliongeza.
Alisema kwamba kutimuliwa kwa Gachagua si jambo kubwa.
“Ni kosa la Rais lakini si kosa kubwa la kumfanya apoteze ushawishi Mlima Kenya,” alisisitiza.
Wengine waliokuwa upande wa Gachagua lakini sasa wamejiunga na Rais Ruto ni Mbunge wa Runyenjes Bw Eric Muchangi na Mbunge Mteule Bi Sabina Chege, waliombatana na Rais katika ziara ya Mlima Kenya ambayo washirika wa Gachagua waliikwepa.
Gachagua pia anajihisi kusalitiwa na Mbunge wa Mathira Bw Eric Wamumbi na mkewe, Bi Maina. Hata baada ya Gachagua kuwa kama baba yao wa jadi katika harusi yao, wawili hao waliungana na waliompigia kura ya kutimuliwa.
Mbunge wa Kangema Bw Peter Kihungi pia amedokeza kuacha kupinga serikali.
“Itakuwa vigumu kutekeleza majukumu ya ubunge ukiwa nje ya serikali. Ningependa Rais Ruto amfikie Gachagua na wapatanishwe kwani tuko katika wakati mgumu sana,” alisema Bw Kihungi.
Kisha kuna usaliti kati ya Rais Ruto na Mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro.
Baada ya kushirikiana katika kampeni hadi kupata asilimia 87 ya kura za eneo hilo mwaka 2022, Rais alimwondoa kwenye Kamati ya Bajeti na Matumizi ya Bunge, na nafasi hiyo ikapewa mbunge wa ODM wa Bw Raila Odinga.