Jamvi La Siasa

Sifuna, Babu Owino na Wanyonyi wakwepa ziara ya Rais jijini, je, Sakaja anawafunika?

Na MOSES NYAMORI, KEVIN CHERUIYOT March 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WABUNGE watatu wa ODM katika Kaunti ya Nairobi jana walisusia ziara ya Rais William Ruto jijini, hatua ambayo ilisawiriwa kuwa upinzani kwa muafaka kati yake na Kinara wa upinzani Raila Odinga.

Makubaliano kati ya wanasiasa hao wakuu uliafikiwa na kutiwa saini mnamo Ijumaa wiki iliyopita.

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna ambaye pia ni Katibu Mkuu wa ODM, mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na mwenzake wa Westlands Timothy Wanyonyi hawakuwa kwenye ziara ya Rais katika eneobunge la Kamukunji.

Bw Sifuna amekuwa mkosoaji mkuu wa Rais Ruto huku nao Mabw Owino na Wanyonyi wakiweka wazi nia zao za kuwania ugavana dhidi ya Johnson Sakaja.

Kukosekana kwa Mabw Wanyonyi na Owino kunahusishwa na hatua ya Kinara wa ODM Raila Odinga kudaiwa kumuunga mkono Bw Sakaja ambaye ni mwanachama wa UDA kutetea ugavana katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Muafaka wa kisiasa kati ya Rais Ruto na Raila unaonekana kumnufaisha Bw Sakaja anayetarajiwa kuwania muhula wa pili wa ugavana.

ODM mnamo Jumapili ilikuwa imewaandikia wabunge na viongozi wake wote jijini kuungana na Rais Ruto katika ziara hiyo na wabunge wake wengine jijini walijitokeza.

Bw Sifuna aliambia Taifa Leo kuwa alikuwa na shughuli nyingine kwani alikuwa akihudhuria kikao cha kamati ya seneti. Mabw Owino na Wanyonyi hawakujibu simu na ujumbe ili kueleza kwa nini walisusia ziara hiyo.

Wale ambao pia walikosekana ni wandani wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ambapo kukosekana kwao kunahusishwa na uhasama kati ya kigogo wao wa kisiasa dhidi ya Rais.

Wao ni mbunge wa Embakasi ya Kati Benjamin Gathiru almaarufu MejjaDonk na mwenzake wa Embakasi Kaskazini James Gakuya.

Mbunge wa Embakasi Kusini Musili Mawathe, mwandani wa Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka naye pia hakuwa kwenye ziara hiyo ya rais.

Wabunge wandani wa Raila ambao waliungana na Rais Ruto ni Mbunge Mwakilishi wa Kike Esther Passaris, Beatrice Elachi (Dagoretti Kaskazini ), Phelix Odiwuor Jalang’o (Langata), George Aladwa (Makadara), Anthony Oluoch (Mathare), Peter Orero (Kibra) na Tom Kajwang’ (Ruaraka).

Wengine ambao si wabunge wa ODM ambao walijumuika na Rais ni Mbunge wa Kamukunji Yusuf Hassan (Jubilee), Dagoretti Kusini John Kiarie (UDA) na Mark Mwenje wa Embakasi Magharibi (Jubilee) kisha Mbunge wa Kasarani Ronald Karauri ambaye alichaguliwa kwa tikiti huru.

Wabunge wote wa ODM walitarajiwa kuandamana na Rais Ruto kutokana na muafaka wake na Raila. Awali Rais alikuwa amepanga ziara ya siku tano Nairobi ila aliipunguza hadi siku tatu ambazo ni jana, Alhamisi na Ijumaa.

Nairobi imekuwa ngome ya kisiasa ya Raila kwa miaka mingi ambapo ODM imekuwa ikitawala na hata mnamo 2022, ililemea UDA jijini. ODM ilishinda viti vingi vya ubunge, udiwani, useneta na mbunge mwakilishi wa kike huku Raila akimbwaga Rais Ruto kwenye kura za urais.

Muungano wa ODM na UDA unatarajiwa kutoa mwelekeo wa kisiasa mnamo 2027 hasa kuhusu ugavana kati ya Mabw Sakaja, Owino na Sifuna.

Hapo jana, Rais alitembelea miradi mbalimbali ya serikali kuu na ile ya kaunti eneo la Kamukunji. Aliandamana na Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki, Gavana Sakaja, Waziri wa Mazingira Aden Duale kati ya viongozi wengine wa kisiasa.

Mamia ya wakazi wa Eastleigh walijitokeza kumlaki Rais ambaye alitangaza mpango wa kupanua Taasisi ya Kiufundi na Mafunzo ya Kamukunji ili kuwasitiri wanafunzi wengi.

Pia aliahidi kutenga Sh50 milioni kujenga jengo kubwa katika taasisi hiyo.

“Natenga hela hizi na nataka ujenzi huo uanze mnamo Juni. Vijana wengi wanastahili kujiunga na taasisi hii ili kupata ujuzi ndipo wajitegemee katika kupata ajira au kujiajiri,” akasema Rais Ruto.