Uhuru pia afuata Raila kuingia boksi ya Ruto
RAIS Mstaafu Uhuru Kenyatta jana alisalimu amri na kuonekana kuanza kushabikia utawala wa mrithi wake Rais William Ruto baada ya wawili hao kukutana nyumbani kwake eneobunge la Gatundu Kusini Kaunti ya Kiambu.
Tukio hilo limeibua joto la kisiasa nchini na linajiri baada ya Taifa Leo kuripoti mnamo Novemba 23 kuwa ‘handisheki’ ya wawili hao ilikuwa ikinukia.
“Rais William Ruto amemtembelea Rais wa zamani Uhuru Kenyatta nyumbani kwake Gatundu. Wawili hao walijadili masuala yanayofungamana na hali ilivyo nchini,” ikasema taarifa hiyo fupi kutoka wa afisi ya Bw Kenyatta.
Mkutano huo ulichemsha mitandao ya kijamii kiasi kuwa baadhi ya Wakenya wameanza kufasiri kuwa Bw Kenyatta anawaandaa wandani wake kuteuliwa kwenye baraza la mawaziri.
SOMA PIA: Handisheki ya Uhuru na Ruto yanukia
Hii ilikuwa mara ya pili kwa wawili hao kukutana hata kabla ya mwezi moja kukamilika, ikizingatiwa kwamba walikuwa katika hafla ya pamoja kule Embu mnamo Novemba 16.
Hafla hiyo ya kutawazwa kwa Askofu Peter Kimani pia ilihudhuriwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ambaye amegeuka kuwa hasimu mkubwa wa utawala wa sasa.
Wakati huo Rais Ruto alionekana kunyenyekea na kusema amechapa kazi kutoka mahali ambapo Bw Kenyatta alimwachia. Alitaja sekta ya elimu na ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kama zilizopiga hatua kubwa.
Kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa 2022, wawili hao walikuwa na uhasama mkubwa mno. Mnamo Machi 28, 2023 shamba la Bw Kenyatta eneo la Kamakis Kaunti ya Kiambu lilivamiwa na kondoo na mbuzi wake kuibwa wakati wa maandamano ya Azimio dhidi ya serikali.
Tukio hilo lilihusishwa na matamshi ya baadhi ya viongozi wa Kenya Kwanza waliodai kuwa Bw Kenyatta alikuwa akifadhili maandamano yaliyokuwa yakiongozwa na Kinara wa Upinzani Raila Odinga.
Aidha, afisi ya Bw Kenyatta ililalamika kuwa ilikuwa ikinyimwa mgao wake anaostahili kikatiba na utawala wa sasa mnamo Juni 10, 2024.
Ufichuzi kwamba mpango unasukwa
Hapo jana, mbunge wa Makadara George Aladwa ambaye ni mwandani wa Raila alisema kuwa kuna mpango ambao unasukwa ili wandani wa Bw Kenyatta wateuliwe serikalini.
“Mkutano kati ya wawili hao haufai kuwashangaza Wakenya kwa sababu juhudi za kuhakikisha kuwa Uhuru anamfuata Raila serikalini zimekuwa zikiendelea na zishazaa matunda,” akasema Bw Aladwa.
“Kwa kukubali ushirikiano huu lazima naye watu wake wawe serikalini na kama ODM, tunamkaribisha ndani,” akaongeza.
Kwa sasa wizara za Usalama wa Ndani na pia ile ya Jinsia hazina washikilizi wa kudumu baada ya Profesa Kithure Kindiki kuteuliwa Naibu Rais. Stella Soi aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Jinsia, alianguka mahojiano ya bunge mnamo Agosti 2024.
Aliyekuwa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe ambaye ni mwandani wa Bw Kenyatta ni kati ya wale ambao duru zinaarifu huenda wakafanikiwa kuingizwa serikalini.
SOMA PIA: Huenda Kalonzo akaachwa mataani handisheki ya Ruto na Uhuru ikiiva
Pia duru zinaarifu kuwa baada ya ushirikiano wa Bw Kenyatta na Rais kuanza, misukosuko ambayo imekuwa ikishuhudiwa kuhusu mirengo miwili ya Jubilee huenda ikaisha huku upande unaoegemea kwa rais huyo wa zamani ukiendelea na uongozi wa chama.
Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati, shida ya Bw Kenyatta serikalini ilikuwa Gachagua na kwa kuwa sasa ameondolewa, hana tatizo kuungana na Raila kumpiga jeki Rais Ruto.
“Uhuru hatafuti wadhifa wa kisiasa. Kwa hivyo, hana chochote cha kupoteza na sasa anaangalia tu maslahi ya familia yake hasa kwenye sekta za kibiashara. Huenda bado ana uadui mkubwa na Gachagua na hawezi kushirikiana naye kutokana na tofauti zao,” akasema Bw Andati.
Mchanganuzi huyo aliongeza kuwa mabadiliko yanatarajiwa katika baraza la mawaziri na makatibu lazima yawe na wandani wa Uhuru.
Pia alisema huenda rais anatumia ushirikiano huo mpya kumtenga Gachagua zaidi kwa kuwa bado anamezea mate kura za Mlima Kenya hata ingawa hatazipata zote mnamo 2027.