Uhuru, Rigathi, Kindiki wanavyowania ubabe Mlima Kenya
Katika siasa za Kenya, eneo la Mlima Kenya linabaki kuwa miongoni mwa maeneo yenye ushawishi mkubwa wa kisiasa za kitaifa.
Hili ni eneo lenye idadi kubwa ya wapiga kura, nguvu ya kiuchumi kupitia sekta kama kilimo na biashara, na historia ndefu ya kutoa viongozi wakuu wa kitaifa.
Ndani ya muktadha huu, swali linalozidi kuibuka ni: nani anapaswa kuwa msemaji wa kisiasa wa Mlima Kenya – mtu wa kusema kwa niaba ya watu wa eneo hilo, kuwasilisha maslahi yao, na kuwaunganisha kisiasa kwa wakati huu ambao siasa za uchaguzi wa 2027 zimeanza kuchacha kati ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na mrithi wake Prof Kithure Kindiki.
Wachanganuzi wa siasa wanasema Uhuru Kenyatta ni jina lisiloweza kupuuzwa katika siasa za Mlima Kenya. Akiwa mtoto wa rais wa kwanza wa taifa na mwenye uzoefu wa kuongoza nchi kwa miaka kumi (2013–2022), Uhuru anasalia kuwa na heshima miongoni mwa watu wa Mlima.
Ana mtandao mkubwa wa kisiasa, wafanyabiashara, viongozi wa kidini, na mashirika ya kijamii.Zaidi ya hayo, ana mifuko mizito na yeye ndiye kinara wa chama cha Jubilee, chama ambacho kilitawala kwa miaka kumi na bado kina wanachama waaminifu, hasa katika kaunti kama Nyeri, Kiambu, Meru na Kirinyaga.
Hata hivyo, changamoto kubwa kwa Uhuru ni mabadiliko ya kisiasa tangu aondoke madarakani. Kupinga kwake waziwazi urais wa William Ruto mwaka 2022 kulimgharimu uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa baadhi ya wafuasi wake wa zamani.
Licha ya hayo, umaarufu wake bado ni mkubwa miongoni mwa baadhi ya jamii na wafanyabiashara, hasa kwa sababu ya nafasi yake kama “mtu wa familia ya kifalme”. Wazee wa eneo hilo bado wanamtambua kama msemaji wa jamii.
Rigathi Gachagua amejiweka mstari wa mbele kujijenga kama msemaji wa sasa wa Mlima Kenya, akijitambulisha kama ‘mtoto wa Mau Mau’ anayefahamu shida za watu wa mlimani.
Akiwa Naibu Rais, alikuwa na jukwaa kubwa la kuwasiliana moja kwa moja na watu wake kupitia miradi ya serikali.Gachagua amekuwa mstari wa mbele katika kushinikiza marekebisho ya sekta ya kahawa, chai, maziwa, na kushughulikia malalamiko ya wakulima kuhusu bei duni na dhuluma kutoka kwa walanguzi.
Kutofautiana kwake na Rais William Ruto kulionekana kukuza umaarufu wake katika eneo la Mlima Kenya na kuunda chama cha DCP kulimpatia nguvu zaidi huku akijisawiri kama mtetezi mkuu wa maslahi ya Mlima Kenya.
Msemaji Mpya
Akiwa naibu rais Profesa Kithure Kindiki anapambana kuwa msemaji mpya wa Mlima Kenya wadhifa ambao wachanganuzi wanasema unamteleza ikilinganishwa na Uhuru na Gachagua.
Tofauti na Gachagua na Uhuru, Kindiki hana chama chake binafsi, lakini ana ushawishi mkubwa serikalini kupitia wadhifa wake. Amejitokeza kuendesha hafla mbalimbali za uwezeshaji kijamii, hasa kwa vijana na wanawake, na kutembelea maeneo ya mlimani mara kwa mara katika shughuli zisizo za kisiasa kujipatia umaarufu huku akikosoa Gachagua.
Wachanganuzi wa siasa wanasema changamoto ya Kindiki ni ukosefu wa msingi wa chama au wafuasi wa kisiasa kutoka eneo pana la Mlima Kenya huku akijaribu kujivua nembo ya mradi wa Rais Ruto ambaye umaarufu wake eneo hilo ulishuka alipomtema Gachagua na kukumbatia kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Ili kufikia kiwango cha kuwa msemaji wa Mlima Kenya, atahitaji kujiimarisha zaidi kwenye ngazi za kisiasa, kujinasua kutoka kwa serikali ya sasa au kuwa na chama katika uchaguzi ujao na kujishinda ufuasi wa dhati kutoka Mlima Kenya Magharibi.
Wachanganuzi wa siasa Pius Mwaniki na Joseph Kiilu wanasema akiwa naibu rais, hawezi kubanduka chama cha UDA kinachoongozwa na Rais Ruto na anachoweza kufanya kwa sasa ni kutumia wadhifa wake kujenga umaarufu Mlima Kenya.
Kindiki anatoka kaunti ya Tharaka Nithi iliyo Mlima Kenya Mashariki huku Uhuru na Gachagua wakitoka Mlima Kenya Magharibi ambako kuna idadi kubwa ya wapiga kura.Kwa sasa, Rigathi Gachagua anaonekana kuwa na nguvu zaidi za kisiasa kufuatia ujasiri wake wa kukosoa serikali.
Amekuwa akijitaja kama kiongozi wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya na kumtambua Uhuru kama ‘muthamaki’ wa eneo hilo.
“Lakini wawili hao wana vyama vyao vinavyowania umaarufu eneo la Mlima Kenya na kwa hivyo ni washindani hadi pale watakapoketi pamoja na kukubaliana mwelekeo watakaochukua wa kuwa na msemaji mmoja wa eneo,” asema Dkt Isaac Gichuki, mchanganuzi wa siasa.