Jamvi La Siasa

Unahalalisha ukatili, Imanyara aambia Raila

Na BENSON MATHEKA July 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Wakili wa Nairobi na mpiganiaji wa demokrasia ya vyama vingi Gitobu Imanyara anamemlaumu aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kuwa kuhubiri injili ambayo haitoi suluhu kwa matatizo ya Kenya.

Bw Imanyara, anasema Raila anapaswa kuepushia nchi mihadhara kwa kuitisha kongamano la kitaifa. “Hatuhitaji mazungumzo ili kuelewa kwamba kutumia risasi dhidi ya waandamanaji wasio na silaha ni kosa. Hili si suala la vikao vya kisomi au “mazungumzo ya kitaifa,” bali ni suala la utu wa msingi.

Kuona vijana wakivuja damu barabarani kwa kudai maisha bora ya baadaye hakuhitaji tafsiri ya kisiasa. Kunahitaji uwazi wa maadili na hatua ya haraka. Lakini mara nyingine tena, tunadhihakiwa na kauli zilizochoka za mazungumzo, uponyaji wa kitaifa na msamaha yote bila haki,” Bw Imanyara alisema katika maoni yaliyochapishwa katika Jarida la Weekly Review.

Kulingana na wakili huyo tatizo si ukosefu wa uelewa. “Kila mtu — kuanzia Ikulu hadi vituo vya polisi na Bunge — anajua kuwa kinachoendelea Kenya si sahihi. Mauaji ya kiholela, kutoweka kwa lazima, mateso na kukamatwa kwa halaiki si tu kinyume cha katiba, bali pia ni ukatili uliovuka mipaka,” alisema.

Anaongeza: “ Lakini vinaendelea, si kwa sababu ya ujinga, bali kwa sababu wanaohusika wanajua hawatachukuliwa hatua yoyote. Hakuna kuwajibishwa: hakuna kamanda wa polisi aliyejiuzulu; hakuna afisa aliyefunguliwa mashtaka na hakuna kiongozi wa kisiasa aliyeondoka ofisini kupisha uchunguzi huru. Ukatili wa Serikali sasa umekuwa jambo la kawaida.”

Bw Imanyara anasema polisi hawaui watu bila maagizo.”Tunafaa kuwa wazi: polisi hawafanyi hivi kwa bahati mbaya, wanatekeleza maagizo. Ukatili tunaoshuhudia si ajali. Ni sera. Ni mkakati. Ni matumizi ya nguvu kwa makusudi ili kukandamiza upinzani, kuwatisha wananchi, na kulinda maslahi ya wachache walio na mamlaka,” alisema.

Alilaumu utawala wa Kenya Kwanza kwa kutokubali makossa.

“Utawala wa Rais Ruto umebobea katika kuwapa wengine jukumu la kutumia vurugu za Serikali huku wakikana kuhusika moja kwa moja. Wakati huohuo, damu ya wasio na hatia inaendelea kulowesha barabara,” asema.

“Kile ambacho Raila Odinga na wanasiasa wenzake hawakioni au wanajifanya hawakioni ni kwamba taifa hili lipo kwenye ukingo wa kuporomoka. Vijana wa Kenya hawaandamani tu kwa sababu ya Mswada wa Fedha au gharama kubwa ya maisha — wanaasi dhidi ya mfumo ambao umewapokonya heshima, fursa na sauti. Mfumo unaowatupa wazazi wao kwenye umasikini, marafiki wao kaburini, na ndoto zao uhamishoni,” anaeleza.

Bw Imanyara anasema raia wamekasirishwa na mfumo unaowaambia wavumilie huku mabilioni yakiporwa. Mfumo unaocheka maumivu yao na kuwaita “wahuni” wanapolalamika. Ukipora kila kitu kutoka kwa watu — matumaini yao, haki zao, uhuru.

“ Tunachoshuhudia si maandamano tu; ni ghadhabu za kizazi. Gen Z, ambao mara nyingi hudharauliwa kama wavivu waliokosa msimamo, wamekuwa dhamiri ya taifa. Ujasiri wao umefichua woga wa tabaka la kisiasa. Upinzani wao umefunua ukatili wa Serikali. Na sauti zao — wazi, kali, na zisizotetereka — zinatikisa bara zima,” akasema

Lakini badala ya kusikiliza, Serikali inajibu kwa risasi. Badala ya kuwajibika, tunapewa propaganda. Badala ya mageuzi, tunapata ukandamizaji. Ujumbe uko wazi: huna haki ya kulalamika, huna haki ya kuandamana, huna haki ya kuishi nje ya udhibiti wa Serikali. Hii si demokrasia; huu ni udikteta.

“Na katikati ya yote haya, Raila Odinga — aliyewahi kusimamia haki, aliyewahi kutembea na wanyonge, aliyewahi kufungwa kwa ajili ya uhuru wetu — sasa anatoa wito wa mazungumzo bila uwajibikaji. Tutawezaje kupona bila ukweli? Amani itapatikanaje bila haki? Ni kiongozi wa gani anayetaka watu watulie wakati miili ya vijana iko mochari na akina mama wao wanalia katika vituo vya polisi?” alihoji.

Historia, anasema, haitawasamehe wale wanaochagua kimya mbele ya ukatili wa Serikali, wala haitakuwa na huruma kwa wanaofanya maelewano na wauaji.

“Wale wanaojifanya hawaoni nao ni wahusika wa uovu huo. Kenya ipo njia panda — tunaweza kuendelea na njia ya ukandamizaji, ambapo Serikali hutawala kwa woga na polisi hufunzwa kupiga risasi badala ya kuhudumia raia; au tuchague njia tofauti. Njia ambapo Katiba ni zaidi ya karatasi, ambapo haki haijahifadhiwa kwa matajiri pekee, na ambapo kila raia — bila kujali umri au hadhi — anaheshimiwa kama binadamu.” asema

Lakini ili hayo yatimie, aeleza, ni lazima tuache kuhalalisha ukatili wa Serikali. Lazima tuuite kwa jina lake, tuweke wazi, na tudai haki. “Lazima tuache kujifanya kana kwamba mazungumzo yanaweza kuchukua nafasi ya uwajibikaji. Na zaidi ya yote, lazima tukatae kutishwa,” akasema.