Jamvi La Siasa

Uteuzi wa Kindiki pigo kwa Mulembe katika Kenya Kwanza

Na BENSON MATHEKA November 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KUTEULIWA na kuapishwa kwa Profesa Kithure Kindiki kama naibu rais baada ya kuondolewa kwa Gachagua kumedidimiza matumaini ya kiongozi kutoka Magharibi mwa Kenya kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Haya yanajiri huku minong’ono ikiibuka kuhusu njama za kumvua Bw Moses Wetangula kiti cha Spika wa Bunge la Kitaifa. Bw Wetangula na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ndio viongozi wakuu kitaifa kutoka jamii ya Mulembe kwa wakati huu.

Kabla ya Profesa Kindiki kuteuliwa kurithi Gachagua, Bw Mudavadi alikuwa miongoni mwa waliopigiwa upatu kwa wadhifa huo. Hata hivyo iliibuka kuwa Rais Ruto alinuia kurudishia eneo la Mlima Kenya wadhifa huo na ndio sababu aliamua kumteua Profesa Kindiki.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba kuteuliwa kwa Kindiki na ushirikiano wa kisiasa wa Rais Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga kumezima nafasi ya kigogo kutoka jamii ya Mulembe kuteuliwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto katika uchaguzi wa 2027. “Kinachojitokeza hapa ni kuwa Rais Ruto aliteua Profesa Kindiki kama naibu wake ili kudumisha sehemu ya umaarufu wake eneo la Mlima Kenya ambao utaathiriwa na kumtema Bw Gachagua. Hii ni pigo kwa eneo la Magharibi ambalo lilikuwa likitegea wadhifa huo,” aeleza mchanganuzi wa siasa Daisy Akoth.

Anasema kuwa akiwa na Bw Odinga upande wake, Rais Ruto anaamini eneo la magharibi limeshughulikiwa.

“Kulingana na matokeo ya chaguzi kuu zilizopita ukiwemo wa 2022 ambao Kenya Kwanza ilishinda, Raila ni maarufu eneo la magharibi na miongoni mwa jamii ya Mulembe kuliko Mudavadi na Wetang’ula na akiwa upande wa Ruto, vigogo wa eneo hilo wasahau unaibu rais,” asema Dkt Akoth.

Minong’ono ya kisiasa inasema kwamba huenda Rais Ruto akafanya mabadiliko katika serikali ambapo eneo la Magharibi litapunguziwa ‘hisa’ katika serikali ya Kenya Kwanza ikabidhiwe Nyanza, ngome thabiti zaidi ya Bw Odinga.

Wiki hii habari zilizokanwa na viongozi wa Kenya Kwanza zilidai kuna njama za kumuondoa Wetangula kama spika wadhifa huo uchukuliwe na mbunge mmoja wa ODM.

Ben Kimanthi, mchambuzi wa siasa anasema kuna uwezekano mkubwa wa Rais Ruto kudumisha Profesa Kindiki kama naibu wake katika uchaguzi mkuu wa 2027 ili kuepuka uasi mkubwa wa eneo la Mlima Kenya likiungana lilivyokuwa 2022.

“Hii inamaanisha kuwa kutakuwa na mabadiliko makubwa yatakayoathiri eneo la Magharibi ambalo limekuwa likimezea mate wadhifa wa mgombea mwenza wa Dkt Ruto katika uchaguzi wa 2027 hasa pale alipoanza kutofautiana naibu wake aliyeondolewa mamlakani,” asema Kimanthi.

Anasema kuanzia sasa hali ya siasa nchini itabadilika pakubwa wagombea urais wakiwania maeneo yaliyo na kura nyingi kupata washirika wa kisiasa.

“Kwa sasa nafasi ya eneo la magharibi katika serikali ya Kenya Kwanza ni tete. Nazungumzia vigogo Mudavadi na Wetangula ambao ushawishi wao katika utawala wa Dkt Ruto umepunguzwa na kuingia kwa Bw Odinga ambaye ni maarufu katika ngome yao kuwaliko,” asema.