Jamvi La Siasa

Uvamizi wa shamba la familia ya Kenyatta unavyoendelea kumponza Riggy G

Na CHARLES WASONGA November 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

HUKU kitendawili kuhusu ni nani waliopanga njama ya uvamizi wa shamba la familia ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, kikiwa hakijateguliwa zaidi ya miaka miwili baada ya kisa hicho kutokea, suala hilo la kiusalama sasa limeingizwa siasa.

Wandani wa Rais William Ruto kutoka Mlima Kenya sasa wiki hii wamefunguka huku wakielekezea kidole cha lawama kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Anayeongoza kwaya ya kumponda kiongozi huyo wa chama cha Democracy for the Citizen Party (DCP) sio mwingine ila ni kipaza sauti wa Dkt Ruto ndani ya nje ya bunge, Kimani Ichung’wah.

Kwenye mahojiano katika runinga ya Inooro, inayopeperusha matangazo kwa lugha ya Agikuyu, Mbunge huyo wa Kikuyu alidai Jumatano kuwa Riggy G  ndiye aliamuru kuondolewa kwa polisi katika shamba hilo lililoko Ruiru, Kiambu, kutoa nafasi kwa wahuni kulivamia.

Drama hiyo ilitokea mchana peupe Machi 27, 2023 huku habari na picha za wahuni hao wakiwabeba kondoo zikipeperushwa mbashara kwenye runinga za humu nchini.

Huku wakiwa wamejihami kwa silaha butu, walivamia shamba hilo kwa jina, Northlands Farm, wakakata miti, wakawasha moto na kutoweka mifugo hao.

Iliripotiwa kuwa wahalifu hao waliwauza kondoo hao kwa bei ya kutupa ya kati ya Sh500 na Sh1,000.

“Aliniita katika afisi yake katika jumba la Harambee House Annex, ambako aliyekuwa naibu rais aliagiza Inspekta Jenerali awaondoe maafisa wa polisi kutoka shamba la Kenyatta ili kutoa nafasi kwa wahuni kuingia humo na kupora mali. Wakati huo rais walikuwa nje ya nchi,” Ichung’wah akadai.

Kwingineko, Mbunge wa Gichunguri Gathoni Wamuchomba wiki hii alinukuliwa akisema hivi: “Wale wanaodai kuwa wanaunganisha jamii yetu wanafaa kwanza kuomba msamaha kwa familia ya Kenyatta. Kwanza warudishe kondoo na mbuzi walioibwa.”