Jamvi La Siasa

Vijana wa Gen-Z wageuka ndoto mbaya kwa Rais

Na MOSES NYAMORI July 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto anaonekana kukubali hali ilivyo katika juhudi zake za kufuta hasira ya vijana ambao wamekuwa mwiba kwake wakiandamana, huku makosa zaidi kutoka kwa serikali yake yakiendelea kuchochea ghadhabu ya kizazi cha Gen Z.

Alipokataa Mswada wa Fedha wa 2024 na kuvunja baraza lake la mawaziri mnamo Julai 11, 2024, Rais Ruto alidhani alikuwa amejibu madai ya vijana waliokuwa wakiandamana.

Lakini vijana hao hawajaridhika na jinsi serikali ya Kenya Kwanza inavyoendesha masuala ya taifa, hali inayozidi kuzorota kutokana na mauaji na utekaji unaodaiwa kufanywa na polisi.

Rais Ruto pia amevunja baadhi ya ahadi alizotoa kwa vijana wakati wa maandamano hayo. Ahadi ya kupunguza idadi ya washauri wake haijatimizwa, kwani sasa ameongeza zaidi katika ofisi yake.

Aidha, amekiuka ahadi ya kupiga marufuku harambee, huku yeye na washirika wake wakiongoza kutoa mamilioni ya pesa katika hafla za michango na “mipango ya uwezeshaji” kote nchini.

Washirika wake wa karibu pia wameanza kuonyesha anasa na maisha ya kifahari mbele ya vijana wasiokuwa na ajira, ambao ndio waliomchagua kwa wingi mwaka wa 2022.

“Ruto anakabiliwa na hali ngumu sana. Kuanzisha mazungumzo rasmi na Gen Z kutamaanisha kutambua rasmi harakati zao, na pia ni kukubali wazi kwamba madai yao ni halali na hayajatatuliwa,” asema Prof David Monda, mhadhiri wa chuo kikuu nchini Amerika na mchambuzi wa kisiasa.

“Akikubali kusuluhisha mzozo huu, itabidi aachane na baadhi ya maafisa wake serikalini. Lakini hiyo inaweza kuwapa nguvu zaidi Gen Z kuendelea kudai mabadiliko zaidi. Lakini mwisho wa yote, lawama kuu ziko Ikulu. Na Ruto hataki kujiuzulu. Kwa hivyo nadhani njia yake itakuwa kutumia nguvu badala ya maridhiano,” aongeza Prof Monda.

Mnamo Juni 25, 2025, vijana waliandamana tena kwa wingi kuadhimisha kumbukumbu ya kuvamia Bunge mwaka jana, wakikumbusha kuwa matatizo waliyotaja bado hayajatatuliwa.

Walitaka Rais ajiuzulu, wakitaja visa vya mauaji ya wakosoaji wa serikali na visa vya utekaji kama msingi. Seneta wa Kitui, Enoch Wambua, asema kukabiliana na Gen Z “kunahitaji zaidi ya maneno matamu ya kisiasa.”

Kwa Gen Z, anasema, hakuna kujificha nyuma ya siasa au kauli za kujipendekeza.

“Namuona Rais Ruto kama kiongozi anayetaka kuwa upande wote kwa wakati mmoja: anataka kuwadumisha wafuasi wake hata kama wananchi wanataka waondoke; anataka kuwa na washauri wa kila sekta licha ya kuahidi kuwapunguza kwa nusu; anadanganya makanisa, wanawake na makundi ya vijana kwa hela nyingi licha ya kuahidi kufutilia mbali harambee,” asema Seneta Wambua.

Ijumaa iliyopita, Rais Ruto alionekana kuishiwa na mbinu za kushughulikia vijana wanaojitokeza si tu kama kundi la wapiga kura, bali kama vuguvugu la kijamii na kisiasa. Aliwaambia kwamba ataondoka tu kupitia njia ya kikatiba na kidemokrasia.

“Kama ni Ruto lazima aondoke, niambie mnataka niondoke vipi. Tuwe wa kweli. Kwa sababu tuna katiba, sivyo? Kama mnataka Ruto aondoke, ushauri wangu ni mmoja – tafuteni mpango bora. Washawishini Wakenya kuwa mna mpango bora kuliko wangu,” alisema Rais Ruto siku mbili baada ya maandamano ya Juni 25.

Kauli hiyo ilionekana kulenga viongozi wa upinzani ambao wamejiunga na vijana kudai kuondoka kwake madarakani.

Kabla ya kuvunja baraza lake la mawaziri, Rais alikuwa ametangaza kongamano la siku sita la wadau wa sekta mbalimbali, ambalo baadaye lilifutiliwa mbali baada ya vijana kulikataa.

Katika kongamano hilo, Rais alipendekeza kuundwa kwa Jukwaa la Kitaifa la Wadau 100 (NMSF) kushughulikia malalamishi waandamanaji.

Jukwaa hilo lingefanya kazi katika kaunti zote 47 kuanzia ngazi ya wadi.Rais Ruto pia alijaribu kuzungumza na vijana kupitia X Space mnamo Julai 5, 2024. Mazungumzo hayo yaligeuka kuwa makali huku vijana wakimweleza bayana madai yao.

“Hatuhitaji tena mazungumzo. Tuna takwa moja tu; Ruto lazima aondoke na serikali yote lazima iondoke. Tunahitaji kubadilisha mfumo mzima. Alikuja X Space lakini bado alitudanganya. Alituambia atapunguza washauri hadi saba, leo wako 21,” alisema Mavin Mabonga, kijana na mwanaharakati wa mitandaoni.

Mwanaharakati Boniface Mwangi aliambia Taifa Jumapili kwamba, vijana wanasubiri wakati ufaao kuwaadhibu viongozi wa kisiasa.

Kwa kuwa uchaguzi uko miaka miwili tu mbele, serikali ya Kenya Kwanza imetangaza mipango ya kuwavutia vijana.

Serikali imeungana na Benki ya Dunia kutekeleza mradi wa Sh20 bilioni wa National Youth Opportunity Towards Advancement (NYOTA) kuwapa vijana uwezo wa kiuchumi na kuvutia kura zao mnamo 2027.

Rais Ruto alitangaza kuwa mpango huo utawanufaisha zaidi ya vijana 800,000 wenye umri wa miaka 18 hadi 29, na hadi miaka 35 kwa wale wenye ulemavu, kwa kuwawezesha kupata mafunzo ya kazi na kukuza utamaduni wa kuweka akiba.

Mradi huo unalenga angalau vijana 70 kwa kila wadi nchini, kwa kuwapa ufadhili, mafunzo ya biashara, na fursa za soko. Hata hivyo, vijana wanataja mpango huu hongo na kuapa kuendeleza na shinikizo zao.

Kulingana na sensa ya 2019 zaidi ya asilimia 75 ya Wakenya 47.6 milioni wana umri chini ya miaka 35.

Katika sajili ya wapiga kura ya 2022, kulikuwa na wapiga kura 8,811,691 wa kati ya umri wa miaka 18 na 34 wakiwa asilimia 40 ya wapiga kura wote.

Idadi hiyo itakuwa juu zaidi ifikapo 2027.

Katika uchaguzi uliopita, zaidi ya nusu ya Gen Z walikuwa chini ya umri wa kupiga kura.

Zaidi ya vijana 14 milioni wa Gen Z watahitimu kupiga kura mwaka wa 2027 ikiwa ni ongezeko la asilimia 79.4 ya kundi hilo.

Wakenya wa umri wa miaka 18 hadi 34 watakuwa 17.8 milioni 17.8 na kuwa katika nafasi muhimu ya kuamua mwelekeo wa siasa za Kenya kutoka mwaka 2027.