Jamvi La Siasa

Viongozi chipukizi wa Kenya Moja wavuruga hesabu za Weta, Musalia

Na CECIL ODONGO September 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWAMKO mpya wa viongozi chipukizi unaoendelea kushuhudiwa Magharibi mwa nchi unatishia umaarufu wa Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ambao wamekuwa wakitawala siasa za eneo hilo kwa kipindi kirefu.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, Mbunge wa Saboti Caleb Amisi, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya na Seneta wa Vihiga Geodfrey Osotsi ni kati ya wanasiasa ambao umaarufu wao unaendelea kuongezeka na sasa wanatishia umaarufu wa Bw Mudavadi na Bw Wetangúla.

Hata Kinara wa ODM Raila Odinga ambaye ametawala siasa za Magharibi tangu 2007, kwa sasa anakabiliwa na njiapanda huku baadhi ya viongozi wa Magharibi wakiapa kufurusha ODM kabisa Kaunti ya Kakamega na Magharibi nzima.

Mabw Mudavadi na Wetangúla wamekuwa sura ya siasa za Magharibi hasa baada ya kifo cha aliyekuwa makamu wa rais Kijana Wamalwa mnamo Agosti 2003.

Kando na kuwa kwenye himaya ya Bw Odinga miaka tofauti na kuteka eneo hilo kisiasa, Mabw Mudavadi na Wetangúla walibadili mwelekeo mnamo 2022 na kumuunga mkono Rais William Ruto.

Bw Wetangúla alifanikiwa kuhakikisha Dkt Ruto anatamba dhidi ya Bw Odinga hasa Kaunti ya Bungoma lakini Bw Mudavadi alionekana kulemewa huku Bw Odinga akitawala hata kwenye ngome yake ya Vihiga.

“Viongozi wetu wa sasa wanamakinikia tumbo zao na uongozi wao unawanufaisha tu badala ya wananchi waliowapigia kura. Waluhya ni namba mbili nchini lakini Wetangúla na Mudavadi ndio wamechangia sisi kubaki nyuma. Wakati siasa inapangwa, sisi tuko wapi?

“Wetangúla na Mudavadi saa hii wameajiriwa na Ruto na wanaweza kufutwa kazi na Rais. Raila yuko kwa serikali na anawafaidi watu wake kwa miradi, hawa viongozi wetu wanatupeleka wapi?” akauliza Bw Natembeya akihutubu wiki mbili zilizopita katika hafla moja Kaunti ya Trans Nzoia.

Wafuasi wa Mabw Natembeya na Wetangúla wamekuwa wakitifuana kwenye hafla mbalimbali za matanga hasa Bungoma na Trans Nzoia.

Bw Natembeya mwezi jana alipigwa jeki baada ya Mbunge wa Kabuchai, Bw Majimbo Kalasinga ambaye anawakilisha eneo la nyumbani kwa Bw Wetangúla kujiunga nao.

“Chukueni vitambulisho na mnamo 2027 lazima heshima ya Mluhya irudi. Nguvu yangu ya kungáa kisiasa ni nyinyi,” akaongeza gavana huyo.

Bw Sifuna naye aliteka mji wa Kakamega mnamo Julai 25 wakati ambapo Bw Odinga alihudhuria Kongamano la ODM Kaunti ya Kakamega.

Wakati huo alikuwa anakabiliwa na shinikizo za kuondoka ODM baada ya kupinga ushirikiano wa chama na Kenya Kwanza.

Bw Sifuna alichangamkiwa sana mbele ya Bw Odinga, hotuba yake ikifasiriwa kuwa yupo tayari kupambana kung’oa ufalme wa Magharibi mikononi Mabw Wetangúla na Mudavadi.

“Niko katika ODM na nitaendelea kupigania mageuzi hata kama baadhi ya ndugu zangu ndani ya chama na walioko serikalini hawapendi. Utawala huu haujanufaisha watu wetu licha ya kuwa Mabw Mudavadi na Wetangúla wanashikilia vyeo vya juu serikalini,” akasema Bw Sifuna.

Kwa sasa katibu huyo mkuu anarindima ngoma ya Kenya Moja akiwa na Bw Amisi ambaye ameonekana kuasi ODM na sasa anaungana na vuguvugu la Tawe la Bw Natembeya.

“Miaka na umaarufu wa Mudavadi na Wetangúla unaendelea kudidimia. Wetangúla alikuwa akitaka kuwasilisha mwaniaji Malava na akaacha na hata UDA yenyewe ina kibarua kutwaa kiti hicho. Hiki kizazi kipya cha viongozi kinachoibuka kimewateka wengi na wapo pazuri kuwahi ushindi,” akasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Bw Martin Andati.

Anasema, mizozo ya ndani kwa ndani kuhusu uchaguzi wa matawi ya ODM pia italemeza umaarufu wa Raila na huenda ramani ya siasa za eneo hilo ikabadilika sana 2027.