Wabunge sasa kuenda kwa raia kuokoa CDF
WABUNGE wanajiandaa kukutana ana kwa ana na wananchi baada ya Bunge kuanzisha mchakato wa kushirikisha umma kote nchini kuhusu Mswada wa Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2025, unaolenga kuhalalisha na kukita kwenye Katiba hazina tatu muhimu.
Mswada huu, uliodhaminiwa na Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo pamoja na mwenzake wa Ainabkoi Samuel Chepkonga, unalenga kukita kwenye Katiba: Hazina ya Maendeleo ya Maeneobunge (NG-CDF), Hazina ya Usawa ya Serikali ya Kitaifa (NGAAF), na Hazina ya Usimamizi ya Seneti.
Ushirikishaji wa umma kuhusu mswada huu utafanyika kuanzia Mei 5 hadi Mei 7, 2025 katika maeneobunge yote na kaunti.
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alisema ushirikishaji huo utafanywa kwa kuzingatia Kifungu cha 256 cha Katiba ambacho kinahusisha marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa bunge.
Kifungu hicho kinataka mswada wowote wa marekebisho ya Katiba kuwasilishwa kwa wananchi na kujadiliwa hadharani kabla ya kujadiliwa na mabunge yote mawili.
Karani wa Bunge la Kitaifa, Bw Samuel Njoroge, alisema kutakuwa na fomu za maoni zitakazotolewa kwa wananchi pamoja na nakala za mswada huo kwa Kiswahili na Kiingereza. Maafisa wa bunge watakuwa tayari kusaidia wananchi wasiojua kusoma.
‘Tutahakikisha mchakato huu ni wazi na unazingatia sheria. Baada ya mazoezi haya, tutakusanya maoni yote na kuyatangaza kwa umma,” alisema Bw Njoroge.
Hata hivyo, viongozi wa kisiasa kama Raila Odinga wamepinga NG-CDF, wakidai kuwa ni njia ya wabunge kuingilia majukumu ya serikali za kaunti. Akizungumza wiki jana kwenye mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Kisumu Ken Nyagudi, Bw Odinga alitishia kuwa NG-CDF itakuwa ajenda kuu ya kampeni za 2027 endapo haitabadilishwa.
Lakini wabunge wamekaidi msimamo huo na kuendelea kushinikiza Wizara ya Fedha kuachilia fedha hizo, wakisema wanafunzi maskini wanazitegemea. Aidha, wabunge wanasema bila NG-CDF, wengi wao huenda wakapoteza viti vyao 2027.
Mswada huu pia unakabiliwa na upinzani wa ndani ambapo baadhi ya wabunge wa kike wanataka suala la uwakilishi wa kijinsia kwa mujibu wa ripoti ya NADCO lijumuishwe katika mchakato huu wa kushirikisha umma.
Kwa mujibu wa Katiba, ili mswada huu upitishwe, unahitaji angalau wabunge 233 na maseneta 45 kuupigia kura.
Lakini Bunge lina wasiwasi kuwa Seneti inaweza kuzuia mswada huo kwa sababu ya mvutano wa muda mrefu baina ya mabunge haya mawili. Mbali na hayo, mashirika yasiyo ya kiserikali pia yameelezea nia ya kwenda mahakamani kupinga mchakato huu, kwa msingi kuwa NG-CDF tayari ilitangazwa kuwa batili na mahakama.
Kwa upande wa Hazina ya Usimamizi ya Seneti, wabunge wanasema itasaidia Seneti kutekeleza vyema majukumu yake ya usimamizi kama inavyoelezwa katika Kifungu cha 96 cha Katiba.
Hazina ya NGAAF, kwa mujibu wa mswada huo, itasaidia makundi maalum kama vijana, wanawake, walemavu na wazee kukuza biashara na maendeleo katika maeneo ya kaunti na maeneobunge.
Sheria ya NG-CDF ilitungwa mwaka 2003 na kurekebishwa 2007, ambapo Serikali iliagizwa kutenga angalau asilimia 2.5 ya mapato yaliyokaguliwa kwa matumizi ya maendeleo katika maeneobunge.
Hata hivyo, mwaka 2020 Mahakama Kuu ilitangaza kuwa sheria hiyo haikuwa ya kikatiba, na ikawapa wabunge mwaka mmoja kuirekebisha ili iambatane na Katiba, jambo ambalo sasa limefikia hatua hii ya kushirikisha umma.