Waliogomewa nyadhifa za CAS waomba Rais asiwaache waumie kwa baridi
WATU waliokuwa wameteuliwa Mawaziri Wasaidizi (CASs) sasa wanamtaka Rais William Ruto kutowaacha kwenye baridi kwa kipindi kirefu.
Wakiongea katika hafla moja ya mazishi ya aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Tharaka Nithi Beatrice Nkatha, mawaziri hao wasaidizi wa zamani walijutia kupoteza nafasi hiyo na kuelezea jinsi wamesubiri kwa kupindi kirefu kutunukiwa nyadhifa zingine serikalini.
Marehemu Nkatha alikuwa miongozi mwa mawaziri 50 wasaidizi walioteuliwa na Rais Ruto mnamo Machi mwaka jana kabla ya Mahakama Kuu kuamua kuwa nyadhifa hizo ni haramu.
Marehemu alihudumu kwa muda mfupi kama CAS katika Wizara ya Fedha, wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta. Kisha aliegemea mrengo wa Rais Ruto hata baada ya kupoteza katika kura ya mchujo ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.
Miongoni mwa watu walioteuliwa kama CASs, na rais Ruto, waliohudhuria mazishi hayo ni Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura, aliyekuwa Mbunge Maalum Wilson Sossion, aliyekuwa Seneta Maalum Millicent Omanga, aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Isiolo Rehema Jaldesa, aliyekuwa Mbunge wa Starehe Charles Njagua na aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Tana River Rehema Hassan.
Wengine waliohudhuria ni Bw Amos Chege na Ann Wanjiku.
Juzi Bw Chege aliteuliwa kuwa mwanachama cha Tume ya Kusimamia Usafishaji wa Mto Nairobi (NRC) pamoja na Bi Omanga aliyekataa uteuzi huo.
Bw Njagua alisema wameunda kundi la mtandao wa WhatsApp kuwaleta pamoja kuisukuma serikali iwatunuku nyadhifa baada ya kupoteza nafasi za CASs.
“Kabla ya Nkatha kufa, tulikuwa tukitembeleana kutaka kujua ikiwa mmoja wetu aliteuliwa serikalini. Tulikuwa tukipekuwa matoleo mbalimbali ya gazeti rasmi ya serikali kutaka kujua ikiwa mmoja wetu ameteuliwa serikalini,” akasema.
Bw Njagua akaendelea: “Juzi niliona jina la Nkatha katika orodha ya watu walioteuliwa kuwa makamishna. Nilimpigia simu nimpongeze lakini baadaye nikagundua kuwa haikuwa yeye.”
Bw Mwaura alisema 15 kati ya watu 50 walioteuliwa CASs wametunukiwa nyadhifa zingine serikalini.
“Kama mwenyekiti wa kundi hili, nilikuwa wa kwanza kuteuliwa. Wengine 14 waliteuliwa mabalozi na mabalozi wasaidizi. Nina uhakikisha kuwa wale waliosalia watapata kazi serikalini,” Bw Mwaura akasema.
Msemaji huyo wa serikali alielezea jinsi walijitetea wateuliwe kama CASs baada ya kuundwa kwa serikali ya Kenya Kwanza lakini mahakama ikazima ndoto zao.
“Tungehakikisha tunahudhuria mikutano ya Rais kote nchini ili tuoenekane katika ngazi za serikali. Katika siasa ikiwa hauonekani unasahulika,” Bw Mwaura akasema.
Wanasiasa hao walimtaka Rais Ruto kumteua mmoja jamaa za Nkatha serikalini kujaza nafasi yake.
“Kwa kuwa nafasi ya marehemu Nkathi ingali serikali, namwomba Rais ateue bintiye au mwanawe wa kiume,” Bw Njagua akasema.
Imetafsiriwa na Charles Wasonga