WAZEE wa jamii ya Luhya Desemba 11, 2025 walifanya kikao cha mashauriano na viongozi wakuu wa ODM kutoka eneo la Magharibi ili kujadili mustakabali wa jamii hiyo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Wazee hao walihoji Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, na Naibu Kiongozi wa chama hicho, Godfrey Osotsi, wakitaka kufahamu nafasi ya jamii ya Waluhya ndani ya ODM baada ya enzi za aliyekuwa Waziri Mkuu, marehemu Raila Odinga.

Taarifa ambazo Taifa Leo imepata zinaonyesha kuwa wazee walitaka ufafanuzi kuhusu hali ndani ya chama na madai ya kutengwa kwa jamii hiyo katika serikali Jumuishi.

Wakiongozwa na Mzee Patrick Wangamati na aliyekuwa rais Noah Wekesa, wazee walilalamika kuwa hawajawahi kupewa taarifa zozote kuhusu makubaliano ya kuunda serikali jumuishi, licha ya jamii hiyo kuwa miongoni mwa wafuasi sugu wa ODM.

Aidha, mkutano huo uliibua maswali kuhusu kile walikitaja kuwa njama za kisiasa dhidi ya Bw Sifuna kutokana na msimamo wake mkali wa kupinga makubaliano kati ya Bw Odinga na Rais William Ruto, msimamo ambao umemfanya akinzane na baadhi ya viongozi wa chama wanaounga mkono mpango huo.

“Tuliwaita viongozi hawa wawili wakuu wa ODM watupe taarifa kuhusu yanayoendelea ndani ya chama. Sehemu kubwa ya jamii yetu iko ODM, kwa hivyo kinachoendelea humo kinatuhusu. Hakuna mtu aliyetuambia chochote kuhusu mpango wa serikali jumuishi,” alisema Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wazee wa Luhya, Fred Omondi.

Baadhi ya maafisa wa juu wa ODM walioingia serikalini kupitia mpango huo ni John Mbadi (Waziri wa Fedha ), Ali Hassan Joho (Madini na Uchumi wa Bahari), Opiyo Wandayi (Kawi na Petroli), Wycliffe Oparanya (Ushirika) na Beatrice Askul (Maeneo Kame).

Mbali na Bw Oparanya, ukanda wa Magharibi pia una Musalia Mudavadi ( Mkuu wa Mawaziri) na Deborah Barasa (Waziri wa Mazingira). Kadhalika, Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, anatoka katika eneo hilo.

Bw Wekesa alisema mkutano huo ni sehemu ya juhudi za jamii kuungana upya kabla ya uchaguzi wa 2027 kutokana na kugawanyika kwao kisiasa mara kwa mara, hali inayowanyima nguvu katika majadiliano kitaifa.

“Sisi ni jamii ya pili kwa idadi nchini, lakini hatuchukuliwi kwa uzito. Tutahakikisha tunaenda katika uchaguzi tukiwa kitu kimoja. Huu ni mwanzo tu wa mikutano zaidi ijayo,” alisema Bw Wekesa.

Katika taarifa ya pamoja baada ya mkutano wazee walisema wameamua kuhimiza umoja ili jamii “isitengwe pembeni”.

“Ni kwa maslahi binafsi ya baadhi ya wanasiasa kugawanya jamii ya Waluhya ili tusinufaike na nguvu ya idadi ambayo tumekirimiwa na Mungu,” ilisema taarifa hiyo.

Wazee walisema wameunda kikundi cha viongozi, wazee, wataalamu na wafanyabiashara ili kuanzisha mazungumzo ya kina ndani ya jamii na pia na jamii nyingine za Kenya.

“Hii ndio njia ya haki ya kupata mwafaka ili tusigeuke kuwa waathiriwa wa mabroka wa kisiasa wanaotumia nguvu ya idadi ya Waluhya kwa maslahi yao binafsi,” waliandika.

Akizungumza kando ya mkutano huo, Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka alitoa wito kwa viongozi wa jamii ya Mulembe kuweka tofauti zao kando na kuungana katika ajenda moja ya pamoja ya eneo la Magharibi.