Yawezekana Ruto anaandaa Gideon kumrithi Bonde la Ufa
MPANGO wa Rais William Ruto wa kumshirikisha Mwenyekiti wa KANU, Gideon Moi katika baraza lake la mawaziri limefasiriwa kama yenye malengo kadhaa ya kufaidi rais kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 na baadaye 2032.
Uchunguzi wa meza ya Jamvi la Siasa umebaini kwamba lengo kubwa zaidi la Dkt Ruto ni kumwandaa Gideon kuwa mrithi wake wa kisiasa katika jamii ya Kalenjin atakapostaafu baada ya kukamilisha muhula wake wa pili.
Hii ni baada ya Rais kuonekana kupoteza imani ya wanasiasa chipukizi kutoka jamii hiyo, ambao amekuwa wakikuza kwa ajili ya kumrithi.
“Japo lengo la muda mfupi la Rais Ruto kumwingiza Gideon kwapani mwake ni kumwondolea aibu kwa kumshinda mgombeaji wa UDA Vincent Chemitei katika uchaguzi mdogo wa useneta Baringo, lengo la muda mrefu ni kumwaandaa kuwa mrithi wake 2032,” anasema mchanganuzi wa kisiasa Philip Chebunet.
Kulingana na mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Moi, Rais ameng’amua kwamba, japo hafifu, Kanu bado inayo “mizizi katika Rift Valley na maeneo mengi nchini; mizizi ambayo ikifufuliwa inaweza kuzalisha miti”
“Kumshirikisha Gideon serikalini kutaipa Kanu nguvu mpya kisiasa na kifedha hali ambayo itamfaidi Rais katika uchaguzi mkuu ujao na hata ile ya 2032,” akasema.
“Japo, Gideon sio mwanasiasa machachari na mwenye kipawa cha usema alivyo Ruto, ni mkwasi na anatoka familia ya “dynasty” inayojulikana. Hii ni tofauti na wanasiasa chipukizi kutoka jamii ya Kalenjin ambao wangali kujijengea jina nje ya maeneo walikozaliwa,” anaongeza Dkt Chebunet.
Kwa upande wake, Gitile Naituli anasema kuwa kwa kumtoa Gideon kutoka mwavuli wa upinzani, kwanza amepunguza upinzani wowote dhidi yake katika eneo la jamii yake ya Kalenjin kuelekea 2027.
“Pili, atamjenga ili awe mrithi wake kama kinara wa siasa katika jamii hiyo atakapostaafu 2032. Kwa hivyo ni wazi kuwa hizi karata ambazo Rais Ruto anapania kucheza kwa kumteua Gideon kuwa Waziri zinalenga kusaidia kisiasa,” anaeleza Profesa Naituli akiongea kuwa inatarajiwa kuwa hatua pia itawatie moyo wafuasi wa Kanu Baringo kumuunga mkono mgombeaji wa UDA katika uchaguzi mdogo wa Novemba 27.
Alipohutubia viongozi wa mashinani wa Kanu katoka Baringo nyumba kwa Gideon Kabarak, Septemba 12, Rais Ruto alifichua atamshirikisha mwanasiasa huyo katika serikali jumuishi.
“Hivi karibuni vyama vya Kanu na UDA vitakutana kujadili namna kufanikisha ushirikiano huu. Mimi ndiye nilimtafuta Gideon ili anasaidie kuisukuma Kenye mbele kimaendeleo. Lengo letu ni kuhakikisha sote tunashirikiana kufanikisha ajenga ya kupandisha Kenya hadhi kuwa taifa iliyostawi zaidi,” akaeleza.
Na wiki hii Katibu Mkuu wa Kanu George Wainaina alithibitisha kuwa makundi ya kiufundi kutoka vyama hivyo mawili yamekuwa yakikutana kujadili ushirikiano huo.
“Lakini alivyosema Rais, ushirikiano huo ni wa kuendeleza nchi wala sio kuwatunuku viongozi fulani. Vile vile, ushirikiano huu haulengi kuifanya Kanu kupoteza sura yake. Kanu itasalia kuwa chama huru,” akaongeza.