MakalaSiasa

JAMVI: Mkakati mpya anaotumia Ruto kuhakikisha anatwaa urais 2022

September 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 3

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto sasa amewakumbatia madiwani katika juhudi zake za kuhakikisha kuwa anajipatia uungwaji mkono katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Naibu wa Rais amekuwa akikutana na madiwani kutoka kaunti mbalimbali takribani kila wiki.

Hii inatokana na ukweli kwamba madiwani ndio wako karibu na wananchi mashinani ikilinganishwa na wabunge au maseneta, hivyo wako katika nafasi bora ya kumpigia debe na kumsaidia kupenya vijijini.

“Madiwani ndio walio uwezo wa kushughulikia mahitaji ya wananchi katika ngazi za vijijini. Wanatangamana na kushauriana na wananchi na kujua miradi wanayohitaji,” akasema Bw Ruto kupitia mtandao wa Twitter.

Kundi la hivi karibuni kukutana na Bw Ruto ni madiwani kutoka Kaunti ya Nakuru ambao walifanya mkutano wa faragha nyumbani kwake katika mtaa wa Karen, Nairobi, Jumatano.

Madiwani wa Nakuru wakiongozwa na Naibu Gavana Eric Korir na Spika wa Bunge la Kaunti Joel Kairu waliahidi kumuunga mkono 2022.

Katika mkutano huo, Naibu wa Rais alisema kuwa anataka kushirikiana na madiwani moja kwa moja katika juhudi za kuhakikisha kwamba anajipatia uungwaji mkono katika maeneo ya mashinani.

“Naibu wa Rais ameamua kushirikiana na madiwani moja kwa moja kutokana na ukweli kwamba baadhi ya wabunge hawaendi katika maeneobunge yao wanapiga domo tu wakiwa Nairobi,” akasema mbunge kutoka kambi ya Bw Ruto aliyeomba jina lake libanwe.

Bw Ruto alikutana na madiwani hao Nakuru siku moja baada ya kufanya kikao na madiwani kutoka kaunti za Vihiga na Murang’a.

Jumanne asubuhi, Bw Ruto alikutana na madiwani kutoka Kaunti ya Vihiga na kisha mchana akafanya kikao cha faragha na viongozi wa Murang’a waliokuwa wameandamana na Mwangi Wa Iria.

Viongozi kutoka Kaunti ya Murang’a wamekuwa wakimshinikiza Bw Ruto kumteua Gavana Wairia ambaye anahudumu muhula wa pili, kuwa mwaniaji mwenza wake 2022.

Wiki iliyopita Naibu wa Rais alikutana na madiwani wa Kaunti ya Kirinyaga walioandamana na Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru.

Madiwani hao waliahidi kumuunga mkono haswa ikiwa atamtaja Bi Waiguru kuwa mwaniaji mwenza wa urais katika uchaguzi wa 2022.

Naibu wa rais pia amewahi kukutana na madiwani kutoka kaunti za Kakamega, Trans Nzoia, Embu, Meru, Kajiado, Narok na baadhi ya Kaunti za Pwani.

“Ufichuzi uliotolewa na Seneta wa Siaya James Orengo kuwa chama cha ODM kinamwandaa kiongozi wake Raila Odinga kuwania urais 2022, umemchochea Bw Ruto kubuni mapema mikakati ya kujipatia ushawishi katika maeneo ya mashinani,” mbunge ambaye ni mwendani wa Bw Ruto akaambia Taifa Jumapili.

Baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara wenye ushawishi, haswa kutoka maeneo ya Mlima Kenya, wamekuwa wakimtembelea Bw Odinga katika afisi yake iliyoko katika jumba la Capitol Hill, Nairobi tangu kusalimiana na kuafikiana kushirikiana mnamo Machi 9.

Licha ya Bw Odinga kusisitiza kuwa mikutano yake na watu wenye ushawishi kutoka eneo la Mlima Kenya, inalenga kuunganisha Wakenya na haina uhusiano na siasa, mrengo wa Bw Ruto inafasiri umeshawishika kuwa ina uhusiano na siasa za 2022.

Wanasiasa wa eneo la Mlima Kenya wamegawanyika kuhusiana na siasa za 2022. Baadhi yao wanaounga mkono Bw Ruto wamekuwa wakisisitiza kuwa hawatamsaliti Bw Ruto ambaye ‘alimsaidia’ Rais Kenyatta kuwa kuingia Ikuluni katika uchaguzi wa 2013 na 2017.

Ukimya wa Rais Kenyatta kuhusiana na siasa za 2022 pia umesababisha baadhi ya wanasiasa kutoka Mlima Kenya kusalia kimya na kutotangaza msimamo wao ikiwa wanamuunga mkono Bw Ruto au la.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa mbinu ya Bw Ruto kukumbatia madiwani huenda ikazaa matunda kwa sababu viongozi hao hutangamana na wananchi mara kwa mara ikilinganishwa na wabunge, maseneta.

“Madiwani wana ushawishi mashinani kwani wao hukutana na wananchi mara kwa mara kusikiza matakwa yao na kuyashughulikia. Hivyo, Bw Ruto akipitisha miradi ya maendeleo kwa madiwani bila shaka atakubalika vijijini,” anasema wakili Felix Otieno.

Lakini mwadhiri Tom Mboya anasema kuwa hatua hiyo itakuwa na mafanikio kidogo kwani hata wengi wa madiwani walitoweka mara tu baada ya kuchaguliwa hawatangamani na wananchi.